Allaah amejithibitishia Mwenyewe katika Kitabu Chake na kupitia kwa Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwamba yuko pamoja na viumbe Wake. Miongoni mwa dalili za Qur-aan ni maneno Yake (Ta´ala):

وَهُوَ مَعَكُمْ أَيْنَ مَا كُنتُمْ

“Naye Yu pamoja nanyi popote mlipo.”[1]

وَأَنَّ اللّهَ مَعَ الْمُؤْمِنِينَ

“Na Allaah Yu Pamoja na waumini.”[2]

إِنَّنِي مَعَكُمَا أَسْمَعُ وَأَرَى

”Hakika Mimi Niko pamoja nanyi, Nasikia na Naona.”[3]

Miongoni mwa dalili za Sunnah ni pamoja vilevile na maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Imani bora kabisa ni wewe kutambua kuwa Allaah yuko pamoja nawe popote ulipo.”[4]

Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa salla) akimwambia rafiki yake Abu Bakr wakati walipokuwa pangoni:

لاَ تَحْزَنْ إِنَّ اللّهَ مَعَنَا

“Usihuzunike – hakika Allaah Yu Pamoja nasi!”[5]

Salaf na imamu wameafikiana juu ya hilo.

Upamoja kilugha maana yake ni matangamano na usuhubiano. Lakini hata hivyo muqtadha yake inategemea ni mazingira na hali gani inatumika. Lakini muqtadha yake hutegemea na mazingira ilivyotumika.

Wakati fulani inaweza kuwa na maana ya kuchanganyika. Mfano wa hilo ni kuchanga maji na maziwa.

Wakati mwingine inaweza kuwa na maana ya matishio na maonyo. Mfano wa hilo ni kama yule mtia adabu anavokwambia muhalifu:

“Nenda! Niko na wewe.”

Wakati mwingine inaweza kuwa na maana ya nusura na msaada. Mfano wa hilo ni kama mtu kusema kumwambia yule anayemuomba msaada:

“Niko pamoja nawe. Niko pamoja nawe.”

Haya na maneno kama haya ambayo yana matamshi moja lakini maana na muqtadha mbalimbali, inategemea yanaegemezwa katika kitu gani na katika mazingira na hali zipi yametajwa, baadhi ya watu wanaita kuwa ni maneno “yenye mashaka”. Sababu ni kwamba wanataka kumfanya msikilizaji atilie shaka kama matamshi yana tamshi moja na maana nyingine au tamshi na maana moja. Uhakika wa mambo ni katika aina ya maneno yaliyo na tamko na maana moja kwa sababu msingi wa lugha umelijenga tamko hili kwa maingiliano yenye kushirikiana. Tamko kuwa na hukumu na muqtadha zenye kutofautiana inatokamana na kwamba limetajwa katika mazingira mbalimbali. Hili halitokamani na ule msingi wa tamko lenyewe.

Yakibainika haya, itakuwa wazi kwamba upamoja ulioegemezwa kwa Allaah ni upamoja wa kihakika na sio upamoja wa majazi. Hata hivyo Allaah kuwa pamoja na viumbe ni upamoja maalum wenye kulingana Naye. Sio kama upamoja wa viumbe baina yao. Upamoja huu uko juu na ni mkamilifu zaidi. Upamoja huu hauna malazimisho kama upamoja wa viumbe kati yao.

Baadhi ya Salaf wamefasiri Allaah kuwa pamoja na viumbe Wake ni kwa ujuzi Wake kwao. Ni sehemu katika malazimisho ya tafsiri ya upamoja. Lengo lao ni kuwaraddi Huluuliyyah Jahmiyyah ambao wamesema kuwa Allaah kwa dhati yake yuko kila mahali. Dalili yao ilikuwa ni Aayah za upamoja. Ndipo Salaf wakabainisha kuwa haina maana kuwa yuko pamoja nasi kwa dhati Yake. Ni jambo lisilowezekana kabisa kwa akili na kwa Shari´ah. Kwa sababu ni jambo lenye kupingana na ulazima wa ujuu na wakati huohuo linapelekea awe Amezungukwa na viumbe Wake, jambo ambalo haliwezekani kabisa.

Upamoja wa Allaah na viumbe Wake umegawanyika aina mbili, wa wenye kuenea na maalum.

1- Wenye kuenea una maana ya kwamba Allaah amewazunguka viumbe wote, waumini na makafiri, wema na waovu, kwa ujuzi, uwezo, kuwaendesha, ufalme na mengineyo yenye maana ya uola Wake. Aina ya upamoja huu unampelekea yule mwenye kuuamini awe daima ni mtambuzi kuwa Allaah (´Azza wa Jall) ni mwenye kumchunga. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Imani bora kabisa ni wewe kutambua kuwa Allaah yuko pamoja nawe popote ulipo.”

Mfano wa upamoja huu ni maneno ya Allaah (Ta´ala):

وَهُوَ مَعَكُمْ أَيْنَ مَا كُنتُمْ

“Naye Yu pamoja nanyi popote mlipo.”[6]

أَلَمْ تَرَ أَنَّ اللَّهَ يَعْلَمُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ مَا يَكُونُ مِن نَّجْوَى ثَلَاثَةٍ إِلَّا هُوَ رَابِعُهُمْ وَلَا خَمْسَةٍ إِلَّا هُوَ سَادِسُهُمْ وَلَا أَدْنَى مِن ذَلِكَ وَلَا أَكْثَرَ إِلَّا هُوَ مَعَهُمْ أَيْنَ مَا كَانُوا

“Je, huoni kwamba Allaah Anajua yale yote yaliyomo mbinguni na yale yote yaliyomo ardhini? Hauwi mnong’ono wa watatu isipokuwa Yeye ni wa nne wao, na wala watano isipokuwa Yeye ni wa sita wao, na wala [hauwi mnong’ono wa] chini kuliko ya hivyo, na wala wa wengi zaidi isipokuwa Yeye Yu pamoja nao popote watakapokuwa.”[7]

2- Maalum una manaa ya nusura na msaada kwa yule mwenye kuegemezewa nao. Ni upamoja maalum kwa yule mwenye kuustahiki kati ya Mitume na wafuasi zao. Mfano wa upamoja huu ni maneno ya Allaah (Ta´ala):

وَأَنَّ اللّهَ مَعَ الْمُؤْمِنِينَ

“Na Allaah Yu Pamoja na waumini.”[8]

إِنَّ اللّهَ مَعَ الَّذِينَ اتَّقَواْ وَّالَّذِينَ هُم مُّحْسِنُونَ

”Hakika Allaah Yu Pamoja na wenye taqwa na wale ambao wao ni wema.”[9]

إِنَّنِي مَعَكُمَا أَسْمَعُ وَأَرَى

”Hakika Mimi Niko pamoja nanyi; Nasikia na Naona.”[10]

لاَ تَحْزَنْ إِنَّ اللّهَ مَعَنَا

“Usihuzunike – hakika Allaah Yu Pamoja nasi!”[11]

Huenda mtu akauliza upamoja ni katika sifa za Allaah za kidhati au za kimatendo. Upamoja wenye kuenea ni katika sifa za kidhati kwa sababu muqtadha yake Allaah anasifika nao milele. Kuhusiana na upamoja wa kimaalum, ni katika sifa za Allaah za kimatendo. Kwa sababu muqtadha yake unategemea na sababu zake. Upamoja huu unapatikana pale kunapokuwepo sababu na kinyume chake.

[1] 57:04

[2] 08:19

[3] 20:46

[4] at-Twabaraaniy katika ”al-Kabiyr” na ”al-Awsatw”, iliyotajwa katika ”Majma´-uz-Zawaa-id” (1/60), al-Bayhaqiy katika ”al-Asmaa’ was-Swifaat” (907) na Abu Nu´aym katika ”al-Hilyah” (6/124).

[5] 09:40

[6] 57:04

[7] 58:07

[8] 08:19

[9] 16:128

[10] 20:46

[11] 09:40

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fath Rabb-il-Bariyyah, uk. 46-48
  • Imechapishwa: 26/04/2020