15. Msingi wa sita: ni wenye nyoyo na ndimi zilizo salama kwa Maswahabah

Katika misingi ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah ni wenye nyoyo na ndimi zilizo salama kwa Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hivyo ndivyo alivyowasifu Allaah (Ta´ala) pindi alipowataja Muhaajiruun na Answaar na akawasifu kisha akasema (Ta´ala):

وَالَّذِينَ جَاءُوا مِن بَعْدِهِمْ يَقُولُونَ رَبَّنَا اغْفِرْ لَنَا وَلِإِخْوَانِنَا الَّذِينَ سَبَقُونَا بِالْإِيمَانِ وَلَا تَجْعَلْ فِي قُلُوبِنَا غِلًّا لِّلَّذِينَ آمَنُوا رَبَّنَا إِنَّكَ رَءُوفٌ رَّحِيمٌ

“Na wale waliokuja baada yao wanasema: “Mola wetu! Tusamehe sisi na ndugu zetu ambao wametutangulia kwa imani na wala Usijaalie katika nyoyo zetu mafundo ya chuki kwa wale walioamini. Mola wetu! Hakika Wewe ni Mwenye huruma mno, Mwenye kurehemu.””[1]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Msiwatukane Maswahabah wangu. Ninaapa kwa Yule ambaye nafsi yangu iko mkononi Mwake! Lau mmoja wenu atatoa dhahabu mfano wa [mlima wa] Uhud haitofikia robo wala nusu ya mmoja wao.”[2]

Hilo ni tofauti na wanavyofanya wazushi ambao ni Raafidhwah na Khawaarij ambao wanawatukana Maswahabah na wanakanusha fadhilah zao.

Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah wanaona kuwa kiongozi baada ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni Abu Bakr, kisha ´Umar, kisha ´Uthmaan kisha ´Aliy – Allaah awe radhi nao wote.

Atayesema vibaya uongozi wa mmoja wao katika hawa huyo ni mpotevu kuliko punda wa kufugwa kwa sababu atakuwa ameenda kinyume na Maandiko na maafikiano juu ya uongozi wa watu hawa kwa mpangilio huu.

[1] 59:10

[2] al-Bukhaariy (3470), Muslim (6541), at-Tirmidhiy (3861), Abu Daawuud (4658), Ibn Maajah (161) na Ahmad (03/55)

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Min Usuwl ´Aqiydah Ahl-is-Sunnah wal-Jamaa´ah, uk. 32-33
  • Imechapishwa: 12/05/2022