19. Mtindo bora kabisa wa kufunza


Abu Muhammad ´Abdullaah bin Abiy Zayd al-Qayrawaaniy (Rahimahu Allaah) amesema:

Kutokana na kwamba dhumuni lako ni kuwafunza nayo watoto kama ambavo unawafunza kisomo cha Qur-aan, basi nimewepesisha ambacho ni tatizo katika zile tafsiri na maana za wale wanachuoni waliobobea. Lengo wapate kuifahamu dini na Shari´ah ya Allaah ili ipate kubarikiwa elimu yao na uweze kusifiwa mwisho wao mwema. Nikakuitikia maombi yako, kwa sababu nataraji mimi na wewe kupata thawabu za kuifunza dini ya Allaah au kulingania kwayo.

MAELEZO

Kitabu hichi kifupi ni chepesi. Hakina mikusanyiko ambayo inakuwa migumu kwa wanafunzi kuielewa. Ni ufupisho mwepesi na wa wazi. Namna hii ndivo mtindo wa wanachuoni wa kale. Utavikuta vitabu vyao ni vyepesi. Elimu inatakiwa kuwepesishwa. Wanafunzi wanatakiwa kufanyiwa wepesi mafunzo kiasi cha itavyowezekana.

Mtunzi wa kitabu anamzungumzisha mwalimu wake ambaye alimuomba atunge kitabu na utangulizi huu. Alimwomba aandike kitabu hiki ili apate kuwafunza wanafunzi zake wadogo kama ambavyo anawafunza Qur-aan. Kwa msemo mwingine mafunzo yao yawe yamekusanya kufunzwa Qur-aan na Fiqh. Huu ndio mtindo bora kabisa wa kufunza. Mwalimu anatakiwa kuzingatia daraja za wanafunzi na aende nao hatua kwa hatua kuanzia katika mambo madogomadogo, mambo ya msingi na mada fupifupi. Wanapaswa kufunzwa Fiqh kama ambavo wanafunzwa Qur-aan. Kukusanywe kati ya kufunzwa Qur-aan, Fiqh na ´Aqiydah. Huu ndio mtindo mzuri na bora kabisa wa kufunza.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bayaan-ul-Ma´aaniy fiy Sharh Muqaddimati Ibn Abiy Zayd al-Qayrawaaniy, uk. 22
  • Imechapishwa: 08/07/2021