Salaf wa mwanzo katika wale waliokuja baada ya Maswahabah (Rahimahumu Allaah) walikuwa kipimo wanachokiweka juu ya mtu ambaye elimu inastahiki kuchukuliwa kutoka kwake ni kule kushikamana kwake na Sunnah. Ibraahiym an-Nakha´iy amesema:

“Walikuwa wanapomwendea mtu ili kuchukua elimu kutoka kwake, basi hutazama swalah yake, Sunnah zake na sifa zake. Baada ya hapo ndio wanachukua elimu kutoka kwake.”[1]

Mmoja katika wanachuoni amesema:

“Hakika miongoni mwa alama za kumpenda Allaah (´Azza wa Jall) ni kumfuata kipenzi cha Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika tabia zake, matendo, maamrisho yake na Sunnah zake.”

Jambo hili ni haki. Limechukuliwa kutoka katika Kitabu cha Allaah (´Azza wa Jall) pale aliposema:

قُلْ إِن كُنتُمْ تُحِبُّونَ اللَّـهَ فَاتَّبِعُونِي يُحْبِبْكُمُ اللَّـهُ وَيَغْفِرْ لَكُمْ ذُنُوبَكُمْ ۗ وَاللَّـهُ غَفُورٌ رَّحِيمٌ

“Sema: “Mkiwa mnampenda Allaah, basi nifuateni mimi. Hivyo atakupendeni Allaah na atakusameheni dhambi zenu na Allaah ni Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehemu.”[2]

al-Hasan al-Baswriy amesema kuhusu Aayah hiyo juu:

“Allaah amefanya alama ya kumpenda Yeye ni kule kufuata Sunnah za Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).”[3]

[1] ad-Daarimiy ”as-Sunnah” yake (01/397) (434a) na (435).

[2] 03:31-32

[3] al-Laalakaa´iy katika ”I´tiqaad Ahl-is-Sunnah” (01/70).

  • Mhusika: Shaykh ´Abdus-Salaam bin Barjas
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Usuwl-ud-Da´wah as-Salafiyyah, uk. 48
  • Imechapishwa: 11/08/2020