24. Kuuliza namna ya Sifa za Allaah ni Bid´ah iliyozusha Ahl-ul-Bid´ah

Vilevile Allaah anasifika kulingana juu ya ´Arshi. Hili limetajwa sehemu saba katika Qur-aan; Twaaha, al-A´raaf, Yuunus, ar-Ra´d, al-Israa´, Luqmaan, as-Sajdah na al-Hadiyd. Zote zimethibiti.

Kulingana (al-Istiwaa´) maana yake ni kuwa juu na kungatika. Kulingana juu ya ´Arshi maana yake ni kwamba yuko juu na amengatika kwenye ´Arshi. Yeye Ndiye ambaye yuko juu ya viumbe Wake wote. ´Arshi ndio sakafu ya viumbe. Yeye Allaah (Subhaanah) yuko juu ya ´Arshi. Ni kulingana ambako kunalingana na utukufu Wake. Hakuna anayejua namna yake isipokuwa Yeye Pekee (Subhaanahu wa Ta´ala). Wakati Imaam Maalik bin Anas (Rahimahu Allaah), ambaye alikuwa ni mwanachuoni mkubwa wa al-Madiynah katika wakati wake na mmoja katika maimamu wane, alipoulizwa: “Ee Abu ´Abdillaah!

الرَّحْمَـٰنُ عَلَى الْعَرْشِ اسْتَوَىٰ

Mwingi wa Rahmah amelingana juu ya ´Arshi.” (20:05)

Amelingana namna gani?” Ghafla uso wake ukageuka kwa mshangao mkubwa aliopata juu ya swali hili. Kisha baada ya hapo akasema:

“Kulingana kunajulikana… “

Bi maana kulingana kunajulikana kwamba ni kuwa juu na kungatika.

“… namna haijulikani. Kuamini hilo ni wajibu na kuulizia hilo ni Bid´ah. Mimi naona kuwa wewe ni mtu muovu” kisha baada ya hapo akaamrisha atolewe.”[1]

Vivyo hivyo ndivyo alivyosema Sufyaan ath-Thawriy, al-Awzaa´iy, Imaam Ahmad, Imaam ash-Shaafi´iy, Ishaaq bin Raahuuyah na maimamu wengine wa Uislamu. Mlango ni ule ule mmoja: maana ya kulingana inajulikana. Maana yake ni kuwa juu na kungatika. Namna haijulikani. Kwa msemo mwingine hakuna anayejua namna alivyolingana isipokuwa Yeye Pekee (Subhaanahu wa Ta´ala). Kuamini hilo ni wajibu, kwa sababu Allaah ndiye amejielezea Mwenyewe. Kuulizia namna ni Bid´ah iliyozuliwa na wanafalsafa miongoni mwa Jahmiyyah, Mu´tazilah na wengineo.

Hali kadhalika inatakiwa kusema juu ya sifa zingine ya kwamba huruma, radhi, ghadhabu, uwezo, mkono na mguu vyote vinajulikana. Kuhusu namna yake haijulikani. Hatujui namna ya huruma Wake ulivyo, ghadhabu Zake, mkono Wake, mguu Wake na macho Yake vyote hatujui namna vilivyo na wala hatuviingilii kwa ndani. Bali tunavithibitisha na kuvipitisha kama vilivyokuja. Tunasema kuwa Yeye ni Mwenye kusikia na Mwenye kuona, tunasema kuwa ni Mwenye mikono miwil kama alivyosema (Ta´ala):

بَلْ يَدَاهُ مَبْسُوطَتَانِ

“Bali Mikono Yake imekunjuliwa.” (05:64)

مَا مَنَعَكَ أَن تَسْجُدَ لِمَا خَلَقْتُ بِيَدَيَّ

“Nini kilichokuzuia usimsujudie Niliyemuumba kwa Mikono Yangu?” (38:75)

Vilevile imekuja katika Hadiyth Swahiyh inayosema:

“Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) aliyetukuka Aweke Mguu Wake kisha pawe sawa. Hapo ndio itasema ­­“Inatosha! Inatosha!”[2]

Vilevile Yeye (Subhaanahu wa Ta´ala) ameeleza kuwa anamghadhibikia yule mwenye kumuasi na humridhia yule mwenye kumtii na anawarehemu waja Wake. Zote hizi ni katika sifa Zake (Jalla wa ´Alaa):

“Allaah Anawacheka watu wawili ambapo mmoja wao kamuua mwenzake. Halafu wote wawili wanaingia Peponi.”[3]

Kughadhibika Kwake, kuridhia Kwake, kusikia Kwake, kuona Kwake na sifa zake zingine zote zinalingana na Yeye peke yake na wala hashabihiani na viumbe Vyake kwa chochote katika hayo kutokana na kanuni isemayo:

لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ ۖ وَهُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ

“Hakuna chochote kinachofanana Naye – Naye ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona.” (42:11)

Ahls-Sunnah wal-Jamaa´ah wanathibitisha Aayah na Hadiyth zinazozungumzia sifa, uthibitishaji ambao hamna ndani yake ufananishaji na wakati huo huo wanamtakasa Allaah (Jalla wa ´Alaa) kufanana na viumbe Wake utakaso usiokuwa ndani yake na ukanushaji. Inahusiana na ukanushaji ulioambatana na uthibitishaji.

[1] ad-Daarimiy katika “ar-Radd ´alaa al-Jahmiyyah”, uk.33, al-Lalakaa´iy katika “Sharh Usuul I´tiqaad Ahl-is-Sunnah wal-Jamaa´ah” (02/398), al-Bayhaqiy katika “Asmaa´ was-Swifaat” (867), Ibn ´Abdi-Barr katika “at-Tamhiyd” (07/151). Haafidhw Ibn Hajar amesema katika “Fath-ul-Baariy” (13/407) ya kwamba mlolongo wa wapokezi wake ni nzuri (Jayyid).

[2] al-Bukhaariy (4849) na Muslim (2846).

[3] al-Bukhaariy (2826) na Muslim (1890).

  • Mfasiri: Firqatunnajia.com