18. Sura ya kwanza: Ubainifu wa maana ya Tawhiyd-ul-Uluuhiyyah na kwamba ndio maudhui ya ulinganizi wa Mitume


Tawhiyd-ul-Uluuhiyyah. Uluuhiyyah ni ´ibaadah. Tawhiyd-ul-Uluuhiyyah ni kumpwekesha Allaah (Ta´ala) kwa matendo ya waja ambayo wanayafanya kwa njia ya ujikurubishaji uliowekwa katika Shari´ah. Mfano wake ni maombi, nadhiri, uchinjaji, kurejea, khofu, utegemezi, shauku, woga na kutubia. Tawhiyd aina hii ndio maudhui ya ulinganizi wa Mitume, kuanzia wa mwanzo wao mpaka wa mwisho wao. Amesema (Ta´ala):

وَلَقَدْ بَعَثْنَا فِي كُلِّ أُمَّةٍ رَّسُولًا أَنِ اعْبُدُوا اللَّـهَ وَاجْتَنِبُوا الطَّاغُوتَ

“Hakika Tulituma katika kila ummah Mtume kwamba: “Mwabuduni Allaah na jiepusheni na Twaaghuut [waungu batili].”[1]

وَمَا أَرْسَلْنَا مِن قَبْلِكَ مِن رَّسُولٍ إِلَّا نُوحِي إِلَيْهِ أَنَّهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا أَنَا فَاعْبُدُونِ

“Hatukutuma kabla yako Mtume yeyote isipokuwa Tulimfunulia Wahy ya kwamba: “Hakika hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Mimi; hivyo basi niabuduni.”[2]

Kila Mtume alikuwa akianza kuwalingania watu wake kwa kuwaamrisha Tawhiyd-ul-Uluuhiyyah. Kama alivosema Nuuh, Huud, Swaalih na Shu´ayb:

يَا قَوْمِ اعْبُدُوا اللَّـهَ مَا لَكُم مِّنْ إِلَـٰهٍ غَيْرُهُ

“Enyi watu wangu! Mwabuduni Allaah, kwani hakika hamna mwabudiwa wa haki mwengine asiyekuwa Yeye.”[3]

وَإِبْرَاهِيمَ إِذْ قَالَ لِقَوْمِهِ اعْبُدُوا اللَّـهَ وَاتَّقُوهُ

”Ibraahiym pindi alipowaambia watu wake: ”Mwabuduni Allaah na mcheni.”[4]

Akamteremshia Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

قُلْ إِنِّي أُمِرْتُ أَنْ أَعْبُدَ اللَّـهَ مُخْلِصًا لَّهُ الدِّينَ

“Sema: “Hakika mimi nimeamrishwa nimwabudu Allaah hali ya kumtakasia Yeye dini.”[5]

Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Nimeamrishwa kuwapiga watu vita mpaka washuhudie ´hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah`.”[6]

Kitu cha kwanza cha wajibu kwa mja ni kushuhudia ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na kuitendea kazi. Amesema (Ta´ala):

فَاعْلَمْ أَنَّهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا اللَّـهُ وَاسْتَغْفِرْ لِذَنبِكَ

“Hivyo basi jua kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na omba msamaha kwa dhambi zako.”[7]

Kitu cha kwanza anachoamrishwa kwacho ambaye anataka kuingia ndani ya Uislamu ni kutamka shahaadah mbili. Kutokana na hayo imepata kubainika kuwa Tawhiyd-ul-Uluuhiyyah ndio malengo ya ulinganizi wa Mitume. Tawhiyd-ul-Uluuhiyyah imeitwa hivo kwa sababu sifa ya Allaah (Ta´ala) inayofahamishwa na jina Lake (Ta´ala) “Allaah”. Allaah ndiye mwabudiwa. Tawhiyd-ul-Uluuhiyyah inaitwa vilevile Tawhiyd-ul-´Ibaadah kwa kuzingatia kwamba uja ni sifa ya mja kwa njia ya kwamba analazimika kumwabudu Allaah hali ya kumtakasia Yeye nia kwa sababu ya kumuhitajia kwake Mola wake na ufakiri wake. Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema:

“Tambua kwamba ufakiri wa mja kwa Allaah ni yeye kumwabudu pasi na kumshirikisha Yeye na chochote. Hana mwenza wa kulinganishwa Naye. Lakini kwa namna fulani imefanana na namna mwili unavyohitajia chakula na kinywaji ingawa kuna tofauti nyingi. Uhakika wa mja ni moyo na roho yake. Hakuna kutengemaa kwake isipokuwa kwa mungu wake Allaah ambaye hapana mungu mwengine wa haki asiyekuwa Yeye. Haupati utulivu duniani isipokuwa kwa kumtaja. Lau mja atapata starehe mbalimbali na furaha bila ya Allaah basi ni jambo halitodumu. Bali itabadilika kutoka kwa namna moja hadi nyingine na kutoka mmoja kwenda kwa mwengine. Lakini kuhusu mola wake ni lazima amuhitajie katika kila hali na kila wakati. Popote atapokuwa ni lazima awe pamoja Naye.”[8]

Aina hii ya Tawhiyd ilikuwa ndio maudhui ya ulinganizi wa Mitume. Kwani ndio msingi ambao kunajengwa juu yake matendo yote. Pasi na kuihakikisha matendo yote hayasihi. Isipohakikishwa basi kunatokea kinyume chake ambacho ni shirki. Allaah (Ta´ala) amesema:

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَاءُ

“Hakika Allaah hasamehi kushirikishwa lakini anasamehe yaliyo chini ya hayo kwa amtakae.”[9]

وَلَوْ أَشْرَكُوا لَحَبِطَ عَنْهُم مَّا كَانُوا يَعْمَلُونَ

“Lau wangemshirikisha basi pasi na shaka yangeporomoka yale waliyokuwa wakiyatenda.”[10]

لَئِنْ أَشْرَكْتَ لَيَحْبَطَنَّ عَمَلُكَ وَلَتَكُونَنَّ مِنَ الْخَاسِرِينَ

“Ukifanya shirki bila shaka yataporomoka matendo yako na hakika utakuwa miongoni mwa waliokhasirika.”[11]

Jengine ni kwa sababu aina hii ya Tawhiyd ndio haki ya kwanza ambayo ni wajibu kwa mja. Amesema (Ta´ala):

وَاعْبُدُوا اللَّـهَ وَلَا تُشْرِكُوا بِهِ شَيْئًا ۖ وَبِالْوَالِدَيْنِ إِحْسَانًا

“Mwabuduni Allaah na wala msimshirikishe na chochot na watendeeni wema wazazi wawili.”[12]

وَقَضَىٰ رَبُّكَ أَلَّا تَعْبُدُوا إِلَّا إِيَّاهُ وَبِالْوَالِدَيْنِ إِحْسَانًا

“Mola wako amehukumu kwamba: “Msiabudu isipokuwa Yeye pekee na kuwafanyia wema wazazi wawili.”[13]

قُلْ تَعَالَوْا أَتْلُ مَا حَرَّمَ رَبُّكُمْ عَلَيْكُمْ ۖ أَلَّا تُشْرِكُوا بِهِ شَيْئًا ۖ وَبِالْوَالِدَيْنِ إِحْسَانًا

“Sema: Njooni nikusomeeni yale aliyoyaharamisha Mola wenu juu yenu: “Kwamba msimshirikishe na chochote na muwafanyie wema wazazi wawili.”[14]

[1] 16:36

[2] 21:25

[3] 07:59, 65, 73 na 85.

[4] 29:16

[5] 39:11

[6] al-Bukhaariy (01/102) na Muslim (01/150).

[7] 47:19

[8] Majmuu´-ul-Fataawaa (01/24-25).

[9] 04:48 na 116

[10] 06:88

[11] 39:65

[12] 04:36

[13] 17:23

[14] 06:151-153

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ´Aqiydat-ut-Tawhiyd, uk. 42-44
  • Imechapishwa: 10/02/2020