15. Maana ya Twaaghuut


Allaah (Ta´ala) amesema:

أَنِ اعْبُدُوا اللَّـهَ

“Mwabuduni Allaah… “

Haya ni maamrisho.

وَاجْتَنِبُوا الطَّاغُوتَ

“… na jiepusheni na Twaaghuut!”

Haya ni makatazo kwa njia ya maamrisho. Twaaghuut inatumiwa kwa kila kitu kilichochupa mipaka kukiwemo shaytwaan (ambaye ndiye aina mbaya kabisa), wachawi, makuhani, watu wenye kuhukumu kinyume na Shari´h ya Allaah na watu wenye kuwaita watu kuwafuata katika maasi. Ibn-ul-Qayyim (Rahimahu Allaah) amesema:

“Twaaghuut ni kila chenye kuabudiwa, chenye kufuatwa na chenye kutiiwa ambacho kiumbe anapitiliza mipaka yake.”

Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) ametuamrisha kumwabudu Yeye na kujiepusha na Twaaghuut, bi maana kila chenye kuabudiwa badala ya Allaah. Masanamu, mizimu, makaburi na makuba ni mfano wa vinavyoabudiwa badala ya Allaah. Vyote hivi vinaitwa kuwa ni Twaaghuut. Lakini yule anayeabudiwa badala ya Allaah hali ya kuwa si mwenye kuridhia hilo haitwi hivo. ´Iysaa (´alayhis-Salaam) na waja wema kama mfano wa al-Hasan na al-Husayn (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ambao wanaabudiwa pasi na kuwa radhi hawaitwi Twaaghuut. Lakini kule kuwaabudu kwao ni Twaaghuut kwa sababu wanamwabudu shaytwaan. Kwa mfano wale wanaomwabudu al-Hasan ukweli wa mambo ni kwamba wanamwabudu shaytwaan ambaye ndiye kawaamrisha kufanya hivo:

وَيَوْمَ يَحْشُرُهُمْ جَمِيعًا ثُمَّ يَقُولُ لِلْمَلَائِكَةِ أَهَـٰؤُلَاءِ إِيَّاكُمْ كَانُوا يَعْبُدُونَ قَالُوا سُبْحَانَكَ أَنتَ وَلِيُّنَا مِن دُونِهِم ۖ بَلْ كَانُوا يَعْبُدُونَ الْجِنَّ ۖ أَكْثَرُهُم بِهِم مُّؤْمِنُونَ

“Siku atakayowakusanya wote kisha atawaambia Malaika: “Je, hawa  ndio waliokuwa wakikuabuduni?” Watasema: “Utakasifu ni Wako!” Wewe ni mlinzi badala yao! Bali walikuwa wakiabudu majini, wengi wao wakiwaamini.”[1]

Kutokana na Aayah hiyo mtu anatakiwa kuviepuka vile vyote vinavyoabudiwa badala ya Allaah. Katika Aayah nyingine imekuja:

فَمَن يَكْفُرْ بِالطَّاغُوتِ وَيُؤْمِن بِاللَّـهِ فَقَدِ اسْتَمْسَكَ بِالْعُرْوَةِ الْوُثْقَىٰ لَا انفِصَامَ لَهَا ۗ وَاللَّـهُ سَمِيعٌ عَلِيمٌ

“Basi atakayemkanusha Twaaghuut na akamuamini Allaah, hakika atakuwa ameshikilia imara kishikilio madhubuti kisichovunjika na Allaah ni Mwenye kusikia yote, Mjuzi wa yote.”[2]

Hii ndio maana ya hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah. Kwa sababu shahaadah maana yake ni kumkufuru Twaaghuut na kumwamini Allaah pekee, ni kama mfano wa maneno Yake:

أَنِ اعْبُدُوا اللَّـهَ وَاجْتَنِبُوا الطَّاغُوتَ

“Mwabuduni Allaah na jiepusheni na Twaaghuut!”

Hapa kuna makanusho na uthibitisho.

Zingatia Allaah ametuamrisha kuepuka, na si kuacha peke yake kuabudu Twaaghuut. Kwa sababu kukiepuka kitu kunakoleza makatazo zaidi kwa sababu maana yake ni kwamba mtu anapaswa kuepuka zile njia zote zinazopelekea katika shirki. Uepukaji una nguvu zaidi kuliko uachaji na maana ya kuepuka ni kwamba mtu aache shirki na vilevile aache kila kitu chenye kupelekea katika shirki. Aayah hii inathibitisha kwamba Mitume wametumilizwa kwa ujumbe wa Tawhiyd: kumwabudu Allaah peke yake na kujiepusha na aina zote za kuabudu Twaaghuut.

[1] 34:40-41

[2] 02:256

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: I´aanat-ul-Mustafiyd bi Sharh Kitaab-it-Tawhiyd, uk. 28-29
  • Imechapishwa: 12/08/2019