16. Uwajibu wa kuamini kuwa Allaah ataonekana Aakhirah


Imaam Ahmad amesema:

“… na Hadiyth nyengine zote kuhusu Kuonekana.”

Bi maana kuonekana Allaah siku ya Qiyaamah. Ni wajibu kwa muumini kuamini kuwa waumini watamuona Allaah siku ya Qiyaamah. Mu´tazilah wanakanusha kuwa Allaah ataonekana siku ya Qiyaamah. Wamejenga makanusho yao juu ya utata batili. Ahl-us-Sunnah wameyaraddi kwa hoja na dalili kutoka katika Qur-aan na Sunnah. Mmoja wao ni Imaam Ibn-ul-Qayyim (Rahimahu Allaah) ambaye ametumia hoja kwa Aayah saba katika Qur-aan. Mtu anaweza kuona kuwa ziko mbali, lakini lau mtu atazizingatia kwa kina basi atakuja kuona kuwa utumiaji wake dalili (Rahimahu Allaah) ni wa sawa.

Moja wapo ni Kauli Yake (Tabaarak wa Ta´ala):

وَاتَّقُوا اللَّـهَ وَاعْلَمُوا أَنَّكُم مُّلَاقُوهُ

“Mcheni Allaah na tambueni kwamba hakika nyinyi ni wenye kukutana Naye.”[1]

Amesema kuwa kukutana kwa mujibu wa lugha ya kiarabu kunapelekea katika kuonana ana kwa ana.

Amesema kuwa wale wenye kukanusha Kuonekana wanatumia hoja kwa Aayah za Qur-aan kwa mfano Kauli Yake (Tabaarak wa Ta´ala):

لَّا تُدْرِكُهُ الْأَبْصَارُ وَهُوَ يُدْرِكُ الْأَبْصَارَ ۖ وَهُوَ اللَّطِيفُ الْخَبِيرُ

“Macho hayamzunguki bali Yeye ndiye anayazunguka macho yote – Naye ni Mwenye kuyaendesha mambo kwa ulatifu, Mwenye khabari zote.”[2]

Amesema kuwa Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah kasema kuwa Allaah hasifiwi kwa makanusho peke yake isipokuwa ni makanusho ambayo ndani yake mna uthibitishaji. Ametaja dalili nyingi juu ya hili ikiwa ni pamoja na:

لَّا تُدْرِكُهُ الْأَبْصَارُ

“Macho hayamzunguki.”

Sentesi hii inathibitisha Kuonekana. Allaah hajasema kuwa hatoonekana; Alichosema ni kwamba hazungukwi. Hakuna chenye kumzunguka Allaah. Wewe unaona jua, mbingu na mambo mengine mengi bila ya kuyazunguka. Unayaona kwa jumla.

Hoja nyingine ni Kauli ya Allaah kumwambia Muusa:

لَن تَرَانِي

“Hutoniona.”[3]

Muusa alimwomba Mola Wake kama anaweza kumuona. Muusa katu asingeliweza kumuomba kitu kama hicho lau ingelikuwa haramu na jambo lisilowezekana kabisa. Kasema:

لَن تَرَانِي

“Hutoniona.”

Bi maana kwa hivi sasa:

فَلَمَّا تَجَلَّىٰ رَبُّهُ لِلْجَبَلِ جَعَلَهُ دَكًّا وَخَرَّ مُوسَىٰ صَعِقًا

“Basi Mola wako alipojidhihirisha katika mlima akalifanya livurugike kuwa vumbi na Muusa akaanguka hali ya kuzimia.”[4]

Muusa hawezi kumuona Allaah hapa duniani. Umbo la mwanaadamu haliwezi kumuona Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) hapa duniani. Vipi itawezekana na wakati Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema katika Hadiyth Swahiyh:

“Pazia Yake ni nuru. Lau Angeliifungua, basi nuru ya Uso Wake ungeliunguza kila anachokiona katika viumbe Wake.”[5]

Umbo la mwanaadamu kwa sasa haliwezi kumuona Allaah (Tabaarak wa Ta´ala). Vipi mwanaadamu ataweza kumuona Allaah (´Azza wa Jall) ikiwa mlima ulisagikasagika pindi alipojionyesha kwao? Lakini wakati Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) atapowafufua viumbe Wake na kuwaingiza Peponi atawapa maumbile na nguvu za kuweza kumuona Allaah (´Azza wa Jall).

Aayah nyingine ni:

لِّلَّذِينَ أَحْسَنُوا الْحُسْنَىٰ وَزِيَادَةٌ

“Kwa wale waliofanya mazuri watapata Pepo na zaidi.”[6]

Mtume mtukufu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameifasiri na kusema neno “zaidi” kunamaanishwa Kuonekana. Ameipokea Muslim katika “as-Swahiyh” yake kupitia kwa Suhayb[7]. Tafsiri hiyo hiyo ndio iliyotolewa na Maswahabah wengine (Radhiya Allaahu ´anhum). al-Husnaa ni Pepo na ziada ni Kuonekana kwa Allaah (Tabarak wa Ta´al) ambako ni bora zaidi kuliko Pepo yenyewe. Baada ya watu kuingia Peponi Allaah atawaambia:

“Mnataka nikuzidishieni?” Watasema: “Tutake nini?” Umeziangaza nyuso zetu, umetuingiza Peponi na kutupa hiki na kile.” Kisha Allaah ajionyeshe kwao ambapo hawatostarehe kwa neema yoyote wala kupata kitu ambacho ni kikubwa zaidi kuliko kumuona Allaah (Tabaarak wa Ta´ala).”

Kama tulivyosema Hadiyth zenye kuthibitisha kuonekana kwa Allaah ni karibu Hadiyth thelathini. Katika hizo ni Hadiyth iliyopokelewa na Jariyr na Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anhumaa):

“Mtamuona Mola wenu kama mnavyouona mwezi huu; hamtosongamana katika kumuona.”[8]

Kuna Hadiyth nyingi kuhusu hilo. al-Bukhaariy na Muslim wamepokea nyingi katika hizo.

[1] 2:223

[2] 06:103

[3] 7:143

[4] 7:143

[5] Muslim (179).

[6] 10:26

[7] Muslim (181).

[8] al-Bukhaariy (7437).

  • Mhusika: ´Allaamah Rabiy´ bin Haadiy al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Usuwl-is-Sunnah, uk. 380-381
  • Imechapishwa: 06/08/2017