16. Mitume wote walikuwa na dini moja


Mitume wote wamekuja kwa kampeni ya kulingania katika Tawhiyd na kukataza shirki. Hii ndio dini ya Mitume. Dini yao ilikuwa ni moja ijapokuwa Shari´ah zao ni zenye kutofautiana. Msingi na asili ya dini na ´Aqiydah yao ilikuwa moja: kumwabudu Allaah kwa mujibu wa Shari´ah Yake. Kwa mfano mwanzoni mwa Uislamu kuswali kwa kuelekea Yerusalemu ilikuwa ni ´ibaadah, kwa sababu Allaah ndiye kaamrisha hivo. Lakini baadaye hukumu hiyo ikafutwa na Qiblah kikabadilishwa kuelekea Ka´bah. Hivyo ´ibaadah ikawa ni kuelekea Ka´bah na kuelekea Yerusalemu kukawa kumekatazwa. Mwenye kuswali kuelekea Yerusalemu anazingatiwa ni kafiri. Allaah anapaswa kuabudiwa kwa mujibu wa ile Shari´ah alioweka katika wakati ule. Wakati Shari´ah ile inafutwa kunahamiwa katika ile Shari´ah iliofutwa na kunaachwa ile iliofutwa. Kwa hiyo dini ya Mitume ni moja ijapokuwa Shari´ah zao ni zenye kutofautiana. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amewafananisha Mitume kama ndugu wenye kuchangia baba na wenye mama tofauti. Kadhalika dini yao ni moja na Shari´ah yao ndio yenye kutofautiana, kutokana na hekima ya Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Allaah huweka katika Shari´ah yale yanayoendana na wakati huo, kila Ummah yale yanayosilihi kwao. Kwani Allaah ni mjuzi zaidi yale yanayosilihi kwa watu:

لِكُلٍّ جَعَلْنَا مِنكُمْ شِرْعَةً وَمِنْهَاجًا

“Kwa kila Ummah katika nyinyi Tumeujaalia Shari’ah na mfumo wake.”[1]

Midhali dini haijafutwa, basi Allaah atapaswa kuabudiwa kwayo. Ikifutwa basi kumwabudu Allaah kunakuwa kwa kuhamia katika kile kilichofuta na kuachana na kile kilichofutwa:

فَمِنْهُم مَّنْ هَدَى اللَّـهُ وَمِنْهُم مَّنْ حَقَّتْ عَلَيْهِ الضَّلَالَةُ

“Basi miongoni mwao wako ambao Allaah amewaongoza na miongoni mwao wako ambao umethibiti kwake upotevu.”[2]

Baadhi yao wamewaitikia Mitume na wengine wamekataa na kwa ajili hiyo wamehukumiwa upotevu. Kulikuwa kumeshakadiriwa kupotea kwa sababu ya ukafiri na ukaidi wao.

[1] 05:48

[2] 16:36

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: I´aanat-ul-Mustafiyd bi Sharh Kitaab-it-Tawhiyd, uk. 29-30
  • Imechapishwa: 12/08/2019