13. Hakuna kinachokuwa ila kile alichotaka Allaah


Abu Ja´far at-Twahaawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

8- Wala hakuna kinachokuwa isipokuwa yale ayatakayo.

MAELEZO

Hapa kunathibitishwa Qadar na utashi wa Allaah. Hakukuwi katika umiliki Wake na viumbe isipokuwa yale aliyoyataka Yeye (Subhaanahu wa Ta´ala) kwa matakwa Yake ya kilimwengu:

إِنَّمَا أَمْرُهُ إِذَا أَرَادَ شَيْئًا أَن يَقُولَ لَهُ كُن فَيَكُونُ

”Hakika amri Yake anapotaka chochote hukiambia: “Kuwa!” nacho huwa.”[1]

Kila kitu katika kheri na shari kinatokana na utashi Wake wa kilimwengu. Hakuna chochote kinachotoka nje ya utashi Wake. Hapa kuna Radd kwa Qadariyyah ambao wanakanusha Qadar. Wanadai kwamba mja ndiye ambaye anayaumba matendo yake mwenyewe. Huku ni kumfanya Allaah ni Mwenye kushindwa kwa sababu mambo yanapitika pasi na kutaka Kwake (Subhaanah). Ni kumtia mapungufu. Uhakika wa mambo ni kwamba hakuna kheri wala shari yoyote inayopitika ulimwenguni isipokuwa kwa utashi wa Allaah. Anaumba kheri kwa hekima na anaumba shari kwa hekima. Kwa upande wa uumbaji Wake yale ya shari sio shari, kwa sababu ameumba kwa malengo makubwa. Malengo ni majaribio na mtihani ili kupambua vibaya na vizuri. Baada ya hapo kila mmoja alipwe kwa lile alilotenda zuri na ovu. Yeye (Subhaanahu wa Ta´ala) anakiumba kila kitu kwa hekima. Haumbi chochote mchezomchezo.

[1] 36:82

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Mukhtaswarah ´alaal-´Aqiydah at-Twahaawiyyah, uk. 36-37
  • Imechapishwa: 11/09/2019