Hadiyth hii inafahamisha kwamba watu huigiliza kitendo cha mtu zaidi kuliko maneno makavu. Kwa sababu mtu akiwanasihi watu na asifanya matendo, watu watamkubalia muda wa kuwa wanamwamini. Lakini pale ambapo yeye mwenyewe atafanya basi kunakuwa na uwezekano mkubwa wa wao kumkubalia. Haya yanaonyesha tabia nzuri ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na uzuri wa kufunza kwake ambapo anawafunza watu kwa njia itayowayakinaisha.

Katika zama za Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) wamongolia waliizingira Shaam katika Ramadhaan na jeshi la Shaam lilikuwa limefunga. Kufunga na wakati huohuo kumzuia adui ni jambo gumu, wakawauliza wanachuoni ambapo wakawajibu kuwa haijuzu kula kwa sababu sio wagonjwa wala hawako safarini. Wakamuuliza pia Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah ambapo akawajibu kwamba wale ili waweze kupambana na adui. Kisha akatumia dalili kwa maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuwaambia waislamu wakati walipouteka mji wa Makkah:

“Nyinyi kesho mtakutana na adui. Kula ndio kunakutieni nguvu zaidi; hivyo basi kuleni.”[1]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akawaamrisha wale na sababu yake ni kwamba kula kunawatia nguvu zaidi na si kwa sababu walikuwa wasafari, kwa kuwa wao walikuwa tayari ni wasafiri.  Hiyo ni dalili inayojulisha kuwa inafaa kwa mpambanaji kula ikiwa kula kunamtia nguvu zaidi ya kupambana na adui. Pamoja na kwamba Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) aliwapa fatwa hiyo, lakini baadhi ya wanajeshi wakaendelea kufunga kutokana na ile fatwa nyingine iliyotolewa na wale wanachuoni wengine. Ndipo akashika mkate mkononini na anatembea kati ya safu za wapambanaji akawa anakula na huku wanamtazama. Yeye pia (Rahimahu Allaah) alikuwa ni mpambanaji na alikuwa miongoni mwa watu wenye ushujaa zaidi kwenye mapambano. Alifanya hivo ili wamuone na wakinaike kwa jambo hilo na hivyo wapate nguvu zaidi za mapambano[2]. Hichi ndio mfano wa kitendo cha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hakutuma mjumbe kuwaambia watu wafungue; bali yeye mwenyewe alifungua mbele za watu ambapo watu nao wakamuigiliza.

Mfano mwingine wa hili ni pindi Quraysh walipomzingira Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahabah wake Hudaybiyah. Wakati Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahabah walipokuwa njia kuelekea Makkah kwa ajili ya kufanya ´Umrah Quraysh waliwazuia, kwa sababu wao ndio walikuwa wakiitawala Makkah kipindi hicho. Ndipo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akawaamrisha Maswahabah wake kutoka katika Ihraam, kunyoa vichwa vyao, kuchinja vichinjwa vyao na warejee Madiynah kutokana na zile sharti maalum walizowekeana. Hakuna yeyote aliyeitikia. Hawakufanya hivo kwa sababu ya kumwasi Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), lakini ilikuwa ni kwa sababu ya kutaraji pengine atabadili msimamo. Akamweleza jambo hilo mmoja katika wakeze na akamshauri yeye aanze kunyoa kichwa chake mbele yao. Akafanya hivo ambapo Maswahabah wakakaribia kugombana ni nani katika yao ataanza kunyolewa[3]. Hiyo ni dalili inayoonyesha kuwa watu wanakinaika zaidi kwa kitendo kuliko maneno. Hii ndio njia ambayo mwanafunzi anatakiwa kushika wakati anapolingania kwake kwa Allaah ili ulinganizi wao uwe ni wenye kukinaisha zaidi na zaidi.

[1] Muslim (1120).

[2] al-Bidaayah wan-Nihaayah (14/30).

[3] al-Bukhaariy (2731).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ash-Sharh al-Mukhtaswar ´alaa Buluugh-il-Maraam (2/419-420)
  • Imechapishwa: 25/04/2020