20. Tawhiyd ndio jambo kubwa aliloamrisha Allaah

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Kubwa Aliloamrisha Allaah ni Tawhiyd, nayo ni kumpwekesha Allaah kwa ´ibaadah.

MAELEZO

Chimbuko la neno ´Tawhiyd` kilugha ina maana ya amepwekesha, anapwekesha na kukifanya kitu kuwa kimoja. Hili halihakikishwi isipokuwa kwa kukanusha na kuthibitisha; mtu akakanusha hukumu isiyokuwa kwa yule anayepwekeshwa, na wakati huohuo kumthibitishia nayo Yeye. Mfano wa hilo ni kwamba Tawhiyd ya mtu haikamiliki isipokuwa mpaka ashuhudie kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah. Hivyo anakuwa amekanusha uungu wote wa haki unaonasibishwa kwa wengine asiyekuwa Allaah (Ta´ala) na sambamba na hilo anauthibitisha kwa Allaah pekee.

Kwa mujibu wa istilahi mtunzi wa kitabu ameifasiri kwa kusema:

“Tawhiyd ni kumpwekesha Allaah kwa ´ibaadah.”

Maana yake ni kwamba kumwabudu Allaah Mmoja wa pekee. Usimshirikishi Yeye na chochote; usimshirikishi Yeye na Nabii yeyote aliyetumilizwa, Malaika aliyekaribu, raisi, mfalme wala yeyote katika viumbe. Bali mpwekeshe Yeye peke Yake hali ya kumpenda,  kumuadhimisha, shauku na khofu. Shaykh (Rahimahu Allaah) anachokusudia ni aina ya Tawhiyd ambayo Mitume walitumwa kwayo ili kuja kuihakikisha. Kwa sababu Tawhiyd sampuli hii ndio ambayo kulitokea kasoro kutoka kwa wafuasi wao.

Vilevile kuna tafsiri nyingine ya Tawhiyd iliyoenea, nayo ni:

“Ni kumpwekesha Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) kwa yale ambayo ni maalum Kwake.”

Kuna aina tatu za Tawhiyd:

1- Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah. Maana yake ni kuamini kwamba Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) yuko peke Yake katika kuumba, ufalme na kuyaendesha mambo. Allaah (Ta´ala) amesema:

اللَّـهُ خَالِقُ كُلِّ شَيْءٍ

“Allaah ni Muumbaji wa kila kitu.” (az-Zumar 39 : 62)

هَلْ مِنْ خَالِقٍ غَيْرُ اللَّـهِ يَرْزُقُكُم مِّنَ السَّمَاءِ وَالْأَرْضِ ۚلَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ

“Je, kuna muumbaji yeyote yule asiyekuwa Allaah anayekuruzukuni kutoka mbinguni na ardhi? Hapana mungu wa haki mwingine isipokuwa Yeye.” (Faatwir 35 : 03)

تَبَارَكَ الَّذِي بِيَدِهِ الْمُلْكُ وَهُوَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ

“Amebarikika ambaye mkononi Mwake umo ufalme Naye juu ya kila jambo muweza.” (al-Mulk 67 : 01)

أَلَا لَهُ الْخَلْقُ وَالْأَمْرُ ۗ تَبَارَكَ اللَّـهُ رَبُّ الْعَالَمِينَ

“Zindukeni! Ni Vyake pekee uumbaji na amri. Amebarikika Allaah, Mola wa walimwengu.” (al-A´raaf 07 : 54)

2- Tawhiyd-ul-Uluuhiyyah. Maana yake ni kumpwekesha Allaah (Subhaanayu wa Ta´ala) kwa ´ibaadah kwa njia ya kwamba mtu asimfanyie Allaah mshirika yeyote pamoja na Allaah ambapo akamwabudu na kujikurubisha Kwake kama jinsi anavyomuabudu Allaah na kujikurubisha Kwake.

3- Tawhiyd al-Asmaa´ was-Swifaat. Maana yake ni kuamini kuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) yuko peke Yake katika majina aliyojiita kwayo Mwenyewe na sifa alizojisifu kwazo Mwenyewe au kupitia ulimi wa Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hili linakuwa kwa kuthibitisha yale aliyojithibitishia Mwenyewe na kukanusha yale aliyojikanushia. Hayo yafanyike pasi na kupotosha, kukanusha, kuzifanyia namna wala kuzifananisha.

Aina anayokusudia hapa mtunzi ni Tawhiyd-ul-Uluuhiyyah. Aina hii ndio ambayo washirikina wamepotea na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akawapiga vita. Vilevile akahalalisha damu zao na mali, ardhi zao, majumba yao na wakati huohuo akawafanya mateka wanawake na vizazi vyao. Aina hii ya Tawhiyd ndio ambayo kwa kiasi kikubwa Mitume wanawatunza watu wao. Amesema (Ta´ala):

وَلَقَدْ بَعَثْنَا فِي كُلِّ أُمَّةٍ رَّسُولًا أَنِ اعْبُدُوا اللَّـهَ

“Kwa hakika Tulituma katika kila ummah Mtume [awaamrishe watu wake] kwamba: “Mwabuduni Allaah.” (an-Nahl 16 : 36)

´Ibaadah haisihi isipokuwa akifanyiwa Allaah (´Azza wa Jall) pekee. Yeyote mwenye kukosea katika Tawhiyd aina hii basi huyo ni mshirikina kafiri hata kama ataikubali Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah na Tawhiyd al-Asmaa´ was-Swifaat. Lau tutachukulia mfano mtu anakiri kikamilifu Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah na Tawhiyd al-Asmaa´ was-Swifaat, lakini mtu huyu anaenda kwenye kaburi na kumuabudu mtu mwenye kaburi hilo au kumuwekea nadhiri ili ajikurubishe kwake, mtu huyu anazingatiwa kuwa ni mshirikina kafiri ambaye atadumishwa Motoni milele. Allaah (Ta´ala) amesema:

إِنَّهُ مَن يُشْرِكْ بِاللَّـهِ فَقَدْ حَرَّمَ اللَّـهُ عَلَيْهِ الْجَنَّةَ وَمَأْوَاهُ النَّارُ ۖ وَمَا لِلظَّالِمِينَ مِنْ أَنصَارٍ

“Hakika mwenye kumshirikisha Allaah bila shaka Allaah atamharamishia Pepo na makazi yake yatakuwa ni Motoni na madhalimu hawatopata yeyote mwenye kunusuru.” (al-Maaidah 05 : 72)

Sababu ya Tawhiyd kuwa ndio jambo kubwa aliloamrisha Allaah ni kwa sababu ndio msingi ambao dini yote imejengwa juu yake. Kwa ajili hiyo ndio maana Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alianza ulinganizi wake kwayo katika kulingania katika dini ya Allaah na akaamrisha wajumbe wake waanze kwayo.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 39-41
  • Imechapishwa: 20/05/2020