Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Ukiambiwa: “Ni misingi ipi mitatu ambayo ni wajibu kwa mtu kuijua?” sema: “Mja kumjua Mola Wake…

MAELEZO

Misingi ni wingi wa “msingi”. Msingi ni kitu ambacho mtu anajengea juu yake. Miongoni mwa hayo ni mfano wa msingi wa ukuta na mizizi ya mti ambayo matawi yanakulia. Allaah (Ta´ala) amesema:

أَلَمْ تَرَ كَيْفَ ضَرَبَ اللَّـهُ مَثَلًا كَلِمَةً طَيِّبَةً كَشَجَرَةٍ طَيِّبَةٍ أَصْلُهَا ثَابِتٌ وَفَرْعُهَا فِي السَّمَاءِ

“Je, huoni vipi Allaah amepiga mfano wa neno zuri kama mti mzuri mizizi yake ni thabiti na matawi yake yanafikia mbinguni.” (Ibraahiym 14 : 24)

Misingi hii mitatu ambayo mtunzi wa kitabu (Rahimahu Allaah) ametaja, ni misingi ambayo mtu ataulizwa ndani ya kaburi: Ni nani Mola Wako? Ni ipi dini yako? Ni nani Mtume wako?

Mtunzi wa kitabu (Rahimahu Allaah) ametaja misingi hii mitatu kwa njia ya swali ili amzindue mtu juu yake. Hili linajulisha kuwa ni suala kubwa na misingi mikubwa. Amesema kuwa hii ni misingi mitatu ambayo ni wajibu kwa mtu kuijua, kwa sababu ni misingi hii ambayo mtu ataulizwa ndani ya kaburi. Wakati ndugu na jamaa zake watakapomzika na kumwacha, atajiwa na Malaika wawili ambao watamkaza na kumuuliza:

“Ni nani Mola Wako? Ni ipi dini yako? Ni nani Mtume wako?”

Muumini atajibu:

“Mola Wangu ni Allaah, Uislamu ndio dini yangu na Muhammad ndio Mtume wangu.”

Kuhusu yule mwenye mashaka na mnafiki watasema:

“Eeh, eeh. Sijui. Nilisikia watu wanasema kitu hivyo na mimi nikakisema.”

Ujuzi wa kumjua Allaah inakuwa kwa njia mbalimbali:

1- Miongoni mwazo ni kutazama na kuzingatia viumbe vya Allaah (´Azza wa Jall). Hilo linapelekea kuweza kumjua na kujua nguvu Zake kubwa na ukamilifu wa uwezo, hekima na rehema Zake. Allaah (Ta´ala) amesema:

أَوَلَمْ يَنظُرُوا فِي مَلَكُوتِ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَمَا خَلَقَ اللَّـهُ مِن شَيْءٍ

“Je, hawatazami ufalme wa mbingu na ardhi na vitu alivyoviumba Allaah.” (al-A´raaf 07 : 185)

قُلْ إِنَّمَا أَعِظُكُم بِوَاحِدَةٍ ۖ أَن تَقُومُوا لِلَّـهِ مَثْنَىٰ وَفُرَادَىٰ ثُمَّ تَتَفَكَّرُوا

“Sema: “Hakika nakuwaidhini kwa jambo moja tu: msimame kwa ajili ya Allaah wawili wawili au mmoja mmoja, kisha mtafakari.” (Sabaa´ 34 : 46)

إِنَّ فِي خَلْقِ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَاخْتِلَافِ اللَّيْلِ وَالنَّهَارِ لَآيَاتٍ لِّأُولِي الْأَلْبَابِ

“Hakika katika kuumbwa mbingu na ardhi na kupishana usiku na mchana, bila shaka ni alama kwa wenye akili.” (Aal ´Imraan 03 : 190)

إِنَّ فِي اخْتِلَافِ اللَّيْلِ وَالنَّهَارِ وَمَا خَلَقَ اللَّـهُ فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ لَآيَاتٍ لِّقَوْمٍ يَتَّقُونَ

“Hakika katika kupishana usiku na mchana na alivyoviumba Allaah katika mbingu na ardhi, bila shaka ni alama kwa wanaomcha Allaah.” (Yuunus 10 : 06)

إِنَّ فِي خَلْقِ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَاخْتِلَافِ اللَّيْلِ وَالنَّهَارِ وَالْفُلْكِ الَّتِي تَجْرِي فِي الْبَحْرِ بِمَا يَنفَعُ النَّاسَ وَمَا أَنزَلَ اللَّـهُ مِنَ السَّمَاءِ مِن مَّاءٍ فَأَحْيَا بِهِ الْأَرْضَ بَعْدَ مَوْتِهَا وَبَثَّ فِيهَا مِن كُلِّ دَابَّةٍ وَتَصْرِيفِ الرِّيَاحِ وَالسَّحَابِ الْمُسَخَّرِ بَيْنَ السَّمَاءِ وَالْأَرْضِ لَآيَاتٍ لِّقَوْمٍ يَعْقِلُونَ

“Hakika katika kuumbwa mbingu na ardhi na kupishana usiku na mchana na merikebu zipitazo katika bahari viwafaavyo watu na aliyoteremsha Allaah kutoka mbinguni katika maji akahuisha kwavyo ardhi baada ya kufa kwake na akaeneza humo kila aina ya mnyama na mgeuko wa pepo na mawingu yanayotiishwa baina ya mbingu na ardhi ni alama kwa watu wenye akili.” (al-Baqarah 02 : 164)

2- Njia nyingine itayomfanya mja kuweza kumjua Mola Wake ni kwa kufikiria alama Zake za Kishari´ah. Alama Zake za Kishari´ah ni Wahy ambao Mitume (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam) waliokuja nao. Mtu anatakiwa kuzitazama alama hizi na yale manufaa makubwa ilizonazo. Manufaa haya viumbe hawawezi kujitosheleza kwayo, si duniani wala Aakhirah. Pindi mtu atakapozitazama, kuzizingatia na elimu na hekima ilizonazo na  akaona ile nidhamu yake na kuafikiana kwake na maslahi ya mja, basi kwa hilo mtu atapata kumjua Mola Wake (´Azza wa Jall). Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

أَفَلَا يَتَدَبَّرُونَ الْقُرْآنَ ۚ وَلَوْ كَانَ مِنْ عِندِ غَيْرِ اللَّـهِ لَوَجَدُوا فِيهِ اخْتِلَافًا كَثِيرًا

“Je, hawaizingatii Qur-aan? Na lau ingelikuwa imetoka kwa asiyekuwa Allaah, bila shaka wangelikuta ndani yake tofauti nyingi.” (an-Nisaa´ 04 : 82)

3- Njia nyingine ni ule ujuzi ambao Allaah (´Azza wa Jall) huingiza ndani ya moyo wa muumini katika kumtambua Allaah (Subhanaahu wa Ta´ala) mpaka inakuwa kana kwamba anamuona Mola Wake na macho yake. Mtume Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema wakati walipoulizwa na Jibriyl: “Ni nini Ihsaan?”:

“Ni kumuabudu Allaah kama vile unamuona. Ikiwa wewe humuoni, basi Yeye anakuona.”[1]

[1] al-Bukhaariy (4777), Muslim (8), Abu Daawuud (4681), at-Tirmidhiy (2738), Ibn Maajah (63) na Ahmad (1/27).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 44
  • Imechapishwa: 20/05/2020