22. Sharti ya kwanza ya Shahaadah: Ujuzi


Sharti za “Nashuhudia ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah”. Katika kushuhudia ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah ni lazima kutimie sharti saba. Haitomfaa kitu mwenye kuitamka isipokuwa kwa kuyakusanya. Nayo ni kama ifuatavyo kwa njia ya ujumla:

Sharti ya kwanza: Ujuzi ambao kinyume chake ni ujinga.

Sharti ya pili: Yakini ambayo kinyume chake ni shaka.

Sharti ya tatu: Kuikubali ambako kinyume chake ni kuikataa.

Sharti ya nne: Unyenyekevu ambao kinyume chake ni kusita.

Sharti ya tano: Ukweli ambao kinyume chake ni uongo.

Sharti ya sita: Kumtakasia nia Allaah ambako kinyume chake ni shirki.

Sharti ya saba: Mapenzi ambayo kinyume chake ni chuki.

Kuhusu upambanuzi wake ni kama ifuatavyo:

1- Sharti ya kwanza: Ujuzi. Kinacholengwa ni kujua maana yake inayokusudiwa, kinachokanushwa na kinachothibitishwa mambo ambayo yanapingana na kuyajahili hayo. Amesema (Ta´ala):

إِلَّا مَن شَهِدَ بِالْحَقِّ وَهُمْ يَعْلَمُونَ

“… isipokuwa yule aliyeshuhudia kwa haki nao wakawa wanajua.”[1]

Bi maana wameshuhudia ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah. Maneno Yake:

“wa hum yaalamuna”

kwa mioyo yao yale yaliyoshuhudiwa kwa ndimi zao. Haitomfaa kitu endapo atatamka na wakati huohuo hajui maana yake. Kwa sababu hakuamini yale yanayofahamishwa nalo.

[1] 43:86

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ´Aqiydat-ut-Tawhiyd, uk. 48
  • Imechapishwa: 12/02/2020