14. Wanandoa wote ni lazima waoane kwa kuridhiana


Miongoni mwa haki za wanandoa wakati wa kufunga ndoa ni pamoja na wanandoa kuoana hali ya kuwa ni wenye kuridhiana. Haijuzu kwa mlezi kumuozesha mwanamke kwa nguvu, ambaye ni bikira au asokuwa bikira, kinyume na ridhaa yake, pasina kujali ni njia ipi. Ridhaa ya mwanamke sio kwa yeye kusema tu ndio [nimekubali] pasina kujali ni njia ipi hata kama atakuwa ni mwenye kulazimishwa. Baadhi ya walezi wajinga wanampiga mwanamke na kumtisha kuwa kamwe hatomuozesha au kwamba atamtaliki mama yake ikiwa kama hakuolewa na mwanaume fulani. Ikiwa atakubali kuolewa naye mlezi huyu mjinga hufikiria kuwa ameridhia kuolewa naye. Uhakika wa mambo Allaah Anajua kuwa amelazimishwa. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yatima anatakiwa kuombwa idhini. Akinyamaza huko ndio kutoa kwake idhini na akikataa asimuozeshe.”[1]

“Asokuwa bikira asiozeshwe isipokuwa mpaka baada ya kutakwa ushauri wala bikira isipokuwa kwa idhini yake.” Wakasema: “Ni ipi idhini yake?” Akasema: “Kunyamaza kwake.”[2]

Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesema:

“Msichana bikira alikuja kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kusema kuwa baba yake amemuozesha kinyume na matakwa yake. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akampa khiyari.”[3]

[1] Abu Daawuud (2093), at-Tirmidhiy (1109), an-Nasaaiy (3270) na Ahmad (2/259) na (2/475). Nzuri kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”al-Irwaa’” (1834)

[2] al-Bukhaariy (5136), Muslim (1419) na Abu Daawuud (2092) na muundo ni wa kwake.

[3] Abu Daawuud (2096), Ibn Maajah (1875) na Ahmad (1/273). Swahiyh kwa njia zake zote kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh Sunan Abiy Daawuud” (6/1827)

  • Mhusika: Shaykh Sulaymaan bin Saliym ar-Ruhayliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Haqq-uz-Zawjayn, uk. 20-21
  • Imechapishwa: 24/03/2017