Tumeshatangulia kujua ni vipi tutatofautisha damu ya hedhi na damu ya ugonjwa. Pindi damu ni hedhi inakuwa na hukumu za hedhi na pindi damu ni ya ugonjwa inakuwa na hukumu ya damu ya ugonjwa. Tumeshatangulia kutaja hukumu muhimu zenye kufungamana na damu ya hedhi.

Ama kuhusiana na hukumu ya damu ya ugonjwa, ni hukumu zile zile kama katika kipindi cha utwaharifu. Hakuna tofauti kati ya mwanamke aliye na damu ya ugonjwa na mwanamke mtwaharifu isipokuwa katika mambo yafuatayo:

La kwanza: Ni wajibu kwake kutawadha katika kila swalah. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Kisha tawadha kwa kila swalah.”[1]

Ina maana ya kwamba asitawadhe kwa ajili ya kuswali swalah iliyowekewa nyakati maalum isipokuwa baada ya kuwa wakati wake umeshaingia. Hata hivyo ni sawa akatawadha pale anapotaka kuswali swalah ambayo haikuwekewa nyakati maalum.

La pili: Anapotaka kutawadha anatakiwa kuosha athari ya damu ukeni na kuweka pamba ili izuie damu. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Chukua pamba na weka kwenye tupu. Inaondosha damu.” Akasema: “Ni zaidi ya hivyo.” Mtume akasema: “Chukua kitambaa.” Akasema: “Ni zaidi ya hivyo.” Mtume akasema: “Izuie basi.”[2]

Damu itayotoka baada ya hapo haidhuru kitu. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisema kumwambia Faatwimah bint Abiy Hubaysh:

“Usiswali unapokuwa na hedhi. Baada ya hapo koga na utawadhe kwa kila swalah na uswali hata kama damu itadondoka kwenye jamvi.”[3]

La tatu: Jimaa. Wanachuoni wana maoni mbali mbali kuhusu jimaa kama hakukhofiwi dhambi. Maoni ya sawa ni kuwa inajuzu kabisa. Sio chini ya wanawake kumi walikuwa na damu ya ugonjwa katika zama za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), lakini si Allaah wala Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakuwakataza kufanya jimaa. Bali katika Kauli Yake Allaah (Ta´ala):

فَاعْتَزِلُوا النِّسَاءَ فِي الْمَحِيضِ ۖ وَلَا تَقْرَبُوهُنَّ حَتَّىٰ يَطْهُرْنَ

“… basi waepukeni wanawake [wanapokuwa] katika hedhi. Wala msiwakaribie [kujimai nao] mpaka watwaharike.” (02:222)

kuna dalili kuwa vinginevyo sio wajibu kuwaepuka. Ikiwa anapata kuswali basi vivyo hivyo anapata kufanya jimaa. Si sahihi kulinganisha jimaa yake na jimaa ya mwanamke mwenye hedhi kwa sababu hawako hata sawa kwa wale wenye kuonelea kuwa ni haramu. Ulinganisho hausihi ikiwa unakosa ufanano wa karibu.

[1] al-Bukhaariy (228).

[2] Abu Daawuud (287), at-Tirmidhiy (128) na Ahmad (6/382).

[3] Ahmad (6/42) na Ibn Maajah (624).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´UthaymiynImaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ad-Dimaa’ at-Twabiy´iyyah lin-Nisaa’ http://www.ibnothaimeen.com/all/books/article
  • Imechapishwa: 30/10/2016