24. Dalili ya ishirini na mbili kutoka katika Sunnah kwamba Allaah yuko juu ya viumbe


22- Abul-Faraj Yahyaa bin Mahmuud ath-Thaqafiy ametuhadithia: Babu yangu Haafidhw Ismaa´iyl bin Muhammad bin al-Fadhwl ametuhadithia: Abul-Hasan ´Aliy bin Muhammad bin Muhammad bin al-Khatwiyb al-Anbaariy ametuhadithia: Abu ´Abdillaah al-Husayn bin ´Umar bin Burhaan ametuhadithia: Ja´far bin Muhammad al-Khuldiy ametuhadithia: Ibraahiym bin ´Abdillaah bin Muslim ametuhadithia: Sahl bin Bakkaar ametuhadithia: ´Abdus-Salaam ametuhadithia, kutoka kwa ´Ubaydah al-Hujaymiy aliyeeleza kwamba Abu Jurayy Jaabir bin Sulaym alisema:

“Nilikaa kwenye ngamia wangu na kuanza kuelekea Makkah ili kumpata. Nikampigisha magoti nje ya mlango wa msikiti. Tahamaki nikamuona (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameketi, amevaa koti likiwa na misitari myekundu. Nikasema: “Amani ya Allaah iwe juu yako, ee Mtume wa Allaah!” Akajibu: “Na wewe pia.” Nikasema: “Sisi watu wa shambani ni watu tusiokuwa na nidhamu. Nifunze maneno ambayo Allaah ataninufaisha kwayo.” Akasema: “Sogea karibu. Ulisemaje?” Nikasema: “Sisi watu wa shambani ni watu tusiokuwa na nidhamu. Nifunze maneno ambayo Allaah ataninufaisha kwayo.”Akasema: “Mche Allaah. Usidharau tendo jema lolote, hata kama ni kumwaga kilichobaki kwenye chombo chako kwa mtu ambaye amekuomba maji. Ukikutana na ndugu yako basi muonyeshe uso wenye bashasha. Tahadhari na kuvaa nguo yenye kuvuka kongo mbili za miguu. Kwani hicho ni kiburi na Allaah hapendi kiburi. Mtu akikutana kwa kitu anachokijua kwako, basi wewe usimtukane kwa kitu unachokijua kwake. Allaah (Ta´ala) atakuandikia wewe thawabu na atamwandikia yeye dhambi. Usitukane chochote katika vile alivyokupa Allaah (´Azza wa Jall).” Abu Jurayy amesema: “Ninaapa kwa Yule aliyeishika nafsi ya Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) sikupatapo kutukana kondoo wangu wala ngamia wangu.” Nikasema: “Umetaja kuvaa nguo isiyovuka kongo mbili za miguu. Wakati mwingine mtu anaweza kuwa na kidonda au kitu ambacho anakionea haya kukionyesha.” Akasema: “Hakuna neno mpaka kwenye muundi wa mguu au mpaka kwenye kongo mbili za miguu. Kuna mtu katika wale waliokuwa kabla yenu ambaye alivaa koti mbili na akawa na akatembea kwa majivuno ambapo Allaah akamtazama kutoka juu ya ´Arshi Yake, akamchukia na akaamrisha ardhi immeze. Yuko ndani ya ardhi. Chunga adhabu ya Allaah (´Azza wa Jall).”[1]

[1] adh-Dhahabiy amesema:

”Cheni ya wapokezi wake ni laini.” (al-´Uluww, uk. 36)

  • Mhusika: Imaam Muwaffaq-ud-Diyn bin Qudaamah al-Maqdisiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ithbaatu Swifat-il-´Uluww, uk. 104-105
  • Imechapishwa: 04/06/2018