Swali 21: Je, ni sawa kwa mtu kusoma majarida na magazeti misikitini ili kukemea makosa yaliyomo ndani kwa ajili ya kuwatahadharisha watu nayo?

Jibu: Majarida na magazeti yasikusanywe na kusomwa mbele za watu. Bali kukusanywe yale yaliyomo ndani yake na yachunguzwe pamoja na wanazuoni na wale wenye madaraka. Kuyaleta msikitini ni fedheha[1] na sio ukemeaji. Na huenda likamfurahisha yule mkemewaji[2]. Baadhi ya watu wanafurahia kosa kufanywa hivo ili liweze kuenea zaidi.

Kuna uwezekano vilevile wanafiki wakajiunga nao ili kueneza shari na batili hii. Ni jambo la khatari sana na huku sio kutatua mambo. Naapa kwa Allaah ya kwamba hii sio njia ya kutatua mambo.

Yule mwenye kutaka kuwanasihi waislamu, viongozi wao na watu wa kawaida asifanye hivo. Asikusanye makosa msikitini, kuyaweka hadharani na kuyaanikaHili ni jambo linalopelekea katika batili zaidi na kila mmoja kujichukulia hatua kwenye mikono yake. Kuna watu wengi wasiojua mambo haya. Kwa kufanya hivi unawafungulia njia na kuwakhabarisha mambo ambayo walikuwa hawayajui. Ukiongezea juu ya madhara yanayopatikana kwa kufanya hivo.

[1] Usisahau kwa kufanya hivi ni kukiuka ule utakatifu wa misikiti ya Allaah pale kunapoingizwa picha ndani yake. Muftiy wa hapo kabla wa Saudi Arabia Shaykh Muhammad bin Ibraahim Aalus-Shaykh (Rahimahu Allaah) amesema:

“Kuhusiana na hukumu ya kutumia picha, wanazuoni (Rahimahumu Allaah) wamesema waziwazi ya kwamba ni haramu kutumia picha ya viumbe wenye roho. Ni mamoja yakawa ndani ya misikiti au nje yake. Lakini ni jambo lisilokuwa na shaka yoyote juu ya kwamba ni kuyadharau makatazo ya Allaah na pia kutumia picha ndani ya nyumba Yake ni haramu zaidi na uhalifu mkubwa zaidi. Kubaya na ujasiri mkubwa zaidi ya huyo ni kutumia picha au kuyavaa wakati wa kuswali.” (Majmuu´-ul-Fataawaa (01/193))

[2] Mwenendo kama huu unawachochea wajinga na kuzijaza chuki nyoyo za raia dhidi ya watawala. Maovu na madhara makubwa yanayopatikana kwa mwenendo kama huu ni jambo liko wazi kabisa. Hamasa hizi za kisiasa zinapelekea katika vurugu na kukosekana utulivu. Kuzuia madhara kunatangulizwa kabla ya kuleta manufaa – ikiwa katika jambo lenyewe kunapatikana manufaa yoyote.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Ajwibah al-Mufiydah ´an As-ilat-il-Manaahij al-Jadiydah, uk. 63-64
  • Imechapishwa: 31/05/2023
  • mkusanyaji: Shaykh Jamaal bin Furahyaan al-Haarithiy