20. Njia ambazo imetajwa mikono na macho

Mikono na macho iliyoegemezwa kwa Allaah (Ta´ala) katika Qur-aan na Sunnah imetajwa kwa njia ya umoja, uwili na wingi. Mfano wa umoja, Allaah (Ta´ala) amesema:

تَبَارَكَ الَّذِي بِيَدِهِ الْمُلْكُ وَهُوَ عَلَى كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ

“Amebarikika Ambaye mkononi Mwake umo ufalme Naye juu ya kila jambo ni muweza.”[1]

وَلِتُصْنَعَ عَلَى عَيْنِي

“… na ili ulelewe Machoni Mwangu.”[2]

Miongoni mwa mifano ya wingi, Allaah (Ta´ala) amesema:

أَوَلَمْ يَرَوْا أَنَّا خَلَقْنَا لَهُمْ مِمَّا عَمِلَتْ أَيْدِينَا أَنْعَامًا فَهُمْ لَهَا مَالِكُونَ

“Je, hawaoni kwamba Sisi tumewaumbia kutokana na yale iliyofanya mikono Yetu wanyama wa mifugo basi wao wanawamiliki.”[3]

تَجْرِي بِأَعْيُنِنَا

”Inatembea chini ya macho Yetu.”[4]

Miongoni mwa mifano ya uwili, Allaah (Ta´ala) amesema:

بَلْ يَدَاهُ مَبْسُوطَتَانِ

“Bali mikono Yake imekunjuliwa.”[5]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Pindi mja anaposimama kwa ajili ya kuswali, basi husimama kati ya macho mawili ya Mwingi wa rehema.”[6]

Hivi ndivyo ilivyotajwa katika “Mukhtaswar-us-Swawaa´iq al-Mursalah” kutoka kwa ´Atwaa´, kutoka kwa Abu Hurayrah, kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), bila ya kutaja marejeo[7].

Hata hivyo macho hayakutajwa ndani ya Qur-aan kwa njia ya mbili. Njia hizi tatu ndivyo mikono miwili na macho miwili yalivyotajwa katika Qur-aan na Sunnah.

Njia hizi tatu zinaoanishwa ifuatavyo:

Njia ya umoja haipingani na uwili wala wingi. Kwa sababu umoja uliyoegemezwa ni wenye kuenea na unafunika mikono na macho yote yaliyothibiti kwa Allaah sawa ikiwa ni njia ya umoja au wingi.

Kuhusiana na kujumuisha kati ya uwili na wingi, hakuna mgongano kabisa endapo tutasema kuwa uwili ndio idadi ya chini kabisa ya wingi. Na endapo tutasema kuwa herufi tatu ndio idadi ya chini kabisa ya wingi, na ndio kilichotangaa, basi tunajua kuwa lengo lililokusudiwa kwa wingi sio idadi ambayo ni zaidi ya mbili. Lengo lililolengwa ni utukuzwaji wenye kuendana na zile sifa zilizoegemezewa. Sifa hizi zimeegemezwa “Sisi” zikilenga utukuzwaji. Pindi Allaah alipotajwa kwa njia ya wingi, ni jambo lenye kuedana na sifa Zake pia zilizoegemezwa Kwake kutajwa kwa njia ya wingi. Wingi unatimiza makusudio ya utukuzaji na uadhimisho zaidi kuliko njia ya umoja na uwili. Hivyo basi, ikiwa Allaah na zile zifa anazoegemezewa zitatajwa kwa njia ya wingi, ndipo hupatikana utukuzaji ulio bora zaidi.

[1] 67:01

[2] 20:39

[3] 36:71

[4] 54:14

[5] 05:64

[6] al-´Uqayliy (01/70). Swahiyh wa mujibu wa Ibn-ul-Qayyim katika ”Mukhtaswar-us-Sawaa´iq al-Mursalah” (419), dhaifu kwa mujibu wa Ibn ´Uthaymiyn katika ”Sharh Swahiyh Muslim” (08/248) na dhaifu kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”adh-Dhwa´iyfah” (1024).

[7] Tazama ”as-Swawaa´iq” (1/256).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fath Rabb-il-Bariyyah, uk. 59-60
  • Imechapishwa: 01/05/2020