136. Khidhr alikuwa Mtume au walii na bado yuko hai au amekwishakufa?

Wanachuoni wametofautiana kuhusu Khidhr. Je, ni Nabii au walii? Kuna maoni mawili:

Maoni ya kwanza: Imesemekana kwamba ni Nabii kwa sababu miujiza hii ambayo alifanya haiwi kwa mwengine zaidi isipokuwa Nabii.

Maoni ya pili: Ya kwamba alikuwa walii na si Nabii na mambo haya aliyoyafanya ni karama katika makarama ya mawalii na sio miujiza. Mawalii mikononi mwao kunapitika makarama na mambo yenye kwenda kinyume na mazowea.

Je, Khidhr yuko hai au ameshakufa?

Dalili sahihi zinafahamisha ya kwamba ameshakufa. Amesema (Ta´ala):

وَمَا جَعَلْنَا لِبَشَرٍ مِّن قَبْلِكَ الْخُلْدَ ۖ أَفَإِن مِّتَّ فَهُمُ الْخَالِدُونَ

”Hatukujaalia kwa mtu yeyote yule kabla yako aishi milele. Je, basi ukifa wewe wao watadumishwa milele?” (al-Anbiyaa´ 21:34)

Allaah (Jalla wa ´Alaa) ameeleza ya kuwa hakuna yeyote mwenye kuishi milele na kwamba viumbe wote watakufa:

كُلُّ مَنْ عَلَيْهَا فَانٍ وَيَبْقَى

”Kila aliyekuwa humo [ulimwenguni] ni mwenye kutoweka.” (ar-Rahmaan 55:26-27)

Khidhr ni mja katika waja wa Allaah na ni katika wanaadamu. Anafikwa na kutoweka kama wengine. Kisha lau angelikuwa hai, basi asingelikuwa na njia nyingine isipokuwa kuja na kumfuata Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ametumwa kwa watu wote. Angelikuwa hai wakati alipotumwa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), basi angelikuja kwake na akampa bay´ah na kumfuata. Haikutajwa kwamba aliwahi kuja kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Bais hii ni dalili ya kuwa ni ameshakufa. Haya ndio maoni yenye nguvu. Kuhusu wanaosema kwamba yuko hai hakuna dalili ya wazi.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Nawaaqidh-il-Islaam, uk. 178-179
  • Imechapishwa: 07/03/2019