20. Mkono ulio juu ni bora kuliko mkono ulio chini

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Ee mwanaadamu! Ni bora kwako ukijitolea fadhila na ni shari kwako ukibaki nayo. Hulaumiwi kwa kuwa na cha kutosheleza. Anza na aliye chini yako. Mkono ulio juu ni bora kuliko mkono ulio chini.”[1]

Kuhusiana na maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam “Hulaumiwi kwa kuwa na cha kutosheleza”, inaweza kufahamika ya kwamba inalaumika mtu akiwa na zaidi ya cha kutosheleza na Allaah ndiye anajua zaidi. Amesema kuwa ni bora kwako kujitolea fadhila, jambo lisilokuwa na shaka yoyote. Kubaki nayo ni shari kabisa ikiwa mtu hajitolei katika yale ya wajibu. Ama kuhusu kujitolea mambo yaliyopendekezwa, ni kubaya kutokana na kule mtu kujikoseshea thawabu zisizokuwa na mfano katika dunia nzima.

108- Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mkono ulio juu ni bora kuliko mkono ulio chini. Mkono ulio juu unatoa na mkono ulio chini unaomba.”[2]

109- Baadhi ya Suufiyyah wamezifahamu Hadiyth hizi kinyume kabisa ingawa ni Swahiyh. Wanasema kuwa mkono ulio juu ni ule mkono wa mwombaji na mkono ulio chini ni ule mkono wa mtoaji. Hoja yao ni kwamba Allaah (Ta´ala) ndiye ambaye anampa mwombaji na kwa ajili hiyo ndio maana mkono wa mwombaji ndio uko juu. Pamoja na hivyo ni tafsiri ya kimakosa yenye kutupiliwa mbali na maana ya Hadiyth. Mkono wa mtoaji ndio ambao uko juu.

110- Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakuna mwenye kujitolea tende kutoka kwenye pato lake la halali isipokuwa Allaah anaipokea kwa mkono Wake wa kulia ambapo inakua kwenye kitanga cha Mwingi wa Rahmah mpaka inakuwa kubwa kuliko mlima.”[3]

111- Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Swadaqah huanguka kwenye kitanga cha Allaah kabla ya kuanguka kwenye kitanga cha mwombaji ambapo Anailea kama ambavyo mmoja wenu anavyomlea mtoto wake au mtoto wa ngamia wake.”[4]

Imepokelewa kutoka kwa Maalik, ath-Thawriy na Ibn-ul-Mubaarak ya kwamba Hadiyth hii na mfano wake zinatakiwa kupitishwa bila ya kuziwekea namna. Hivyo ndivyo amesema at-Tirmidhiy.

[1] Muslim (1036).

[2] al-Bukhaariy (1429), Muslim (1033), Abu Daawuud (1632), an-Nasaa’iy (5/61), Maalik (2/259) na Ahmad (2/67).

[3] al-Bukhaariy (1410), Muslim (1/405) na Ahmad (3/331).

[4] at-Tirmidhiy (656), an-Nasaa’iy (5/57) na Ibn Maajah (1842).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Ahmad al-Qurtwubiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Qam´-ul-Hirsw biz-Zuhd wal-Qanaa´ah, uk. 73-75
  • Imechapishwa: 18/03/2017