Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Abu Waaqid al-Laythiyy (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Tulitoka pamoja na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwenda Hunayn na sisi ndio punde tu tumetoka katika ukafiri. Washirikina walikuwa na mkunazi unaoitwa “Dhaat Anwaatw” wakiuadhimisha na kutundika silaha zao. Tukapita karibu na mkunazi huo tukasema: “Ee Mtume wa Allaah, tufanyie Dhaat Anwaatw kama jinsi na wao walivyokuwa na Dhaat Anwaatw. Ndipo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Subhaan Allaah! Haya ndio yaleyale yaliyosemwa na watu wa Muusa: “Tufanyie mungu kama jinsi na wao walivyokuwa na mungu.” Ninaapa kwa yule ambaye nafsi yangu iko mikononi Mwake; mtafuata desturi za waliokuwa kabla yenu.””[1]

MAELEZO

Abu Waaqid al-Laythiy (Radhiya Allaahu ´anh) alikuwa ni mmoja katika wale waliosilimu mwaka wa Ushindi wa nane baada ya Kuhajiri.

Maneno yake mtunzi:

“Unaoitwa “Dhaat Anwaatw.”

ni wingi wa “Nawtw” ikiwa na maana ya kutundika. Walikuwa wakitundika silaha zao kwa ajili ya kutafuta baraka. Haya yalisemwa na Maswahabah ambao wamesilimu karibuni na bado hawajaielewa Tawhiyd vizuri:

“… tufanyie Dhaat Anwaatw kama jinsi na wao walivyokuwa na Dhaat Anwaatw… “

Huu ndio mtihani wa kufuata kichwa mchunga na kuiga. Huu ndio mtihani mkubwa. Hapo ndipo alistaajabu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwelikweli na akasema:

“Allaahu Akbar! Allaahu Akbar! Allaahu Akbar!”

Alikuwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anaposhangazwa na kitu au anapokemea jambo,  basi husema kwa kukariri “Allaahu Akbar” au “Subhaan Allaah! Mtafuata desturi za waliokuwa kabla yenu.”

Bi maana njia wanazopita juu yake watu na baadhi kuwaigiliza wengine. Hakuna kilichowafanya kusema haya isipokuwa kuwafuata wa kale na kujifananisha na washirikina.

“Haya ndio yaleyale yaliyosemwa na watu wa Muusa: “Tufanyie mungu kama jinsi na wao walivyokuwa na mungu.”

Baada ya Muusa (´alayhis-Salaam) kuvuka bahari na wana wa israaiyl na Allaah akamzamisha adui yao ilihali wanashuhudia, waliwapitia watu waliokuwa wakiyaadhimisha masanamu yao. Watu hawa wakamwambia Muusa (´alayhis-Salaam):

اجْعَل لَّنَا إِلَـٰهًا كَمَا لَهُمْ آلِهَةٌ ۚ قَالَ إِنَّكُمْ قَوْمٌ تَجْهَلُونَ

“Hebu tufanyie na sisi mungu kama hawa walivyokuwa na miungu. [Muusa] akasema: “Hakika nyinyi ni watu mnaofanya ujahili.””

Akawakemea na kuwaambia:

إِنَّ هَـٰؤُلَاءِ مُتَبَّرٌ مَّا هُمْ فِيهِ

“Hakika hawa yatateketezwa yale waliyo nayo… “

Bi maana batili:

وَبَاطِلٌ مَّا كَانُوا يَعْمَلُونَ

“… na ni yenye kubatilika yale waliyokuwa wakiyatenda.”

Kwa sababu kitendo ni cha shirki:

أَغَيْرَ اللَّـهِ أَبْغِيكُمْ إِلَـٰهًا وَهُوَ فَضَّلَكُمْ عَلَى الْعَالَمِينَ

“Je, nikutafutieni mungu asiyekuwa Allaah na hali Yeye amekufadhilisheni juu ya walimwengu?” (07:140)

Akawakemea (´alayhis-Swalaatu was-Salaam) kama ambavyo Mtume wetu Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) pia aliwakemea watu hawa. Lakini pamoja na hivyo watu hawa hawakushirikisha. Wana wa israaiyl hawakufanya shirki, kwa sababu hawakufanya jambo hilo. Vivyo hivyo Maswahabah hawa; lau wangechukua Dhaat Anwaatw wangelikuwa wametumbukia katika shirki. Lakini Allaah akawakinga. Pindi Mtume wao alipowakataza, wakajiepusha. Walisema maneno haya kwa sababu ya ujinga, na si kwa kukusudia. Pindi walipotambua kuwa kitendo hicho ni shirki, wakakomeka na hawakufanya kitu. Laiti wangelifanya basi wangekuwa wamemshirikisha Allaah (´Azza wa Jall).

Kikusudiwacho katika Aayah ni kwamba kuna ambao wanaabudu miti. Washirikina hawa walichukua Dhaat Anwaatw na vivyo hivyo Maswahabah hawa kutokana na uchache wa elimu walijaribu kujifananisha na washirikina, lakini Allaah akawa amewalinda kupitia Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Kinacholengwa ni kuwa kuko ambao wanatafuta baraka kupitia miti na kuiadhimisha. Kuiadhimisha maana yake ni kubaki karibu nayo kwa muda mrefu kwa ajili ya kujikurubisha kwayo. Uadhimisho ni kubaki maeneo fulani.

Haya yanafahamisha mambo mengi makubwa:

1 – Ukhatari wa kuwa na ujinga juu ya Tawhiyd. Ambaye ni mjinga juu ya Tawhiyd ni vyepesi kwake kutumbukia ndani ya shirki bila yeye kujua. Kuanzia hapa ni wajibu kujifunza Tawhiyd na kujifunza yenye kupingana nayo, ambayo ni shirki, ili mtu aweze kuwa juu ya yakini na ujuzi. Hili khaswa pale ambapo mtu atamuona mwenye kufanya hivo na huku akidhani kuwa ni haki kwa sababu ya ujinga. Hapa kuna ukhatari wa ujinga na khaswa katika mambo ya ´Aqiydah.

2 – Katika Hadiyth kuna ukhatari wa kujifananisha na washirikina. Kujifananisha huku kunaweza kupelekea katika shirki. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Yeyote atakayejifananisha na watu, basi yeye ni katika wao.”[2]

Hivyo haijuzu kujifananisha na washirikina.

3 – Ni shirki kutafuta baraka kupitia mawe, miti na majengo. Haijalishi kitu hata kama mwenye kufanya hivo atayapa majina mengine. Kutafuta baraka kutoka kwa mwengine asiyekuwa Allaah katika mawe, miti, makaburi na mawalii ni shirki ijapo yatapewa majina mengine lisilokuwa shirki.

[1] at-Tirmidhiy (2180), Ahmad (05/218), Ibn Abiy ´Aaswim (76) na Ibn Hibbaan (6702). Ni Swahiyh kwa mujibu wa Ibn Hajar katika “al-Iswaabah” (04/216).

[2] Abu Daawuud (4031) na Ahmad (02/50). Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah amesema: “Mnyororo wake ni mzuri.” (Iqtidhwaa´-us-Swiraatw al-Mustaqiym (01/236-239)). Haafidhw al-´Iraaqiy amesema: “Mlolongo wa wapokezi wake ni Swahiyh.” (Taariykh-ul-Ihyaa’ (02/65)). Haafidhw bin Hajar amesema: “Mlolongo wa wapokezi wake ni mzuri.” (Fath-ul-Baariy (06/98)).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh al-Qawaa´id al-Arba´ah, uk. 31-34
  • Imechapishwa: 18/08/2022