20 – Madhambi yanaingia katika laana ya Mtume

Madhambi yanamwingiza mja katika laana ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Aliyalaani maasi na yale yaliyo khatari zaidi kuliko hayo, ambayo nayo yana haki zaidi ya kulaaniwa.

Amemlaani mwanamke mwenye kufanya tattoo na mwenye kufanywa tattoo, mwenye kurefusha nywele na yule mwenye kurefushwa nywele, mwenye kukata nyusi na yule mwenye kukatwa nyusi.

Amemlaani mwenye kula ribaa, muwakilishi wa ribaa, mwandishi wa ribaa na mashahidi wake.

Amemlaani mwanaume anayemuoa mwanamke baada ya kutalikiwa mara tatu ili mwanamke huyo aweze kurudi kwa yule mume wake wa kwanza na amemlaani huyo mwanaume wa kwanza.

Amemlaani mwizi.

Amemlaani mwenye kunywa pombe, mwenye kuhudumu pombe, kutengeneza pombe, mwenye kutengenezewa pombe, mwenye kuuza pombe, mwenye kununua pombe, mwenye kutumia pesa zinazotokamana na pombe, mwenye kuibeba na yule mwenye kubebewa.

Amemlaani yule mwenye kubadilisha alama na mipaka ya kiwanja.

Amemlaani yule mwenye kuwalaani wazazi wake wawili.

Amemlaani yule mwenye kuwinda kwa sababu tu ya kutaka kujifurahisha.

Amemlaani mwanaume mwenye kujifananisha na wanawake na mwanamke mwenye kujifananisha na wanaume.

Amemlaani yule mwenye kuchinja kwa ajili ya asiyekuwa Allaah.

Amemlaani yule mwenye kuzusha uzushi au kumlinda mzushi.

Amewalaani watengeneza mapicha.

Amemlaani yule mwenye kufanya kitendo cha watu wa Luutw.

Amemlaani yule mwenye kuwatukana wazazi wake.

Amemlaani yule mwenye kumpoteza kipofu na njia.

Amemlaani yule mwenye kumwingilia mnyama.

Amemlaani yule mwenye kumweka alama mnyama usoni.

Amemlaani yule mwenye kumdhuru muislamu au kumfanyia vitimbi.

Amemlaani mwanamke mwenye kuyatembelea makaburi.

Amemlaani yule mwenye kuyafanya makaburi kuwa ni sehemu ya kuswalia au akayawekea makaburi mataa.

Amemlaani mwanaume mwenye kumwingilia mke wake kwa nyuma.

Amesema kuwa mwanamke ambaye ataitwa kitandani na mume wake kisha akakataa basi amelaaniwa mpaka atapoamka.

Amemlaani yule mwenye kujinasibisha na asiyekuwa baba yake.

Ameeleza kuwa yule mwenye kumuashiria nduguye chuma basi Malaika wanamlaani.

Amemlaani yule mwenye kuwatukana Maswahabah.

  • Mhusika: Imaam Ibn Qayyim-il-Jawziyyah
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ad-Daa’ wad-Dawaa’, uk. 72
  • Imechapishwa: 09/01/2018