19. Ni ipi hukumu ya mwenye kula katika Ramadhaan na wakati huohuo hapingi uwajibu wake?

Swali 19: Ni ipi hukumu ya mwenye kula katika Ramadhaan na wakati huohuo hapingi uwajibu wake? Je, ametoka nje ya Uislamu kwa kule kuacha kwake kufunga kwa sababu ya kuzembea zaidi ya mara moja?

Jibu: Mwenye kula katika Ramadhaan kwa makusudi bila ya udhuru wa Kishari´ah amefanya dhambi kubwa. Lakini hakufuru kwa mujibu wa maoni sahihi zaidi ya wanachuoni. Ni lazima kwake kutubia kwa Allaah (Subhaanah) pamoja na kulipa. Zipo dalili nyingi zinazothibitisha kwamba kuacha kufunga sio kufuru kubwa midhali mtu hapingi kuwa ni wajibu na bali ameacha kufunga kwa sababu ya ivivu na kuzembea. Ni lazima kwake kulisha maskini kwa kila siku moja aliyochelewesha kulipa mpaka akaingiliwa na Ramadhaan nyingine pasi na kuwa na udhuru wa Kishari´ah kutokana na yale yaliyotangulia katika jibu la swali la kumi na saba[1]. Kadhalika kuacha kutoa zakaah na kuhiji mtu hakufuru kwa vitendo hivyo. Lakini ni lazima kwake kutoa zakaah juu ya ile miaka iliyompita na akawa hakutoa ambapo alizembea. Vilevile ni lazima kwake kuhiji pamoja na kutubu tawbah ya kweli kwa sababu ya kuchelewesha. Hayo ni kutokana na ujumla wa zile dalili za Kishari´ah katika hayo ambazo zimefahamisha juu ya kutokukufuru midhali mtu hapingi kuwa ni wajibu. Miongoni mwa dalili hizo ni ile Hadiyth kuhusu kuadhibiwa kwa aliyeacha kuitolea mali yake zakaah siku ya Qiyaamah mpaka hatimaye ataona njia yake ima kuelekea Peponi au Motoni.

[1] Tazama https://firqatunnajia.com/17-ni-ipi-hukumu-ya-aliyechelewesha-kulipa-mpaka-akaingiliwa-na-ramadhaan-nyingine/

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdllaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: As-ilah Muhimmah tata´alaqah bisw-Swiyaam, uk. 25-26
  • Imechapishwa: 01/05/2019