16. Ahl-us-Sunnah wako kati ya Murji-ah na Khawaarij

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Katika mlango wa matishio ya Allaah wako kati na kati baina ya Murji-ah na Wa´iydiyyah.

MAELEZO

Haya ni masuala ya kufuru na imani kwa waumini wenye kutenda madhambi makubwa kwa yule mwenye kufanya dhambi kubwa ilio chini ya shirki. Mfano wa madhambi hayo ni uzinzi, kuiba, kunywa pombe na madhambi makubwa mengineyo ambayo yako chini ya shirki.

Khawaarij wamemkufurisha na wamesema kuwa anatoka nje ya Uislamu na kuingia katika ukafiri. Wanatumia hoja kwa Aayah kutoka katika Qur-aan. Ni Aayah zisizokuwa wazi na hawazirejeshi katika Aayah zilizo wazi. Kwa mfano wa maneno Yake:

وَمَن يَعْصِ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ فَإِنَّ لَهُ نَارَ جَهَنَّمَ خَالِدِينَ فِيهَا أَبَدًا

“Yeyote atakayemuasi Allaah na Mtume Wake, basi hakika atapata Moto wa Jahannam hali ya kudumu humo milele.”[1]

Wametumia Aayah hii kwamba kila mwenye kumuasi Allaah ataingia Motoni na atadumishwa humo milele na kwamba ni kafiri. Matokeo yake wanamkufurisha mwizi, mzinzi na mwenye kunywa pombe. Kila mwenye kufanya dhambi kubwa wanamkufurisha na wanamtoka nje ya Uislamu. Kadhalika wanamdumisha Motoni milele akifa kabla ya kutubia. Haya ndio madhehebu ya Wa´iydiyyah. Ni kwa nini wakaitwa hivo? Wametendea kazi Aayah za matishio na wakaziacha Aayah za ahadi ambapo Allaah ameahidi msamaha na tawbah. Mfano wa Aayah hizo ni maneno Yake (Ta´ala):

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَاءُ

 “Hakika Allaah hasamehi kushirikishwa lakini anasamehe yaliyo chini ya hayo kwa amtakae.”[2]

Allaah ameeleza kuwa hamsamehi mwenye kufanya shirki kubwa na kwamba anasaemehe yale yote yaliyo chini ya shirki. Ndani yake kunaingia maasi aina yote. Hii ni ahadi ya Allaah (Jalla wa ´Alaa).

Upande wa pili Murji-ah, ambao ni Murji-ah, wanaosema kuwa mwenye kufanya dhmbi kubwa ni mwenye imani kamilifu wakatendea kazi ahadi. Wamesema kuwa imani haidhuriki kwa maasi kabisa kama ambavo matendo mema hayafai pamoja na ukafiri. Ndio wakaitwa “Murji-ah”. Kwa sababu wamechelewesha matendo nje ya imani na wamesema kuwa imani ni kule kusadikisha kwa moyo.

[1] 72:23

[2] 04:116

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh ´Aqiydat-il-Imaam Mujaddid Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab, uk. 34-35
  • Imechapishwa: 27/03/2021