20. Uwajibu wa kuwaraddi Ahl-ul-Bid´ah na kutowanyamazia


Imaam al-Barbahaariy (Rahimahu Allaah) amesema:

9- Tambua kupinda kutoka katika Njia iliyonyooka ni kwa namna mbili. Wa kwanza ni mtu ameteleza akapinda na Njia, pamoja na kuwa hakukusudia isipokuwa kheri. Kosa lake lisichukuliwe kama kiigizo, kwa sababu ni mwenye kuangamia. Mwingine, ameenda kinyume na haki na yale wachaji Allaah waliyokuwemo kabla yake. Huyo ni mpotevu na ni mwenye kuwapoteza wengine na ni shaytwaan aliyeasi katika Ummah huu. Yule mwenye kumfahamu ni lazima kwake kutahadharisha naye na kuwabainishia watu hali yake ili asije yeyote akatumbukia katika Bid´ah yake na akaangamia.

MAELEZO

Mtu kama huyu haijuzu kumnyamazia. Bali ni lazima kuliweka wazi jambo lake na kumfedhehesha mpaka watu waweze kutahadhari naye. Haitakiwi kusema kuwa watu wako huru, watu wana uhuru wa maoni, uhuru wa kuongea – kama inavyosemwa leo – kuheshimu mtazamo wa mtu mwengine, masuala hapa sio masuala ya maoni bali ni masuala ya kufuata. Allaah ametuonesha njia ya wazi na akatwambia kuifuata:

وَأَنَّ هَـٰذَا صِرَاطِي مُسْتَقِيمًا فَاتَّبِعُوهُ

“Hii ni njia Yangu iliyonyooka, hivyo basi ifuateni.” (06:153)

Yeyote ambaye anatujia na anataka sisi tutoke katika njia hii, sisi kwanza tutakataa. Pili si kwamba inatosheleza kule kukataa tu, bali ni lazima kwetu kubainisha na kutahadharisha watu naye. Si sawa kumnyamazia. Kwa kuwa tukimnyamazia watu watadanganyika naye na khaswa pale ambapo atakuwa ni mfaswaha wa kuzungumza na kuandika na utamaduni, watu watadanganyika naye na kusema huyu ni kigogo, bingwa wa wafikiriaji – kama hali ilivyo hivi sasa. Masuala haya ni khatari sana.

Hapa kuna uwajibu wa kumradi anayekwenda kinyume. Ni kinyume na wanavyosema baadhi ya watu kwamba Ruduud zinatakiwa kuachwa na kwamba watu waache na kila mmoja abaki na maoni yake na aheshimiwe. Wanasema kuna uhuru wa maoni na kuzungumza. Namna hii Ummah utaangamia. Salaf hawakuwanyamazia watu mfano wa hawa. Bali waliwafedhehesha na kuwaraddi. Walitambua khatari walionayo juu ya Ummah.

Sisi hatuwezi kunyamaza shari ya watu hawa. Ni lazima kwetu kubainisha yale aliyoyateremsha Allaah. Vinginevyo tutakuwa ni wenye kuficha wale ambao Allaah amesema juu yao:

إِنَّ الَّذِينَ يَكْتُمُونَ مَا أَنزَلْنَا مِنَ الْبَيِّنَاتِ وَالْهُدَىٰ مِن بَعْدِ مَا بَيَّنَّاهُ لِلنَّاسِ فِي الْكِتَابِ ۙ أُولَـٰئِكَ يَلْعَنُهُمُ اللَّـهُ وَيَلْعَنُهُمُ اللَّاعِنُونَ

“Hakika wale wanaoficha yale Tuliyoyateremsha katika hoja za wazi na uongofu baada ya kuwa Tumeyabainisha kwa watu katika Kitabu, hao anawalaani Allaah na wanalaaniwa na kila yule mwenye kulaani.” (02:159)

Jambo [laana hii] haimgusi mzushi peke yake. Inawagusa vilevile watu wanaowanyamazia. Lawama na adhabu inampata pia yule mwenye kuwanyamazia. Kwa kuwa ni wajibu kubainisha, kuwawekea watu wazi. Hii ndio kazi ya Ruduud za kielimu. Ruduud za kielimu zilizoenea hivi sasa kwenye maktabah za waislamu, zote zinaitetea Njia iliyonyooka na zinatahadharisha dhidi ya watu hawa. Tusipandikizwe fikra hizi; uhuru wa maoni, uhuru wa kuzungumza na kuwaheshimu wengine.

Sisi makusudio yetu sio kuwaingilia wengine. Makusudio yetu ni haki. Makusudio yetu sio kuwajeruhi watu na kutoa aibu za watu, makusudio yetu sisi ni kubainisha haki. Hii ni amana Allaah kawabebesha wanachuoni. Haijuzu kuwanyamazia mfano wa hawa. Lakini kwa masikitiko makubwa, lau kutatokea mtu akawapiga radd mfano wa watu kama hawa, watu wanasema kuwa wewe ni mtu mwenye papara na mababaisho mengine. Haya hayawazuii wanachuoni kuwabainishia watu shari ya walinganizi hawa wapotevu.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Sharh-is-Sunnah, uk. 47-49
  • Imechapishwa: 28/12/2017