13. Elimu inapelekea katika uongofu na ujinga unapelekea katika upotevu

Wakatendea kazi yale waliyoletewa na Mitume Yake na kufikishwa na Vitabu Vyake. Wakajifunza yale Aliyowafunza… – Ni lazima kujifunza Qur-aan na Sunnah na kuvifahamu kama alivyokusudia Allaah na Mtume Wake. Yule ambaye anaipa mgongo Qur-aan na Sunnah ananyimwa uongofu. Kujifunza elimu yenye manufaa, kuitendea kazi na kuipupia, bi maana elimu aliyokuja nayo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni katika sababu za uongofu. Ama yule ambaye anaipa mgongo ananyimwa uongofu. Amesema (Ta´ala):

وَالَّذِينَ كَفَرُوا عَمَّا أُنذِرُوا مُعْرِضُونَ

“Na wale waliokufuru kwa yale wanayoonywa kwayo ni wenye kukengeuka.”[1]

Kuipa mgongo haki, kuipuuza na kutoikubali kunasababisha upotevu na upindaji.

… wakasimama pale Alipowawekea mpaka waliowekewa… – Miongoni mwa sifa za Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah ni kwamba wanasimama katika mpaka wa elimu. Yale wanayoyajua wanayazungumza. Yale wasiyoyajua wanayanyamazia. Amesema (Ta´ala):

وَلَا تَقْفُ مَا لَيْسَ لَكَ بِهِ عِلْمٌ

“Wala usifuatilie yale usiyo na elimu nayo.”[2]

Bi maana usipaparike na usizungumze juu ya Allaah usiyoyajua. Simama kwenye mpaka wako. Yale unayoyajua katika elimu yenye manufaa yazungumze na toa fatwa kwayo na yale usiyoyajua komeka hapo mpaka kwanza uyajue. Namna hii ndivo wanavokuwa waumini.

… na wakaachana na wakatosheka na yale Aliyowahalalishia kutokamana na yale Aliyowaharamishia – Miongoni mwa sifa zao ni kwamba wanatosheka na halali kutokamana na haramu na wanatosheka na vizuri kutokamana na vichafu. Hili linahusu chakula, mavazi, vinywaji na wanawake wao. Wanatosheka na yale aliyohalalalisha Allaah na wanajiepusha na yale aliyowaharamishia. Amesema (Ta´ala) miongoni mwa sifa za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

يَأْمُرُهُم بِالْمَعْرُوفِ وَيَنْهَاهُمْ عَنِ الْمُنكَرِ وَيُحِلُّ لَهُمُ الطَّيِّبَاتِ وَيُحَرِّمُ عَلَيْهِمُ الْخَبَائِثَ وَيَضَعُ عَنْهُمْ إِصْرَهُمْ وَالْأَغْلَالَ الَّتِي كَانَتْ عَلَيْهِمْ

“Anawaamrisha mema na anawakataza maovu na anawahalalishia vizuri na anawaharamishia maovu na anawaondoshea mizigo yao na minyororo iliyokuwa juu yao.”[3]

[1] 46:3

[2] 17:36

[3] 7:157

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bayaan-ul-Ma´aaniy fiy Sharh Muqaddimati Ibn Abiy Zayd al-Qayrawaaniy, uk. 17-18
  • Imechapishwa: 06/07/2021