18. ´Ibaadah zote anatakiwa kufanyiwa Allaah pekee

Allaah (Subhaanah) kule kuwaomba kwao ameita kuwa ni shirki. Ni wajibu kwa wale wote ambao ´ibaadah ni yenye kuwawajibikia kumtakasia ´ibaadah Allaah pekee. Kusiwekwe matarajio kwa mwengine asiyekuwa Allaah. Asiogopwe mwengine asiyekuwa Allaah. Asitakwe msaada mwengine asiyekuwa Allaah. Asitakwe uokozi mwengine asiyekuwa Allaah. Kusichinjwe kwa ajili ya mwingine asiyekuwa Allaah. Asiwekewe nadhiri mwengine asiyekuwa Allaah. Asinyenyekewe mwengine asiyekuwa Allaah. Kusiswaliwe kwa ajili ya mwengine asiyekuwa Allaah. Kusifungwe kwa ajili ya mwengine asiyekuwa Allaah na mengineyo. Yote afanyiwe Allaah peke yake. Atayejikurubisha kwa mwengine asiyekuwa Allaah – sawa awe ni walii, Mtume, sanamu, mti au jiwe kwa kumuomba, kumchinjia, kumuwekea nadhiri, kumswalia, kumfungia au kitu kingine ni mshirikina kafiri. Atakuwa amemshirikisha Allaah na ameabudu pamoja Naye mwengine. Hivyo ndivyo walivyofanya washirikina wa mwanzo pindi walipoabudu makaburi, miti, mawe na masanamu. Ndio maana Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

وَلَوْ أَشْرَكُوا لَحَبِطَ عَنْهُم مَّا كَانُوا يَعْمَلُونَ

“Lau wangemshirikisha yangebatilika yale waliyokuwa wakitenda.” (06:88)

إِنَّهُ مَن يُشْرِكْ بِاللَّـهِ فَقَدْ حَرَّمَ اللَّـهُ عَلَيْهِ الْجَنَّةَ وَمَأْوَاهُ النَّارُ ۖ وَمَا لِلظَّالِمِينَ مِنْ أَنصَارٍ

“Hakika yule atakayemshirikisha Allaah bila shaka Allaah atamharamishia Pepo na makazi yake yatakuwa ni Motoni. Na madhalimu hawatopata yeyote mwenye kunusuru.” (05:72)

وَلَقَدْ أُوحِيَ إِلَيْكَ وَإِلَى الَّذِينَ مِن قَبْلِكَ لَئِنْ أَشْرَكْتَ لَيَحْبَطَنَّ عَمَلُكَ وَلَتَكُونَنَّ مِنَ الْخَاسِرِينَ بَلِ اللَّـهَ فَاعْبُدْ وَكُن مِّنَ الشَّاكِرِينَ

“Hakika umefunuliwa Wahy wewe na kwa wale waliokuwa kabla yako ya kwamba ukifanya shirki bila shaka zitabatilika ‘amali zako na [Aakhirah] utakuwa miongoni mwa waliokhasirika. Bali Allaah pekee mwabudu na uwe miongoni mwa wenye kushukuru.” (39:65-66)

Aina zote hizi za ´ibaadah ni wajibu kumtakasia nazo Allaah. Atayemfanyia chochote katika hayo asiyekuwa Allaah sanamu, mti, jiwe au kaburi ni mshirikina. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَمَن يَدْعُ مَعَ اللَّـهِ إِلَـٰهًا آخَرَ لَا بُرْهَانَ لَهُ بِهِ فَإِنَّمَا حِسَابُهُ عِندَ رَبِّهِ ۚإِنَّهُ لَا يُفْلِحُ الْكَافِرُونَ

“Yeyote yule anayeomba pamoja na Allaah mungu mwengine hana ushahidi wowote juu ya hilo, basi hakika hesabu yake iko kwa Mola wake, kwani hakika hawafaulu makafiri.” (23:117)

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 29
  • Imechapishwa: 08/12/2016