14. Wapelekee mambo yenye kutatiza wanachuoni

Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) amesema:

“Lililo juu yake ni kuziamini na kujisalimisHa nazo. Mfano wa Hadiyth hizo ni Hadiyth ya “mkweli na msadikishwaji” na Hadiyth kuhusu Qadar na Hadiyth nyengine zote kuhusu Kuonekana. Haijalishi kitu hata kama kuna ambao hawawezi kuzisikia au kuchukulia kwa ubaya kuzisikiza. Lililo juu yake ni kuziamini na asirudishe herufi hata moja kwenye Hadiyth hizo au nyenginezo zilizopokelewa kutoka kwa wapokezi waaminifu.”

MAELEZO

Hii ndio ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah pasi na kujali ni maudhui yepi. Ima mwanafunzi akajua maana ya maandiko na hivyo akazungumza kwa elimu na akawabainisha watu, au hajui. Katika hali hiyo asihukumu maandiko kwa akili na maoni yake. Wala haijuzu kwake akayarudisha. Midhali yamesihi kutoka kwa Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) basi ni lazima kuyaamini hata kama hajui maana yake. Ana haki ya kuuliza. Hata hivyo awaulize wanachuoni walio na ´Aqiydah na mfumo wa Salaf, na khaswa kuhusu mambo ya ´Aqiydah. Vivyo hivyo anatakiwa kufanya kila pale anapotatizwa na jambo. Jambo hilo linaweza kuwa linahusiana na Qadar au na majina na sifa za Allaah; anatakiwa kuwauliza wanachuoni ili abainikiwe na haki. Kuna maandiko ambayo yanaweza kumtatiza mjinga. Moja katika hayo ni yale yaliyopokelewa na ´Abdullaah bin Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye amesema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), ambaye ni mkweli na mwenye kusadikishwa, ametueleza: “Hakika kila mmoja wenu hukusanywa umbo lake katika tumbo la mama yake siku arubaini akiwa ni mkusanyiko wa mbegu. Kisha huwa donge la damu kwa muda kama huo. Kisha huwa pande la nyama kwa muda kama huo. Kisha Allaah humtumia Malaika na akampulizia roho na akaamrishwa aandike maneno manne; riziki yake, muda wake wa kuishi, matendo yake na kama atakuwa mtu muovu au mwema.”[1]

Haya yanaweza kuwatatiza watu wengi, lakini wanachuoni wanayajua. Wanajua kuwa uandishi huu ni wenye kuafikiana na yale yaliyoandikwa katika Ubao uliohifadhiwa yaliyoandikwa na kalamu kwa miaka 50.000 kabla ya kuumba mbingu, ardhi na viumbe vyengine vyote. Ni wajibu kutambua kwamba yale yaliyoandikwa pindi kipomoko kilipokuwa tumboni mwa mama ni yenye kuafikiana na yale yaliyomo kwenye Ubao uliohifadhiwa.

[1] al-Bukhaariy (6549) na Muslim (2643).

  • Mhusika: ´Allaamah Zayd bin Muhammad al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Latwiyfah ´alaa Usuwl-is-Sunnah al-Muniyfah, uk. 65-67
  • Imechapishwa: 07/10/2019