15. Mfano wa kumi kuonyesha jinsi Raafidhwah wanavodai kuwa Maswahabah wamepotosha Qur-aan

Shaykh wao al-Majlisiy amethibitisha mapokezi haya katika kitabu chake “Miraat-ul-´Uqul” na kusema:

“Hadiyth ni yenye kuthibiti.”

Kisha akasema:

“Mapokezi ni sahihi. Ni jambo lililo wazi ya kwamba mapokezi haya kama yalivo mapokezi mengine mengi yanaweka wazi kabisa juu ya kwamba Qur-aan imepunguzwa na kubadilishwa. Ninaonelea kuwa mapokezi haya juu ya mlango huu yamepokelewa kwa njia nyingi, Mutawaatir.”[1]

Vipi al-Majlisiy anaweza kusema ya kwamba kumepokelewa mapokezi kwa njia nyingi juu ya kwamba Qur-aan ambayo Jibriyl aliteremka nayo ilikuwa na Aayah 17.000 ikiwa kama ni mtu mmoja tu aliyesema hivo na kwamba wale waliopokea hilo kutoka kwake ni kundi la waongo? Je, madai haya yanakubaliwa hata na makafiri, seuze waislamu?

Nyinyi mnadai ya kwamba Qur-aan kamilifu iko kwa watu wa familia ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Ni kwa nini basi waifiche Qur-aan hiyo tangu wakati Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipofariki mpaka hivi leo ikiwa kama Allaah Alimtuma Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa walimwengu wote? Ni ufichaji upi mbaya kuliko huu? Allaah Amesema katika Kitabu Chake:

إِنَّ الَّذِينَ يَكْتُمُونَ مَا أَنزَلْنَا مِنَ الْبَيِّنَاتِ وَالْهُدَىٰ مِن بَعْدِ مَا بَيَّنَّاهُ لِلنَّاسِ فِي الْكِتَابِ ۙ أُولَـٰئِكَ يَلْعَنُهُمُ اللَّـهُ وَيَلْعَنُهُمُ اللَّاعِنُونَ

“Hakika wale ambao wanaficha yale Tuliyoyateremsha katika Hoja zilizo wazi na uongo baada ya kuwa Tumeyabainisha kwa watu katika Kitabu, hao Anawalaani Allaah na wanalaaniwa na kila mwenye kulaani.”[2]

Je, wale wenye busara hawaoni kuwa malengo ya Raafidhwah na uongo huu ni kuwatukana na kuwalaani watu watukufu wa nyumba ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)? Wanawalaani Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum) kwa njia ya moja kwa moja na watu wa familia ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa njia isiyokuwa ya moja kwa moja.

Madai haya ya uongo kwamba mapokezi haya yamepokelewa kupitia njia nyingi ni kama madai ya mayahudi na manaswara juu ya kwamba wamepokea kwa njia nyingi ya kuwa Masihi alisulubiwa na kwamba ´Iysaa ni mwana wa Allaah kwa mujibu wa manaswara na ´Uzayr ni mwana wa Allaah kwa mujibu wa mayahudi. Yote haya ni njama juu ya uongo. Raafidhwah hawana mapokezi yoyote isipokuwa ni katika uongo mkubwa.

Uongo huu unazunguka kwa watu wawili; Abu Ja´far na Abu ´Abdillaah. Je, mapokezi yaliyopokelewa kwa njia nyingi yanakuwa namna hii? Mapokezi kuwa yamepokelewa kupitia njia nyingi ina maana ya kwamba wapokezi ni wengi kwa msingi wa kwamba ni jambo lisilowezekana wakakubaliana juu ya uongo na kiasi cha wingi hao wameipokea kwa kila kundi – kuanzia mwanzo wa upokezi mpaka mwisho wake – na upokezi huo uwe umesikika au umeonekana. Makubaliano ya Raafidhwah juu ya uongo ni jambo rahisi sana kwao, lakini masharti mengine yote ni yenye kutengwa. Abu ´Abdillaah na Abu Ja´faar hawana lolote kuhusiana na Raafidhwah na kuvuka kwao mipaka na uongo wao juu ya Allaah, Kitabu Chake na Maswahabah wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

[1] Mir-aat-ul-´Uquul (12/525) kupitia kitabu cha ´Abdullaah bin Muhammad as-Salafiy ”Min ´Aqaa-id-ish-Shiy´ah”, uk. 20.

[2] 02:159

  • Mhusika: ´Allaamah Rabiy´ bin Haadiy al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Intiswaar li Kitaab-il-´Aziyz al-Jabbaar, uk. 42-43
  • Imechapishwa: 19/03/2017