14. I´tikaaf na kuwekwa kwake katika Shari´ah

[1] I´tikaaf ni Sunnah katika Ramadhaan na masiku mengine ya mwaka. Msingi katika hilo ni maneno Yake (Ta´ala):

وَأَنتُمْ عَاكِفُونَ فِي الْمَسَاجِدِ

“Ilihali ni wenye kukaa I’tikaaf misikitini.”[1]

Kadhalika kumepokelewa Hadiyth nyingi Swahiyh juu ya I´tikaad yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Vivyo hivyo kumepokelewa mapokezi mengi kutoka kwa Salaf, kama ilivyotajwa katika “al-Muswannaf” ya Ibn Abiy Shaybah na “al-Muswannaf” ya ´Abdur-Razzaaq[2].

Imethibiti ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alifanya I´tikaaf katika yale masiku kumi ya mwisho ya Shawwaal[3] na kwamba ´Umar alisema kumwambia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Niliweka nadhiri katika kipindi cha ukafiri ya kwamba nitafanya I´tikaaf usiku mmoja katika msikiti Mtakatifu.” Ndipo akasema: “Tekeleza nadhiri yako [na ukae I´tikaaf usiku mmoja].”[4]

[2] Hata hivyo imekokotezwa zaidi katika Ramadhaan. Abu Hurayrah amesema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akikaa I´tikaaf masiku kumi katika kila Ramadhaan yale ilihali alikaa I´tikaaf masiku ishirini katika ule mwaka alokufa ndani yake.”[5]

[3] Lililo bora ni kufanya I´tikaaf mwishoni mwa Ramadhaan, kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akifanya I´tikaaf yale masiku kumi ya mwisho ya Ramadhaan mpaka pale Allaah (´Azza wa Jall) alipomfisha[6].

[1] 02:187

[2] Hapa katika lile chapisho lililotangulia kulikuwa Hadiyth juu ya fadhila za kitendo hicho “Yule mwenye kufanya I´tikaaf siku moja… “. Nikaona kuwa ni dhaifu na hivyo nikawa nimeiondosha baada ya kuitaja na kuizungumzia kwa upambanuzi katika “Silsilah al-Ahaadiyth adh-Dhwa´iyfah” (5347). Hapo nimeonyesha kasoro zake zilizokuwa zimefichikana na mimi na kabla yangu al-Haythamiy.

[3] Ni kipande cha Hadiyth ya ´Aaishah iliyopokelewa na al-Bukhaariy na Ibn Khuzaymah katika “as-Swahiyh” zao. Imetajwa katika “Swahiyh Abiy Daawuud” (2127).

[4] Ameipokea al-Bukhaariy, Muslim na Ibn Khuzaymah na nyongeza ni ya al-Bukhaariy katika upokezi mmoja, kama ilivyotajwa katika “al-Mukhtaswar”. Imetajwa vilevile katika “as-Swahiyh Abiy Daawuud” (2136-2137).

[5] Ameipokea al-Bukhaariy na Ibn Khuzaymah katika “as-Swahiyh” zao. Imetajwa katika marejeo yaliyotangulia (2126) na (2130).

[6] Ameipokea al-Bukhaariy, Muslim na Ibn Khuzaymah. Imetajwa katika “al-Irwaa´” (966) na “Swahiyh Abiy Daawuud” (2125).

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Qiyaam Ramadhwaan, uk. 34-35
  • Imechapishwa: 07/05/2019