Maneno Yake:

 وَتَوَاصَوْا بِالصَّبْرِ

“… na wakausiana kuwa na subira.”

Subira juu ya yanayowafika. Maana ya subira kilugha ni kujizuia. Makusudio yake hapa ni kuizuia nafsi katika kumtii Allaah. Imegawanyika aina tatu:

Ya kwanza: Subira katika kumtii Allaah.

Ya pili: Subira juu ya yale Allaah aliyoharamisha.

Ya tatu: Subira juu ya makadirio ya Allaah.

1- Mtu anatakiwa kuwa na subira juu ya kumtii Allaah. Kwa sababu nafsi inapenda uvivu na inapenda raha. Kwa hiyo ni lazima kwa mtu kuisubirisha juu ya matendo mema, swalah, funga na jihaad katika njia ya Allaah. Ingawa inayachukia mambo haya aisubirishe na aizuie juu ya kumtii Allaah.

2- Subira juu ya yale Allaah aliyoharamisha. Nafsi inapenda mambo ya haramu na mambo ya matamanio. Inavutika huko. Kwa hivyo ni lazima aifungamanishe na aizuie kutokamana na mambo ya haramu. Jambo hili linahitajia subira. Si jambo lepesi kuinyima nafsi matamanio ya haramu. Ambaye hana subira nafsi yake inamshinda na inamvuta katika mambo ya haramu.

3- Subira juu ya makadirio ya Allaah machungu: Ni ile misiba inayomfika mtu katika kufisha ndugu wa karibu, kupoteza mali au maradhi yanayomfika mtu. Ni lazima asubiri juu ya mipango na makadirio ya Allaah. Asivunjike moyo na wala asikasirike. Bali auzuie mdomo kutokamana na makelele, kukasirika na aizuie nafsi kutokamana na kuvunjika moyo na avizuie viungo kutokamana na kujipiga makofi na kupasua nguo. Huku ndio kusubiri juu ya misiba.

Kuhusu madhambi asifanye subira kwayo. Bali anatakiwa kutubu kwayo na ayakimbie mbali. Lakini wakati wa misiba ambayo haitokani na wewe bali imetokana na Allaah (´Azza wa Jall) ambayo Allaah ima amekukadiria nayo kwa ajili ya kukupa majaribio na mtihani au amekuadhibu kwayo kutokana na madhambi ya matendo yako, kama alivosema (Ta´ala):

وَمَا أَصَابَكُم مِّن مُّصِيبَةٍ فَبِمَا كَسَبَتْ أَيْدِيكُمْ وَيَعْفُو عَن كَثِيرٍ

“Haukusibuni katika msiba wowote isipokuwa ni kutokana na yale yaliyochuma mikono yenu na anasamehe mengi.”[1]

Muislamu anapofikwa na msiba kwake mwenyewe, mali yake, mtoto wake, ndugu yake au mmoja katika ndugu zake wa waislamu basi ni lazima kwake kufanya subira na kutarajia malipo kutoka kwa Allaah. Amesema (Ta´ala):

الَّذِينَ إِذَا أَصَابَتْهُم مُّصِيبَةٌ قَالُوا إِنَّا لِلَّـهِ وَإِنَّا إِلَيْهِ رَاجِعُونَ أُولَـٰئِكَ عَلَيْهِمْ صَلَوَاتٌ مِّن رَّبِّهِمْ وَرَحْمَةٌ ۖ وَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُهْتَدُونَ

“Wale ambao unapowafika msiba husema ´Hakika sisi ni wa Allaah na hakika sisi Kwake tutarejea`. Hao zitakuwa juu yao barakah kutoka kwa Mola wao na rehema na hao ndio wenye kuongoka.”[2]

Hii ndio subira. Miongoni mwa hayo ni kufanya subira juu ya maudhi wakati wa kulingania kwa Allaah (´Azza wa Jall). Hakika haya ni miongoni mwa majanga. Ni lazima kwako kufanya subira juu ya yale maudhi yanayokupata katika njia ya kheri. Usiache kufanya matendo ya kheri. Kwa sababu baadhi ya watu wanataka kufanya kheri lakini wanapokabiliwa na kitu kinachowachukiza wanasema kuwa sio wajibu wao kuziingiza nafsi zao katika mambo hayo. Matokeo yake wakiwa ni waalimu wanaacha kufundisha, wanaacha kulingania kwa Allaah, akiwa ni Khatwiyb wa msikiti basi anaacha kutoa Khutbah, anaacha kazi ya uimamu msikitini na anaacha kuamrisha mema na kukataza maovu. Huyu hakusubiri juu ya yale maudhi yanayomfika. Ikiwa kosa limetokana na wewe basi ni lazima kwako kurejea katika haki na usahihi. Lakini midhali uko katika haki na hukukosea basi ni lazima kwako kufanya subira na kutarajia malipo kutoka kwa Allaah, uhisi kuwa jambo hilo ni katika njia ya Allaah (´Azza wa Jall), kwamba ni mwenye kupewa thawabu kwayo na ukumbuke yaliyowapitikia Mitume (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam) na ni vipi walisubiri na wakapambana katika njia ya Allaah mpaka Allaah (´Azza wa Jall) akawanusuru.

[1] 42:03

[2] 02:156-157

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 32-36
  • Imechapishwa: 25/11/2020