1 – Ni haramu kumjamii mwanamke kwenye tupu ya mbele katika hali ya hedhi. Amesema (Ta´ala):

وَيَسْأَلُونَكَ عَنِ الْمَحِيضِ ۖ قُلْ هُوَ أَذًى فَاعْتَزِلُوا النِّسَاءَ فِي الْمَحِيضِ ۖ وَلَا تَقْرَبُوهُنَّ حَتَّىٰ يَطْهُرْنَ

“Wanakuuliza kuhusu hedhi. Sema: “Hiyo ni dhara, hivyo basi waepukeni wanawake katika hedhi. Wala msiwakaribie kujimai nao mpaka watwaharike.”[1]

Uharamu huu ni wenye kuendelea mpaka pale itapokatika damu hii ya hedhi na akaoga. Amesema (Ta´ala):

وَلَا تَقْرَبُوهُنَّ حَتَّىٰ يَطْهُرْنَ ۖ فَإِذَا تَطَهَّرْنَ فَأْتُوهُنَّ مِنْ حَيْثُ أَمَرَكُمُ اللَّـهُ

“Wala msiwakaribie kujimai nao mpaka watwaharike. Watakapotwaharika basi waendeeni kupitia pale alipokuamrisheni Allaah.”[2]

Ni halali kwa mume wa mke huyu mwenye hedhi kustarehe naye mbali na kumjamii kwenye tupu ya mbele. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Fanyeni kila kitu isipokuwa tendo la ndoa.”

Ameipokea Muslim.

2 – Mwanamke mwenye hedhi ataacha kufunga na kuswali katika kipindi cha hedhi yake. Ni haramu kwake kufanya mawili hayo na wala hayasihi kutoka kwake. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Je, pale mwanamke anapopata hedhi si haswali na wala hafungi?”

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

Mwanamke mwenye hedhi akitwahirika basi atalipa swawm na wala hatolipa swalah. ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesema:

“Tulikuwa tukipata hedhi wakati wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na tulikuwa tukiamrishwa kulipa swawm na wala hatuamrishwi kulipa swalah.”

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

Tofauti – na Allaah ndiye mjuzi zaidi – ni kwamba swalah ni yenye kukariri na hivyo ndio maana ikawa sio wajibu kuilipa kutokana na uzito na ugumu wa kufanya hivo tofauti na swawm.

3 – Ni haramu kwa mwanamke mwenye hedhi kugusa msahafu pasi na kizuizi. Amesema (Ta´ala):

لَّا يَمَسُّهُ إِلَّا الْمُطَهَّرُونَ

“Haigusi isipokuwa waliotakaswa kabisa.”[3]

Kadhalika kutokana na ile barua ambayo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimwandikia ´Amr bin Hamz:

“Asiuguse msahafu isipokuwa aliye twahara.”

Ameipokea an-Nasaa´iy na wengineo. Jambo hilo limefanana na Mutawaatir kutokana na vile watu walivyolipokea. Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema:

“Madhehebu ya maimamu wane ni kwamba asiuguse msahafu isipokuwa aliye twahara.”

Kuhusu mwanamke kusoma Qur-aan bila kuigusa ndipo mahali ambapo wanachuoni wametofautiana. Lililo salama zaidi ni yeye asiisome Qur-aan isipokuwa wakati wa dharurah, kama kwa mfano akichelea kuisahau. Allaah ndiye mjuzi zaidi.

4 – Ni haramu kwa mwanamke mwenye hedhi kufanya Twawaaf kwenye Ka´bah. Alisema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)  kumwambia ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) wakati alipopata hedhi:

“Fanya yale anayofanya mwenye kuhiji isipokuwa tu usifanye Twawaaf kwenye Nyumba mpaka utwahirike.”

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

5 – Ni haramu kwa mwanamke mwenye hedhi kubaki ndani ya msikiti. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Mimi siuhalalishi msikiti kwa aliye na hedhi wala na janaba.”

Ameipokea Abu Daawuud.

“Msikiti hauhalaliki kwa mwenye hedhi wala mwenye janaba.”

Ameipokea Ibn Maajah.

Inafaa kwake kupita msikitini pasi na kukaa. ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesimulia: “Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisema: “Nipe mkeka huo wa kuswali msikitini.” Nikasema: “Mimi niko na hedhi.” Akasema: “Hakika hedhi yako haiko mikononi mwako.”[4]

Hakuna neno kwa mwanamke mwenye hedhi kusoma Adhkaar za Kishari´ah kama kusema “Laa ilaaha illa Allaah, Allaahu Akbar, Subhaan Allaah”, du´aa na kusoma Adhkaar zilizowekwa katika Shari´ah za asubuhi na jioni, wakati wa kulala na wakati wa kuamka. Hakuna ubaya vilevile akasoma vitabu vya elimu kama mfano wa Tafsiyr ya Qur-aan, Hadiyth na Fiqh.

[1] 02:222

[2] 02:222

[3] 56:79

[4] Yamesemwa na mtunzi wa “al-Muntaqaa”. Wameipokea kundi isipokuwa al-Bukhaariy (01/140).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tanbiyhaat, uk. 25-30
  • Imechapishwa: 24/10/2019