15. Kushuka kwa Allaah kwenye mbingu ya chini

al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye ameeleza kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mola Wetu (Tabaarak wa Ta´ala) huteremka katika mbingu ya chini pale kunapobaki theluthi ya mwisho ya usiku na husema: “Ni nani mwenye kuniomba nimuitikie? Ni nani mwenye kuniomba nimpe? Ni nani mwenye kuniomba msamaha nimsamehe?”[1]

Hadiyth hii imepokelewa na Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum) takriban ishirini . Ahl-us-Sunnah wameafikiana juu ya kuikubali.

Kushuka kwa Allaah (Ta´ala) katika mbingu ya dunia ni katika sifa Zake za kimatendo zinazohusiana na matakwa na hekima Yake. Ni ushukaji wa kikweli wenye kulingana na utukufu na ukubwa Wake. Si sahihi kupotosha maana yake na kusema ni kushuka amri Yake, kushuka rehema Zake au kushuka Malaika Wake. Hili ni batili kwa mitazamo ifuatayo:

1- Linaenda kinyume na udhahiri wa Hadiyth. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameegemeza ushukaji kwa Allaah (Ta´ala). Kimsingi ni kwamba kitu kinaegemezwa kwa yule ambaye kimetokea kwake au aliyekifanya. Pindi anapoegemezewa mtu mwengine, inazingatiwa kuwa ni upotoshaji wenye kupingana na ule msingi.

2- Tafsiri kama hiyo inapelekea maneno yawe na maana yenye kufutwa, kimsingi ni kutokuwepo ufutwaji.

3- Kushuka amri au rehema Zake ni jambo ambalo si maalum katika kipindi hichi cha usiku tu. Bali amri na rehema Zake hushuka kila wakati.

Endapo mtu atasema kuwa makusudio ni kushuka kwa amri maalum na rehema maalum. Katika hali hii mambo haya hayalazimishi kushuka kila wakati.

Haya yanaraddiwa kwa njia ya kwamba lau tutasema kuwa makisio haya na tafsiri hii ni sahihi, tunaona kuwa Hadiyth inasema kuwa jambo hili linateremka katika mbingu ya chini. Kuna faida ipi rehema ishuke mpaka katika mbingu ya chini mpaka Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aweze kutukhabarisha jambo hilo?

4- Hadiyth imejulisha kwamba Yule mwenye kushuka husema:

“Mola Wetu (Tabaarak wa Ta´ala) huteremka katika mbingu ya chini pale kunapobaki theluthi ya mwisho ya usiku na husema: “Ni nani mwenye kuniomba nimuitikie? Ni nani mwenye kuniomba nimpe? Ni nani mwenye kuniomba msamaha nimsamehe?”

hakuna hata mmoja awezaye kusema hivyo zaidi ya Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fath Rabb-il-Bariyyah, uk. 52-53
  • Imechapishwa: 28/04/2020