22. Kuamini Mizani siku ya Qiyaamah

Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) amesema:

“Inatakiwa kuamini Mizani siku ya Qiyaamah. Hadiyth inasema:

“Mja atapimwa siku ya Qiyaamah na hatokuwa na uzito sawa na bawa la mbu.”[1]

Matendo ya waja yatapimwa, kama ilivyotajwa kwenye mapokezi. Yanatakiwa kuaminiwa na kuthibitishwa. Mwenye kurudisha hilo anatakiwa kupuuzwa na asijadiliwe.”

MAELEZO

Wanachuoni wametofautiana kama watu watapimwa viwiliwili vyao baada ya kukubaliana juu ya kupimwa kwa matendo siku ya Qiyaamah. Maoni sahihi ni kwamba mtu atapimwa yeye na matendo yake. Dalili ya hilo ni maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Ataletwa mtu mkubwa na mnene siku ya Qiyaamah. Hatokuwa na uzito mbele ya Allaah sawa na ubawa wa mbu. Someni:

فَلَا نُقِيمُ لَهُمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ وَزْنًا

“Hatutowasimamishia siku ya Qiyaamah uzito wowote.”[2][3]

Wakati ´Abdullaah bin Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) alipopanda juu ya mti ,….. wakashangazwa namna muundi wake ulivyo mwembamba ambapo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema:

“Mnashangazwa na wembamba wa muundi wake? Ninaapa kwa Allaah ni wenye uzito zaidi kwenye mizani kuliko Uhud.”[4]

Kuhusu kupimwa kwa matendo, zipo Hadiyth nyingi zinazofahamisha juu ya hilo ikiwa ni pamoja na ile Hadiyth ya kadi[5]. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَنَضَعُ الْمَوَازِينَ الْقِسْطَ لِيَوْمِ الْقِيَامَةِ فَلَا تُظْلَمُ نَفْسٌ شَيْئًا ۖ وَإِن كَانَ مِثْقَالَ حَبَّةٍ مِّنْ خَرْدَلٍ أَتَيْنَا بِهَا ۗ وَكَفَىٰ بِنَا حَاسِبِينَ

“Tutaweka mizani ya uadilifu siku ya Qiyaamah – hivyo nafsi haitodhulumiwa kitu chochote japo ikiwa uzito wa mbegu ya hardali Tutaileta. Inatosheleza Kwetu kuwa wenye kuhesabu.”[6]

Hadiyth inasema:

“Hakuna kitu kilicho na uzito zaidi kwenye Mizani kama tabia njema.”[7]

 “Kuna maneno mawili mepesi zaidi kwenye ulimi, mazito zaidi kwenye mizani na ni yenye kupendwa zaidi na Mwingi wa huruma:

سُبْحَانَ اللَّهِ ، وبِحَمْدِهِ سُبْحَانَ اللَّهِ الْعَظِيمِ

“Allaah ametakasika kutokamana na mapungufu na sifa zote njema ni Zake. Allaah, hali ya kuwa ametukuka, ametakasika kutokamana na mapungufu.”[8]

Hadiyth hizi ni Swahiyh.

Mizani na adhabu ya ndani ya kaburi yamekanushwa na Mu´tazilah. Ama Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah wameyaamini hayo.

[1] al-Bukhaariy (4729) na Muslim (2785).

[2] 18:105

[3] al-Bukhaariy (4729) na Muslim (2785).

[4] Ahmad (3991) na Ibn Hibbaan (7069). Ahmad Shaakir amesema: ”Cheni ya wapokezi wake ni Swahiyh.” al-Albaaniy ameitaja katika ”as-Silsilah as-Swahiyhah” (2750) na (3192).

[5] at-Tirmidhî (2639) na Ibn Maajah (4300). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy. Ahmad Shaakir amesema: ”Cheni ya wapokezi wake ni Swahiyh.”

[6] 21:47

[7] Abu Daawuud (4799) na at-Tirmidhiy (2003). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh-ul-Jaamiy´” (5726).

[8] al-Bukhaariy (6406) na Muslim (2694).

  • Mhusika: ´Allaamah Ahmad bin Yahyaa an-Najmiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Itmaam-ul-Minnah, uk. 111-113
  • Imechapishwa: 22/04/2019