Mwanamke mwenye hedhi au mwenye damu ya uzazi akitwahirika kabla ya kuzama kwa jua, basi itamlazimu kuswali Dhuhr na ´Aswr ya siku hii. Akitwahirika kutokamana na hedhi na damu ya uzazi kabla ya kuchomoza kwa alfajiri, basi itamlazimu kuswali Maghrib na ´Ishaa ya usiku huo. Kwa sababu wakati wa swalah ya pili ndio wakati wa swalah ya kwanza katika hali ya udhuru. Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah amesema katika “al-Fataawaa”:

“Kwa ajili hiyo ndio maana jamhuri ya wanachuoni kama Maalik, ash-Shaafi´iy na Ahmad wanaona mwanamke mwenye hedhi akitwahirika mwishoni mwa mchana basi ataswali Dhuhr na ´Aswr zote mbili. Pia wanaona kuwa akitwahirika mwishoni mwa usiku basi ataswali Maghrib na ´Ishaa zote mbili. Hayo yamenukuliwa na ´Abdur-Rahmaan bin ´Awf, Abu Hurayrah na Ibn ´Abbaas. Kwa sababu wakati ni wenye kushirikiana kati ya swalah mbili katika hali ya udhuru. Akitwahirika mwishoni mwa mchana basi wakati wa Dhuhr bado ni wenye kuendelea na hivyo ataiswali kabla ya ´Aswr. Akitwahirika mwishoni mwa usiku basi wakati wa Maghrib bado ni wenye kuendelea katika hali ya udhuru na hivyo ataiswali kabla ya ´Ishaa.”[1]

Ama akiingiliwa na wakati wa swalah kisha akapata hedhi au damu ya uzazi kabla ya kuwahi kuswali, basi maoni yenye nguvu ni kwamba si lazima kwake kulipa swalah hiyo iliyompata mwanzoni mwa wakati wake kisha akapata hedhi au damu ya uzazi kabla ya kuiswali. Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah amesema katika “Majmuu´-ul-Fataawaa”:

“Kuhusiana na masuala haya, kilicho dhahiri katika dalili ni madhehebu ya Abu Haniyfah na Maalik ya kwamba hakuna kinachomlazimu. Kwa sababu ulipaji unalazimu kwa amri mpya na wala katika hali hii hakuna amri inayomlazimu kulipa. Jengine ni kwamba amechelewesha ucheleweshaji unaofaa. Kwa hivyo hakufaradhishiwa. Kuhusu ambaye kapitikiwa na usingizi au aliyesahau – japokuwa si mwenye kuzembea – yale wanayoyafanya sio ulipaji. Bali huo ndio wakati wao wa kuswali pale atapoamka au atapokumbuka.”[2]

[1] (22/434).

[2] (23/335).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tanbiyhaat, uk. 32-33
  • Imechapishwa: 29/10/2019