22. Aina ya Tawassul zinazokubalika Kishari´ah

Tawassul imegawanyika mafungu mawili:

La kwanza: Tawassul iliyowekwa katika Shari´ah.

La pili: Tawassul iliyokatazwa.

Kuna aina mbalimbali za Tawassul ikiwa ni pamoja na zifuatazo:

1- Kufanya Tawassul kwa Allaah kwa majina na sifa Zake. Amesema (Ta´ala):

وَلِلَّـهِ الْأَسْمَاءُ الْحُسْنَىٰ فَادْعُوهُ بِهَا

”Allaah ana Majina mazuri kabisa, hivyo basi muombeni kwayo.”[1]

Kwa mfano muislamu aseme: “Ee Allaah! Ee ar-Rahmaan ar-Rahiym! Ee Hannaan! Ee Mannaan! Dhal-Jalaal wal-Ikraam! Nakuomba unipe kadhaa na kadhaa!”

2- Kufanya Tawassul kwa Allaah kwa kudhihirisha ufukara na kwamba unamuhitajia Yeye (Subhaanah). Ayyuub (´alayhis-Salaam) alisema:

أَنِّي مَسَّنِيَ الضُّرُّ وَأَنتَ أَرْحَمُ الرَّاحِمِينَ

“Hakika mimi nimepatwa na dhara, Nawe ndiye mbora zaidi wa kurehemu kuliko wengine wote wenye kurehemu.”[2]

Zakariyyah (´alayhis-Salaam) alisema:

قَالَ رَبِّ إِنِّي وَهَنَ الْعَظْمُ مِنِّي وَاشْتَعَلَ الرَّأْسُ شَيْبًا وَلَمْ أَكُن بِدُعَائِكَ رَبِّ شَقِيًّا

“Akasema: “Mola wangu! Hakika mimi mifupa imeninyong’onyea na kichwa kimeng’aa mvi na wala sikuwa mwenye kunyimwa katika kukuomba du’aa, ee Mola wangu.”[3]

Yuunus (´alayhis-Salaam) alisema:

أَن لَّا إِلَـٰهَ إِلَّا أَنتَ سُبْحَانَكَ إِنِّي كُنتُ مِنَ الظَّالِمِينَ

“Hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Wewe – utakasifu ni Wako, hakika mimi nilikuwa miongoni mwa madhalimu.”[4]

3- Kufanya Tawassul kwa Allaah kwa matendo mema. Kama ilivo katika maneno Yake (Ta´ala):

رَّبَّنَا إِنَّنَا سَمِعْنَا مُنَادِيًا يُنَادِي لِلْإِيمَانِ أَنْ آمِنُوا بِرَبِّكُمْ فَآمَنَّا ۚ رَبَّنَا فَاغْفِرْ لَنَا ذُنُوبَنَا وَكَفِّرْ عَنَّا سَيِّئَاتِنَا

“Mola wetu! Hakika sisi tumemsikia mwenye kuita anaita katika imani kwamba “Mwaminini Mola wenu” hivyo tukaamini.  Ee Mola wetu! Tusamehe dhambi zetu na tufutie makosa yetu.”[5]

Kama ilivo pia katika kile kisa cha watu watatu ambao walibanika pangoni ambapo wakamuomba Allaah kwa matendo mema na Allaah akawafariji[6]. Hiyo Tawassul iliyotajwa katika Aayah mbili tukufu ambayo imetumiwa kama dalili na wale wahalifu. Nako ni kujikurubisha kwa Allaah kwa matendo mema.

4- Kufanya Tawassul kwa Allaah (Ta´ala) kwa du´aa ya waja wema. Kama kwa mfano kwenda kwa mja mwema, aliyehai na kumwambia: “Niombee!” Kama alivosema Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuwaambia baadhi ya Maswahabah wake:

“Ndugu yangu! Usinisahau katika du´aa yako.”[7]

Kama ambavo vilevile Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum) walivokuwa wakimuomba wakimuomba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) awaombee kwa Allaah na wakiombana kuombeana wao kwa wao.

[1] 07:180

[2] 21:83

[3] 19:04

[4] 21:87

[5] 03:193

[6]al-Bukhaariy (04/369).

[7] Abu Daawuud (1498) na at-Tirmidhiy (3557).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bayaan Haqiyqat-it-Tawhiyd, uk. 37
  • Imechapishwa: 01/04/2019