Abu Ja´far at-Twahaawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

16- Ni Mwenye kusifika milele juu ya sifa Zake kabla ya kuumba Kwake.

MAELEZO

Hakuna kilichokuwa kabla ya Allaah. Hiyo ina maana kwamba ni Mwenye kusifiwa kwa sifa kamilifu. Sifa Zake ni za milele na za daima. Kama ambavo Yeye ni wa kwanza asiyekuwa na mwanzo vivyo hivyo sifa Zake (Subhaanah) ni za milele zenye kumfuata Yeye. Ni za milele kwa sababu Yeye ni wa milele. Haikuwahi kutokea kwamba kuna wakati alikuwa bila ya sifa Zake kisha zikaja kujitokeza huko baadaye, kama wanavosema wapotevu. Wanasema kwamba kuna wakati Alikuwa pasi na sifa kisha zikaja kujitokeza huko baadaye. Wanajenga hoja yao juu ya kwamba sifa za milele zinapelekea uwepo wa waungu wengi au wamilele wengi. Fikira yao hii ina maana ya kwamba kulikuwepo wakati ambapo Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) alikuwa ni mpungufu na akakamilika kikamilifu kwa sababu ndipo alipata sifa Zake. Allaah ametakasika na makosa kutokamana na yale wanayoyasema! Sifa za milele hazipelekei katika waungu wa milele. Kwani sifa sio kitu cha uinje; bali ni maana inayomwandama yule Mwenye kusifiwa nayo. Haina maana kwamba ni kitu cha kipekee kilichoko nje ya Yule mwenye kusifiwa nazo. Kwa mfano unaposema mtu fulani ni mwenye usikizi na uoni, mjuzi na mwenye uelewa, ina maana kwamba wanakuwa watu wengi? Sifa nyingi hazipelekei kuwepo kwa watu wengi kama wanavosema wapotevu. Kwa hivyo sifa za Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) hazina mwanzo kama ambavyo dhati Yake haina mwanzo. Ni Mwenye kusifiwa kuwa ni Muumbaji daima na siku zote.

Ama kuhusu matendo Yake (Subhaanah), ni za milele upande wa kimaumbile (قديمة النوع), zinajitokeza kutokana na matukio (حادثة الآحاد). Allaah alikuwa ni Mwenye kuzungumza kabla ya kuzungumza, alikuwa ni Mwenye kuumba kabla ya kuumba. Hata hivyo ni Mwenye kuzungumza na kuumba kwa sababu haya ni matendo yenye kujijadidi.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Mukhtaswarah ´alaal-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 42-43
  • Imechapishwa: 17/09/2019