Swali 19: Ni jambo lililoenea kati ya vijana wa leo ya kwamba ni lazima kwa mtu kufanya uwiano wakati wa kukosoa. Wanasema pindi mtu anapotaja Bid´ah na makosa ya mtu fulani, basi ni lazima vilevile kutaja mazuri yake. Wanasema kufanya hivi ndio uadilifu na uwiano. Je, mfumo huu katika ukosoaji ni sahihi? Je, ni lazima kutaja mazuri wakati ninaporaddi?

Jibu: Swali hili limeshatanguliwa kujibiwa. Ikiwa yule mkosolewaji ni katika Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah na wakati huohuo kosa lake halihusiani na ´Aqiydah, ni kweli. Sifa zake nzuri na mazuri yake yanatakiwa kutajwa. Kosa lake linafunikwa na kuinusuru kwake Sunnah. Lakini ikiwa yule mkosolewaji ni katika wapotevu, wapindaji, watu wenye misingi ya kuangamiza au ya kutia shaka, huyu haijuzu kwetu kutaja mazuri yake – endapo atakuwa nayo. Kwa sababu ukitaja mazuri utakuwa unawadanganya watu ambapo watakuja kumjengea dhana nzuri mtu ambaye ni mpotevu, mzushi, khurafi au Hizbiy. Baada ya hapo matokeo yake waanze kukubali fikira za mtu huyo.

Allaah (´Azza wa Jall) amewaraddi makafiri, watenda dhambi na wanafiki pasi na kutaja mazuri yao[1]. Vilevile maimamu wa Salaf wamewaraddi Jahmiyyah, Mu´tazilah na wapotevu wengine pasi na kutaja mazuri yao. Kwa sababu mazuri yao yanafunikwa na upotofu, kufuru, ukanamungu na unafiki. Ni jambo lisilokuwa la sawa ukamraddi mtu ambaye ni mpotevu, mzushi na mtu aliyepinda kisha eti useme mtu huyu ni mzuri na ana mazuri ilihali amekosea. Kumsifu kwako ni kubaya zaidi kuliko upotevu wake kwa sababu watu wanaamini kule kumsifu kwako. Pindi unapomsifu mpotevu mzushi huyu unawahadaa watu. Huku ni kufungua mlango fikira za wapotevu kuanza kukubalika kwa watu[2].

Ama ikiwa yule mwenye kuraddiwa ni katika Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah, basi Radd inatakiwa iwe kwa adabu. Akumbushwe kosa alilofanya katika masuala ya Fiqh au ya Ijtihaad. Tunasema kuwa fulani amefanya Ijtihaad lakini amekosea katika suala hili na dalili inasema kinyume navyo na Allaah amsamehe. Namna hii ndivyo zilikuwa Radd kati ya maimamu wanne na wengineo. Hili halipunguzi nafasi yake ya kielimu ikiwa ni katika Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah. Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah hawakukingwa na kukosea. Wanakosea. Wanaweza wapitwa na dalili na kuchanganya mambo. Hatunyamazii makosa. Tunalibainisha pamoja kumpa udhuru mwenye nalo. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakimu akihukumu na akajitahidi na kupatia, anapata ujira mara mbili. Na akihukumu na kujitahidi na kukosea, anapata ujira mara moja.”[3]

Haya yanahusiana na masuala ya Fiqh.

Lakini kosa ikiwa linahusiana na mambo ya ´Aqiydah, haijuzu kwetu kuwasifu wapotevu na wengineo wenye kwenda kinyume na Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah kama vile Mu´tazilah, Jahmiyyah, mazanadiki, wakanamungu[4] na watu wengine wenye kutia shaka katika wakati wa leo. Ni wengi walioje hii leo.

Msingi wa hoja tata hii ya kwamba mazuri na mabaya yote mawili yanatakiwa kutajwa wakati wa kukosoa ni jambo linalotoka kwa baadhi ya vijana walioandika kijitabu kuhusu hilo. Hivyo baadhi ya vijana wakaanza kukieneza kwa furaha. Nimesoma kijitabu hiki ambacho mwandishi analazimisha haki sawa. Nimesoma pia Radd ya Shaykh Rabiy´ bin Haadiy al-Madkhaliy kwa kijitabu hiki. Ni Radd ya kutosheleza. Humo amebainisha kuwa maneno haya ni kosa na ni kueneza batili. Vivyo hivyo ameweka wazi ya kwamba Salaf walikuwa wakiwaraddi watu wapotevu bila ya kuwasifu, kwa sababu kuwasifu katika mnasaba huu ni mgongano.

[1] Hakuna yeyote mwenye kukosa mazuri, hata mayahudi na manaswara. Kujengea juu ya kanuni ya haki sawa ni lazima kwetu kutaja mazuri ya makafiri pindi tunapowataja. Haya hayasemwi na mtu mwenye akili, sembuse mwanafunzi. Salaf hawakuwa wakitaja mazuri wakati wa kukosoa. Na endapo watataja mazuri, basi ilikuwa ni ili mtu asidanganyike nao na sio kwa sababu ni lazima kwa mtu afanye hivo. Hapa kunafuatia baadhi ya mifano yenye nguvu ambayo inampa uwongofu na nuru kwa yule mwenye kuizingatia:

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema kuhusu Khawaarij:

“Kupitia mgongo wa huyu watajitokeza watu watakaoisoma Qur-aan pasi na kuvuka koo zao. Wanatoka katika dini kama ambavyo mshale unatoka kwenye upinde wake. Wanawaua waislamu na kuwaacha waabudia masanamu. Lau nitakutana nao basi nitawaua kama walivyouawa kina ´Aad.” (al-Bukhaariy (3166))

Katika upokezi mwingine imekuja:

“Mtazidharau swalah zenu mkizilinganisha na swalah zao na swawm zenu mkizilinganisha na swawm zao.” (al-Bulhaariy (3414))

Katika upokezi mwingine imekuja:

“Waueni popote mtapokutana nao.” (al-Bukhaariy (3415))

Naapa kwa jina la Allaah ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakutaja sifa zao kwa ajili ya kuwasifu au kwa ajili ya kuwadanganya watu; amefanya hivyo ili kuwatahadharisha watu wasidanganyike na matendo yao ya dhahiri. Salaf walielewa hivyo na wakatendea kazi hilo katika maisha yao na wakafanya hilo kuwa ni mfumo wanaouitakidi. Kwa mfano Imaam Ahmad alimwangusha al-Karaabiysiy wakati aliposema kuwa matamsi ya Qur-aan yameumbwa. Imaam ´Abdullaah (Rahimahu Allaah) amesema:

“Nilimsikia baba yangu akisema: “Ni maneno maovu na fedheha kusema kuwa matamshi ya Qur-aan yameumbwa. Hiyo ndio ´Aqiydah Jahmiyyah.” Nikasema: “Husayn al-Karaabiysiy anasema hivyo.” Akasema: “Khabithi – Allaah amfedheheshe – anasema uwongo.” (as-Sunnah (01/165))

Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) amesema maneno makali zaidi kuliko hivyo juu ya al-Haarith al-Muhaasibiy. ´Aliy bin Abiy Khaalid amesema:

“Nilimwambia Ahmad kuhusu Shaykh aliyekuwa pamoja nasi: “Shaykh ni jirani yangu. Nimemtahadharisha juu ya mtu, lakini anapenda kukusikia unachosema juu ya Haarith yule mfupi (al-Muhaasibiy). Uliniona pamoja naye kwa miaka mingi na ukanambia: “Usikae naye, usizungumze naye.” Sikuzungumza naye tokea siku ile. Hata hivyo Shaykh huyu anakaa naye. Unasemaje juu yake?” Ahmad akageuka mwekundu usoni na mishipa yake ya shingoni na macho vikavimba. Sijapatapo kumuona namna . Kisha akasema hali ya kuwa ni mwenye kutetemeka: “Yule pale? Allaah amfanye hili na lile! Hakuna mwenye kumjua isipokuwa tu yule mwenye uzoefu naye na kumtambua! Hakuna mwenye kumjua isipokuwa tu yule mwenye uzoefu naye na kumtambua! Alikaa na al-Mughaaziliy, Ya´quub na wengine akawafanya wapinde katika madhehebu ya Jahm. Wakaangamia kwa sababu yake.” Shaykh yule akasema: “Ee Abu ´Abdillaah! Ni mtu mwenye kusimulia Hadiyth na ni mmakinifu na ni mnyenyekevu.” Abu ´Abdillaah akakasirika na kusema: ”Usidanganyike na unyenyekevu na upole wake. Usidanganyike na kuinamisha kwake kichwa. Ni mtu muovu. Hakuna anayemtambua isipokuwa tu yule mwenye uzoefu naye! Usizungumze naye. Hatakiwi kuonyeshwa heshima. Je, wewe unakaa na kila mzushi anayesimulia Hadiyth kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)? Hapana. Hatakiwi kuonyeshwa heshima!” (Twabaaqaat-ul-Hanaabilah (01/233))

Uko wapi uadilifu wenye kudaiwa kutoka kwa Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah)? Hakutaja zuri hata moja kutoka kwa al-Karaabiysiy wala al-Muhaasibiy pamoja na kuwa al-Karaabisiy alikuwa ni bahari ya elimu. Tazama historia yake katika “Taarikh Baghdaad” (08/64) na “Siyar A´laam-in-Nubalaa´” (12/79).

Allaah amrehemu Imaam Ahmad. Lau angeliyafanya hayo hii leo basi angelituhumiwa kuwa ni msimamo mkali, kibaraka, mwanasekula na majina ya bandia mengine ambayo yanatumiwa na Hizbiyyuun wanapozidiwa na hoja. Kwa sababu hakuwapaka mafuta na kuwaridhisha watu wa Bid´ah. Raafiy´ bin Ashras (Rahimahu Allaah) amesema:

“Miongoni mwa adhabu ya mtenda dhambi mzushi ni kutotaja mazuri yake.” (Tazama “Sharh ´Ilal at-Tirmidhiy” (01/353))

[2] Soma kisa hiki uone ukhatari wa jinsi watu wanavyoweza kudanganyika kwa kuwasifu Ahl-ul-Bid´ah. Imaam adh-Dhahabiy na wengineo wamepokea:

“Abul-Waaliyd amesema katika kitabu “Ikhtiswaar Firaq-il-Fuqahaa´” alipotajwa Abu Bakr al-Baaqilaaniy: “Nilimuuliza Abu Dharr al-Harawiy ambaye alikuwa amelemea katika madhehebu ya ki-Ash´ari: “Ilikuweje?” Akasema: “Siku moja nilikuwa natembea na Abul-Hasan ad-Daaraqutwniy tukakutana na Abu Bakr bin at-Twayyib al-Ash´ariy. ad-Daaraqutwniy akamkumbatia na kumbusu paji lake la uso na macho yake. Walipotengana nikamwambia: “Ni nani huyu ambaye umemfanyia hivi? Sikudhania katu kama unaweza kufanya kitu kama hicho. Kwa vile wewe ndiye Imaam wa wakati wako.” Akajibu kwa kusema: “Yule ni Imaam wa waislamu na mtetezi wa dini; Qaadhwiy Abu Bakr at-Twayyib.” Tokea wakati huo nikaanza kwenda kwake na kufuata madhehebu yake.” (Tadhkirat-ul-Huffaadhw (3/1104-1105) na Siyar A´laam-in-Nubalaa´ (17/558-559))

Pindi ad-Daaraqutwniy alipofanya yakufanya kwa al-Baaqilaaniy al-Ash´ariy na akamtukuza kama Imaam wa waislamu na kadhalika, wakadanganyika wale walioyaona na kwa sababu hiyo wakafuata madhehebu ya Ashaa´irah. Haya yanawahusu wale wote wenye kuwasifu Ahl-ul-Bid´ah wal-Ahwaa´, matokeo yake atasababisha wengi kuingia katika madhehebu yao na khaswa ikiwa wanaonekana ni wema kwa uinje na Allaah ndiye anajua zaidi.

[3] al-Bukhaariy (6919) na Muslim (1716).

[4] Huenda akawepo mtu mwenye kuuliza ni kwa nini nyinyi siku zote mnataja mapote ambayo yameshapotea kama Mu´tazilah, Jahmiyyah, mazanadiki, Ashaa´irah, Khawaarij na Murji-ah mnazungumzia ´Aqiydah na kuna faida gani ya kufanya hivo. Ni kweli kwamba mapote haya yameshapotea na wafuasi na waasisi wake wameshaiaga dunia kwa siku nyingi. Lakini hata hivyo fikira zao bado zipo. I´tiqaad zao zipo. Wafuasi wao ambao wameathirika nao wako kati yetu. ´Aqiydah yao na fikira zao zinarithiwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine. Kuna watu wenye kuzieneza. Kwa mfano ´Aqiydah ya Mu´tazilah ipo. Iko na wengi ambao wanajinasibisha na Uislamu. Mapote yote ya Shiy´ah kukiwemo Zaydiyyah wana madhehebu ya Mu´tazilah. Ashaa´irah ni pote lililo na mkusanyiko mkubwa kati ya waislamu wengi hii leo. Fikira za Murji-ah zinapatikana pia. Ahnaaf wanaonelea kuwa imani ni kusadikisha na maneno na kwamba matendo hayaingii ndani ya imani. Pamoja na hivyo madhehebu haya ni afadhali kidogo kuliko wanafalsafa wa Murji-ah. Ijapo kila zama kuna ´Aqiydah na madhehebu haya yenye kwenda kinyume na ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah, katika kila zama daima kuna mwenye kuyatetea. Kamati yenye kudumu kwa ajili ya tafiti za kielimu na kufutu Saudi Arabia ilitoa fatwa ya matahadharisho dhidi ya Irjaa´ na kusema:

“Murji-ah wanayaondosha matendo katika imani na wanasema kuwa imani ni ima kusadikisha kwa moyo peke yake au kusadikisha kwa moyo na kutamka kwa ulimi. Kwa mujibu wao wanaonelea kuwa matendo ni sharti juu ya kutimia kwa imani na sio sehemu katika imani. Wanaonelea kuwa mwenye kusadikisha kwa moyo wake  na kutamka kwa ulimi, basi wanaona kuwa huyo ni muumini mwenye imani kamili hata kama ataacha mambo ya wajibu na kufanya mambo ya haramu. Wanasema kuwa anastahiki kuingia Peponi ingawa hakupatapo kufanya kitendo cha kheri chochote.

Ni jambo lisilokuwa na shaka yoyote ya kwamba maoni haya ni batili na ni upotevu wa wazi kabisa wenye kwenda kinyume na Qur-aan na Sunnah na yale waliyomo Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah. Fikira hizi zinawafungulia njia waovu na watenda madhambi… ” (Fatwa (21436) 1421-04-08, at-Tahdhiyr min al-Irjaa´ wa ba´dhw al-Kutub ad-Daa´iyah ilayh, uk. 08-09)

Wakanamungu katika Wahdat-ul-Wujuud na wengineo wapo vilevile. Wanamfuata Ibn ´Arabiy at-Twaa´iy na Suufiyyah waliovuka mipaka.

Kwa hivyo pindi tunapotaja mapote haya hatuzungumzii mifupa ambayo imeshateketea. Hakika tunazungumzia juu ya mapote yaliyopo leo kati ya waislamu. Haya wanayajua wanafunzi. Watu wasioyajua, au wenye kutaka kuwatia watu mchanga wa machoni na kueneza I´tiqaad za batili, ndio wenye kutukataza kutahadharisha mapote haya. Watu hawa wanatakiwa kuuliza kabla ya kukemea. Haya ilikuwa tu ni kwa kifupi tu na Allaah ndiye anajua zaidi. Hapa kunafuatia baadhi ya mifano kuonyesha kuwa yale mapote yaliyoangamia fikira zake zipo hii loe:

1 – Sayyid Qutwub amesema:

“Qur-aan udhahiri wake ni kama ulimwengu kama mfano wa ardhi na mbingu.” (Fiy Dhwilaal-il-Qur-aan (4/2328))

Hii ni fikira ya kwamba Qur-aan imeumbwa, ´Aqiydah ambayo ni ya Jahmiyyah na wengineo. Amesema pia kuwa Qur-aan ina namna na usulubu kama wa nyimbo na akatoa mfano wa “ash-Shams”, “al-Fajr”, “al-Ghaashiyah”, “at-Twaariyq” na “al-Qiyaamah”. Amemsifu Allaah kama mtengenezaji katika Suurah “al-A´laa”. Utakasifu ni Wako Allaah kwa yale wanayoyasema. Tazama urukusa wa 3883.

2 – Amesema pia wakati alipokuwa akitafsiri Suurah “al-Ikhlaasw”:

“Hakuna uhakika isipokuwa uhakika Wake na hakuna uwepo wa hakika isipokuwa uwepo Wake. Uwepo mwingine wote una chanzo chake katika ule uhakika wa kweli.” (Fiy Dhwilaal-il-Qur-aan (6/4002))

´Allaamah na Shaykh Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn (Rahimahu Allaah) amesema:

“Nimesoma tafsiri yake ya Suurah “al-Ikhlaasw”. Amesema maneno makubwa yenye kwenda kinyume na mfumo wa Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah, kwa sababu tafsiri yake inaashiria kuwa anazungumza kwa Wahdat-ul-Wujuud.” (Baraa-atu ´Ulamaa´-il-Ummah, uk. 42)

Muhaddith na Shaykh al-Albaaniy (Rahimahu Allaah) amesema:

“Sayyid Qutwub anazungumza maneno ya Suufiyyah na mtu hawezi kufahamu jengine kwake isipokuwa kwamba anaonelea Wahdat-ul-Wujuud.” (Baraa-atu ´Ulamaa´-il-Ummah, uk. 37)

Ameandika kwa hati ya mkono wake (Rahimahu Allaah) mwanzoni mwa kitabu cha Shaykh Rabiy´ bin Haadiy al-Madkhaliy (Hafidhwahu Allaah) ”al-´Awaaswim mimmaa fiy Kutub Sayyiq Qutwub min al-Qawaaswim”:

Yote uliyomkosoa Sayyid Qutwub ni haki na ni sawa. Hivyo itambainikia kila msomaji muislamu ambaye angalau ana elimu kidogo ya Uislamu, ya kwamba Sayyid Qutwub hakuwa na utambuzi wowote juu ya Uislamu, si katika misingi wala tanzu zake. Ee ndugu Rabiy´! Allaah akujaze kheri kwa kuwa umetimiza wajibu huu wa kubainisha na kufichukua ujinga na upotofu wake katika Uislamu.(Uk. 03, chapisho la pili, 1421 na gazeti la “as-Salafiyyah” 07/1422, uk. 46)

3 – Muhammad Qutwub amesema:

”Watu wanahitaji kulinganiwa katika Uislamu. Lakini mara hii hawalinganiwi katika Uislamu kwa sababu wamekataa kutamka shahaadah, kama walivofanya mara ya kwanza. Mara hii wanalinganiwa kwa sababu wanakataa kile kinachopelekea katika shahaadah hiyo, nayo ni kuhukumu kwa Shari´ah.”  (Waaqi´unaa al-Mu´aaswir, uk. 29)

Huku ni kuwakufurisha waislamu wote kwa jumla. Vipi anaweza kusema kuwa wanakataa hukumu ya Allaah? Vipi anaweza kuwalinganisha na kipindi cha washirikina kabla ya Uislamu? Hakutaja ufafanuzi wowote na wala hakuwabagua wale wenye kuhukumu na Shari´ah ya Allaah na hawana katiba nyingine zaidi ya Qur-aan. Waandishi hawa mara nyingi hutamka namna hii. Ni kana kwamba hawaitambui nchi ya Kiislamu ya Salafiyyah katika kisiwa cha Kiarabu. Kana kwamba hawawatambui waislamu katika pande za dunia katika Ahl-ul-Hadiyth, Answaar-us-Sunnah na wengineo wenye kufuata mfumo wa Salaf. La kushangaza ni kuona jinsi baadhi ya wanaotamka namna hiyo wanaishi katika nchi hii ya Kiislamu Saudi Arabia. Maoni yao ni ya khatari kwa msomaji kwa sababu msomaji mwepesi anaweza kufikiria kuwa hii leo hakuna nchi yoyote ile ya Kiislamu inayotamka shahaadah, inayotendea kazi muqtadha yake na kuhukumu Shari´ah ya Allaah na kwamba hakuna baadhi ya watu au makundi yenye kumuabudu Allaah peke yake katika uso wa ardhi. Namna hii ndivyo wanavyomhadaa msomaji na kumpaka mchanga wa machoni ili atumbukie kwenye Takfiyr, jambo ambalo wengi wametumbukia ndani yake. Kwa ajili hiyo ndio maana inatakiwa kwa msomaji kuwa makini na fikira hizi zilizoenea zenye kutoka kwa waandishi wengi kama hawa – Allaah awaongoze katika usawa.

4 – Kuna mmoja ambaye anajinasibisha na ulinganizi ambaye amesema:

“Katika kudhihirisha maasi ni pamoja na mtu kujifakhari nayo mbele ya marafiki zake na kuelezea jinsi mtu alifanya hili na lile na kuanza kutaja idadi ya maasi. Huyu hatosamehewa ikiwa hatotubia. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema kuwa hatosamehewa pale aliposema:

“Ummah wangu wote utasamehewa isipokuwa wale wanaodhihirisha maasi.” (Kanda “Jalsah ´alaar-Raswiyf”)

Imetajwa wapi katika Hadiyth ya kwamba Allaah hatomsamehe mtu huyu? Ni nani katika Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah aliyesema kuwa mtenda dhambi hata kama atafanya dhambi kwa kujionyesha na akafa kwamba hatosamehewa akifa kabla ya kutubu? Je, hili si liko chini ya utashi wa Allaah; akitaka atamsamehe na akitaka atamuadhibu? Vinginevyo hiyo ni ´Aqiydah Khawaarij na Mu´tazilah. Mlinganizi huyu anaendelea kusema:

“Baya zaidi kuliko hilo ni kwamba baadhi wanaelezea jinsi wana mahusiano ya kiharamu na marafiki wa kike na wanasafiri huku na kule. Anajishibisha kwa maasi. Baadhi wanarekodi maasi. Hawatakiwi kuonyeshwa heshima yoyote. Ni wenye kuritadi kwa kitendo chake hichi. Anarekodi jinsi anavyomdanganya msichana na baadaye anafanya naye machafu. Huku ni kuritadi kutoka katika Uislamu. Huyu atadumishwa Motoni ikiwa hatosamehewa na Allaah.” (Kanda “Jalsah ´alaar-Raswiyf”)

Amesema juu ya waimbaji ambapo kanda zao zinaenezwa na vijana na ndani yake nyimbo za fedheha zenye kuwahadaa mabarobaro na wasichana:

“Mimi naweza kusema kwa utulivu ya kwamba mtu huyu anayadharau maasi. Ni jambo lisilokuwa na shaka yoyote ya kwamba kudharau dhambi, khaswa inapokuwa ni dhambi kubwa ambayo kuna maafikiano juu ya uharamu wake, ya kwamba ni kufuru. Hapana shaka yoyote kuwa matendo ya watu ni kuritadi kutoka katika Uislamu. Nayasema haya hali ya kuwa ni mwenye utulivu na moyo wenye ukinaifu.” (Kanda “ash-Shabaab; As-ilah wa Mushkilaat)

Kukufurisha na kufasiri kule kuenea kwa maasi kati ya watu kwamba ni jambo lenye kuepelekea katika kufuru ni jambo linalofahamisha ujasiri uliochupa mipaka wa kukufurisha kwa madhambi makubwa na kutokuwa na uchaji Allaah. Hii ni ´Aqiydah ya Khawaarij amabo wanakufurisha kwa sababu madhambi makubwa. Mtu kuzungumzia madhambi na uhusiano wa haramu ni jambo linaloweza kuwa na maana nyingi. Mtu hakusema waziwazi ya kwamba anaonelea kuwa ni halali. Pengine kilichompelekea kufanya hivo ni ujinga. Ndio maana kinachotakiwa ni kumkumbusha na sio kukufurisha. Huu ndio mfumo wa Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah. Kudharua maasi hakufahamishi kuyachezea shere. Hakuna yeyote anayefanya madhambi, ni mamoja makubwa au madogo, isipokuwa kwanza huanza kwa kuyadharau na kuyapuuza. Kwa hivyo yule mwenye kufanya hivo si kwamba anafanyia mashkara. Na ni nani aliyekingwa na kukosea? Na Allaah ndiye anajua zaidi.

5 – Kuna mwengine ambaye anauliza swali na wakati huohuo anajibu:

“Tuchukulie kuwa maovu yanayopatikana hii leo katika jamii yetu ni maasi tu. Wengi leo wanafikiria kuwa ribaa, madawa ya kulevya, pombe na rushwa ni maasi tu au dhambi kubwa… Ndugu! Nimefuatilia jambo hili na kuona kuwa watu wengi katika jamii yetu wanaona kuwa ribaa ni halali. Mnajua kuwa benki katika nchi zetu zina wateja zaidi ya milioni moja? Je, wateja wote hawa milioni wanajua kuwa ribaa ni haramu na kwamba wanachokifanya ni dhambi tu? Hapana, kwa jina la Allaah! Kwa sababu ya kuenea kwa wingi kwa madhambi hii leo basi kuna khatari wengi kuonelea kuwa madhambi haya makubwa ni halali.” (Kanda “at-Tawhiyd Awwalan”)

Ninasema kama nilivyosema hapo juu na kuongezea ya kwamba mfano kama huu ni khatari kwa mzungumzaji pale anapopindukia na kusema kuwa madhambi yanayotokea katika jamii yetu kama vile ribaa, pombe na madawa ya kulevya na rushwa si kwamba ni maasi peke yake au dhambi kubwa. Isitoshe anaapa kwa jina la Allaah juu ya hilo.

Kusema kwamba anayefanya madhambi haya ni mwenye kuyahalalisha pasi na kumsikia mtu mwenyewe anasema waziwazi kuwa ni halali, hukumshuhudia akisema kitu cha waziwazi chenye kuashiria kuwa anayahalalisha madhambi haya, kunafahamisha waziwazi udhaifu wa uchaji Allaah wa mzungumzaji huyu na kutojali. Hii ndio ´Aqiydah ya Khawaarij na Mu´tazilah.

Ninawanasihi watu hawa na watu mfano wao kujirejea katika matamshi kama haya ambayo yanawatia khatarini wao kwanza kabla ya wengine. Kurejea katika haki ni bora kuliko kuendelea katika batili.

6 – Mwengine wa tatu amesema (na ni daktari katika ´Aqiydah) wakati alipokuwa ameshika gazeti la hoteli moja iliopo Ghuba (na amefanya hayo msikitini na hakuonyesha adabu ya utukufu wa msikiti):

“Kuna hoteli moja katika nchi iliopo Ghuba, Dubai, inayoitwa “Metropolitan Hotel”. Kwenye hoteli hii kunasemwa waziwazi kwamba wanahudumu pombe. Isitoshe kuna… Huku ni kuita waziwazi kwenye pombe. Wamefikia kiasi cha kuchukua picha zenye kuthibitisha juu ya kwamba kuna densi za waliovaa vibaya na pombe. Tunajilinda kwa Allaah kutokana na ukafiri huu. Bila ya shaka ni kufuru na ni kuhalalisha kitu alichoharamisha Allaah.” (Sharh at-Twahaawiyyah (02/272))

Amesema tena katika moja ya vitabu vyake:

“Kumejitokeza kufuru na ukanamungu katika magazeti yetu. Madhambi yameenea katika vilabu vyetu. Kunalinganiwa katika uzinzi katika redio na runinga zetu. Tumehalalisha ribaa.”

Kitabu hiki kimechapishwa kwa vichwa vya khabari mbalimbali. Pakistan kinaitwa “Kashf-ul-Ghummah ´an ´Ulamaa´-il-Ummah”, Amerika kinaitwa “Wa´du Kissinger” na Misri kinaitwa “Haqaa-iq hawl Ahdaath-il-Khaliyj”.

Kwa hali yoyote mwenyewe unaona jinsi mzungumzaji wa maneno haya anavyothubutu kuthibitisha ya kuwa sisi tunaonelea kuwa ribaa na madhambi mengineyo yaliyopo kwamba ni halali. Si sisi wala jamii zetu hatuonelei kuwa ribaa ni halali. Wala hatuonelei kuwa pombe katika miji ya majirani zetu ni kufuru yenye kumtoa mtu katika Uislamu. Yote waliyotaja watu hawa wenye kujinasibisha na ulinganizi ni madhambi na sio kufuru. Ni aina ya kufuru ndogo, maasi na madhambi makubwa yenye kupunguza ukamilifu wa imani ya mtu na sio imani yote. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hazini mwenye kuzini pale anapozini hali ya kuwa ni muumini, haibi mwenye kuiba pale anapoiba hali ya kuwa ni muumini… ” (al-Bukhaariy (2243))

Ni jambo lisilokuwa na shaka ya kwamba imani inayokanushwa hapa ni ukamilifu wake. Kuna hali mfano wa hizo nyingi katika Shari´ah yetu.

Hivi sasa mwenyewe umejionea fikira zilizo na baadhi ya walinganizi, seuze vijana waliodanganyika wenye kukaa na walinganizi hawa. Wanajifunza fikira na I´tiqaad kama hizi zenye kuangamiza mfumo wa Salaf. Baada ya haya yote mtu anaweza kuuliza ni kwa nini tunazungumzia mapote potofu na yaliyopinda ambayo yameshapotea kutokana na ´Aqiydah na mifumo yao wakati ´Aqiydah na upindaji wao bado upo? Kwa ajili hiyo tafakari umuhimu wa kulingania katika Tawhiyd na kuitendea kazi, kutahadharisha mapote yote katika kila zama na kila mahali na kurejea katika Qur-aan na Sunnah kutokana na mfumo wa Salaf.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Ajwibah al-Mufiydah ´an As-ilat-il-Manaahij al-Jadiydah, uk. 52-64
  • Imechapishwa: 31/05/2023
  • mkusanyaji: Shaykh Jamaal bin Furahyaan al-Haarithiy