12. Swalah ya usiku na fadhila za kisomo cha Qur-aan


Imewekwa katika Shari´ah kwa waislamu wote kujitahidi aina mbalimbali za ´ibaadah katika mwezi huu mtukufu ikiwa ni pamoja pia na swalah za Sunnah, kusoma Qur-aan kwa mazingatio na kuelewa, kusema “Subhaan Allaah”, “al-Hamdulillaah”, “Laa ilaaha illa Allaah”, “Allaahu Akbar”, Astaghfarullaah”, kusoma du´aa zilizowekwa katika Shari´ah, kuamrisha mema, kukataza maovu, kulingania katika dini ya Allaah (´Azza wa Jall), kuwasaidia mafukara na masikini, kuwatendea wema wazazi, kuwaunga ndugu, kumkirimu jirani, kumtembelea mgonjwa na aina nyenginezo za matendo ya kheri. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Umekujieni mwezi wa Ramadhaan, mwezi wa baraka. Allaah huwafunikeni, huteremsha rehema, hufuta madhambi na huitikia du´aa ndani yake. Allaah hutazama namna mnavyoshindana ndani yake na hujifakhari kwenu mbele ya Malaika Zake. Kwa hivyo muonyesheni Allaah yale mazuri yenu. Hakika mla khasara ni yule mwenye kunyimwa rehema za Allaah.”[1]

Imepokelewa pia ya kwamba (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Atayefanya kitendo cha kheri ndani yake ni kama ambaye amefanya kitendo cha faradhi kwa usiokuwa huo. Mwenye kufanya kitendo cha faradhi ndani yake ni kama ambaye amefanya matendo sabini kwa usiokuwa huo.”[2]

Amesema vilevile (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika Hadiyth Swahiyh:

“Kufanya ´Umrah katika Ramadhaan ni sawa na kuhiji” au alisema “… kuhiji pamoja na mimi.”[3]

Kuna Hadiyth na mapokezi mengi yanayoonyesha kuwa imewekwa katika Shari´ah kushindana katika matendo mema katika mwezi huu mtukufu. Katika matendo hayo ni swalah ya usiku. Ni Sunnah iliyokokotezwa. Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amesema kuhusu waja Wake:

كَانُوا قَلِيلًا مِّنَ اللَّيْلِ مَا يَهْجَعُونَ وَبِالْأَسْحَارِ هُمْ يَسْتَغْفِرُونَ

“… walikuwa kidogo tu katika usiku wakilala kwa raha na kabla ya alfajiri wakiomba maghfirah.”[4]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mwezi mtukufu baada ya Ramadhaan ni mwezi mtukufu wa Allaah Muharram na swalah bora baada ya faradhi ni swalah ya usiku.”[5]

Ameipokea Muslim katika “as-Swahiyh” yake.

Swalah ya usiku ina ngazi kuu. Allaah (Jalla wa ´Alaa) amesema kuhusu waja Wake:

وَالَّذِينَ يَبِيتُونَ لِرَبِّهِمْ سُجَّدًا وَقِيَامًا

“Na wale wanaokesha usiku kwa ajili ya Mola wao wakisujudu na kusimama.”[6]

Amesema (Subhaanah) kuhusu wachaji Allaah:

كَانُوا قَلِيلًا مِّنَ اللَّيْلِ مَا يَهْجَعُونَ وَبِالْأَسْحَارِ هُمْ يَسْتَغْفِرُونَ

“… walikuwa kidogo tu katika usiku wakilala kwa raha na kabla ya alfajiri wakiomba maghfirah.”[7]

 Allaah alisema kumwambia Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

يَا أَيُّهَا الْمُزَّمِّلُ قُمِ اللَّيْلَ إِلَّا قَلِيلًا نِّصْفَهُ أَوِ انقُصْ مِنْهُ قَلِيلًا أَوْ زِدْ عَلَيْهِ وَرَتِّلِ الْقُرْآنَ تَرْتِيلًا إِنَّا سَنُلْقِي عَلَيْكَ قَوْلًا ثَقِيلًا

“Ee uliyejifunika! Simama usiku [uswali] kucha isipokuwa [muda] mdogo tu, nusu yake – au ipunguze kidogo, au izidishe – na soma Qur-aan vizuri ipasavyo. Hakika Sisi tutakuteremshia juu yako kauli nzito.”[8]

Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amesema:

تَتَجَافَىٰ جُنُوبُهُمْ عَنِ الْمَضَاجِعِ يَدْعُونَ رَبَّهُمْ خَوْفًا وَطَمَعًا وَمِمَّا رَزَقْنَاهُمْ يُنفِقُونَ فَلَا تَعْلَمُ نَفْسٌ مَّا أُخْفِيَ لَهُم مِّن قُرَّةِ أَعْيُنٍ جَزَاءً بِمَا كَانُوا يَعْمَلُونَ

“Mbavu zao zinatengana na vitanda wanamuomba Mola wao kwa khofu na matumaini na katika yale tuliyowaruzuku wanatoa. Basi nafsi yoyote haijui yaliyofichiwa katika yanayoburudisha macho. Ni malipo [kwa waumini] kwa yale waliyokuwa wakiyatenda.”[9]

Aayah zinazoonyesha fadhila za swalah ya usiku ni nyingi. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa mara nyingi akiswali swalah ya usiku na akisema:

“Enyi watu! Enezeni Salaam, lisheni chakula, waungeni ndugu na swalini usiku wakati watu wamelala ili muingie Peponi kwa usalama.”[10]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) mara nyingi alikuwa akiswali Rakaa´ kumi na moja na akitoa Tasliym baada ya kila Rakaa´ mbili na akimalizie kwa Witr Rakaa´ moja. Wakati mwingine alikuwa akiweza kuswali Witr Rakaa´ tisa, saba au tano. Lakini (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) mara nyingi alikuwa akiswali Rakaa´ kumi na moja na wakati fulani akiswali Rakaa´ kumi na tatu ambapo anarefusha kisomo, Rukuu´ na Sujuud.

Katika mambo ambayo naiusia nafsi yangu mimi na nyinyi ni kusoma Qur-aan tukufu kwa wingi na kufanya hivo mchana na usiku. Pamoja na mtu kuzingatia na kuelewa maana yake kuu inayosafisha nyoyo na inayotahadharisha kufuata matamanio na nyayo za shaytwaan. Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) ameiteremsha Qur-aan ikiwa ni mwongozo, mawaidha, ikitoa bishara njema, ikitahadharisha, ikifunza, ikielekeza na rehema kwa waja wote. Atayeshikamana nayo na akafuata mwongozo wake ni mwenye furaha na ameokoka. Mwenye kuipa mgongo amekula khasara na ni mwangamivu. Allaah (Ta´ala) amesema:

إِنَّ هَـٰذَا الْقُرْآنَ يَهْدِي لِلَّتِي هِيَ أَقْوَمُ

“Hakika hii Qur-aan inaongoza katika yaliyonyooka kabisa.”[11]

وَأُوحِيَ إِلَيَّ هَـٰذَا الْقُرْآنُ لِأُنذِرَكُم بِهِ وَمَن بَلَغَ

“Na nimefunuliwa Wahy hii Qur-aan ili nikuonyeni kwayo na kila itakayomfikia.”[12]

يَا أَيُّهَا النَّاسُ قَدْ جَاءَتْكُم مَّوْعِظَةٌ مِّن رَّبِّكُمْ وَشِفَاءٌ لِّمَا فِي الصُّدُورِ وَهُدًى وَرَحْمَةٌ لِّلْمُؤْمِنِينَ

“Enyi watu! Hakika yamekujieni mawaidha kutoka kwa Mola wenu na shifaa ya yale yote yaliyomo vifuani, na mwongozo na Rahmah kwa waumini.”[13]

قُلْ هُوَ لِلَّذِينَ آمَنُوا هُدًى وَشِفَاءٌ

“Sema: “Hiyo ni kwa walioamini ni mwongozo na shifaa.””[14]

Katika Hadiyth Swahiyh Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mimi nimekuacheni vizito viwili. Kimoja wapo ni Kitabu cha Allaah. Ndani yake mna uongofu na nuru. Shikeni Kitabu cha Allaah na shikamaneni nacho.”

Kisha akasema:

“Na kizazi changu. Nakukumbusheni Allaah juu ya kizazi changu. Nakukumbusheni Allaah juu ya kizazi changu.”[15]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akashaji´isha na kusisitiza juu ya Kitabu cha Allaah. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika Khutbah ya kuaga:

“Nimekuachieni kitu ambacho lau mtashikamana nacho basi hamtopotea; Kitabu cha Allaah na Sunnah zangu.”[16]

Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Mbora wenu ni yule mwenye kujifunza Qur-aan na akawafunza wengine.”[17]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisema kuwaambia Maswahabah zake:

“Ni nani katika nyinyi anayetaka kwenda Batwhaan au al-´Aqiyq na kuleta ngamia wawili walio na nundu kubwa bila ya kutenda dhambi wala kukata kizazi?” Wakasema: “Sote tunataka, ee Mtume wa Allaah.” Akasema: “Mmoja wenu kwenda msikitini na akajifunza au akasoma Aayah mbili kutoka katika Kitabu cha Allaah ni bora kwake kuliko kupata ngamia wawili, [ngamia] watatu na wane ni bora kuliko [ngamia] wane na ngamia wengine waliobaki.”[18]

Hadiyth zote hizi ni Swahiyh kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kuna Hadiyth na Aayah nyingi na zinazojulikana zinazozungumzia fadhila za Qur-aan na zinazoshaji´isha kuisoma, kujifunza nayo na kuifunza. Makusudio ya kisomo ni kuzingatia Qur-aan na kuelewa maana yake. Baada ya hapo itendewe kazi. Allaah (Ta´ala) amesema:

أَفَلَا يَتَدَبَّرُونَ الْقُرْآنَ أَمْ عَلَىٰ قُلُوبٍ أَقْفَالُهَا

“Je, hawaizingatii Qur-aan au nyoyoni mwao mna kufuli?”[19]

كِتَابٌ أَنزَلْنَاهُ إِلَيْكَ مُبَارَكٌ لِّيَدَّبَّرُوا آيَاتِهِ وَلِيَتَذَكَّرَ أُولُو الْأَلْبَابِ

“Kitabu Tumekiteremsha kwako kikiwa ni chenye baraka ili wapate kuzingatia kwa makini Aayaat zake na ili wapate kukumbuka wale wenye akili.”[20]

Kimbilieni – Allaah akurehemuni – kusoma Kitabu cha Mola Wenu. Zingatieni maana yake. Fanyeni wakati na vikao ijae hayo. Qur-aan tukufu ndio kamba ya Allaah madhubuti na njia iliyonyooka; mwenye kushikamana nayo itamfikisha kwa Allaah na kwenye Pepo Yake. Mwenye kuipa mgongo amekula khasara duniani na Aakhirah.

Tahadharini – Allaah akurehemuni – kutokamana na yote yenye kuzuia na kukushughulisheni na Kitabu cha Allaah katika magazeti, masuhufi na vitabu mfano wa hivo ambavyo madhara yake ni makubwa. Ikiwa kweli mtu analazimka kuyasoma hayo basi ayasome katika wakati maalum. Isitoshe mtu asome tu kiasi cha haja. Mtu atenge wakati maalum wa kusoma na kusikiliza Kitabu cha Allaah. Mtu anatakiwa kusikiliza maneno ya Allaah na kwacho ayaponye maradhi ya moyo wake na kukitumia juu ya kumtii Mola Muumba Wake, Mola na Mfalme ambaye ananufaisha na kudhuru, anayetoa na kuzuia. Hakuna mungu mwingine wa haki isipokuwa Yeye na hakuna Mola asiyekuwa Yeye.

Ni wajibu kujiepusha na vikao vilivyo na mambo ya kipuuzi, nyimbo, idhaa za redio, usengenyaji na kuponda heshima za wengine. Baya na lililo na madhara zaidi ni mambo ya sinema na mfano wa hayo yaliyo na mambo ya uchi. Yanaufanya moyo kuwa mgonjwa na kuuweka moyo mbali na kumdhukuru Allaah na kusoma Qur-aan. Yanasababisha tabia kuwa mbaya na kuachwa tabia nzuri. Ninaapa kwa Allaah kwamba yana madhara kabisa na mambo ya kipuuzi na yanatoa matokeo mabaya. Tahadharini navyo – Allaah akurehemuni – watu wanaojishughulisha navyo na wenye kufurahia matendo yao machafu. Mwenye kuwaita watu katika hayo anapata madhambi yao na madhambi ya wale wenye kupotea kwavyo. Vivyo hivyo kila atayeita katika batili na kupuuzisha haki. Huyu anapata madhambi yake na madhambi ya wataomfuata katika hayo. Yamesihi katika Hadiyth kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Tunamuomba Allaah atuongoze sisi na waislamu wote katika njia iliyonyooka. Hakika Yeye ni Mwenye kusikia na yukaribu. Swalah na salaam zimwendee Mtume wetu Muhammad, kizazi chake na Maswahabah zake.

[1] at-Twabaraaniy katika ”Musnad-ush-Shaamiyyiyn” (2238). Imezuliwa kwa mujibu wa al-Albaaniy  katika ”Dha´iyf-ut-Targhiyb wat-Tarhiyb” (592).

[2] Ibn Khuzaymah (1881) na al-Bayhaqiy katika ”Fadhwaa-il-ul-Awqaat” (1/146). Munkari (Hadiyth dhaifu inayoenda kinyume na Hadiyth Swahiyh) kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”as-Silsilah adh-Dhwa´iyfah” (871).

[3] al-Bukhaariy (1782) na Muslim (1256).

[4] 51:17-18

[5] Muslim (1163).

[6] 25:64

[7] 51:17-18

[8] 73:01-05

[9] 32:16-17

[10] at-Tirmidhiy (2485), Ibn Maajah (3251) na Ahmad (23835). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh-ul-Jaami´” (7865).

[11] 17:09

[12] 06:19

[13] 10:57

[14] 41:44

[15] Muslim (2408).

[16] Muslim (1218) bila ya neno ”… na Sunnah zangu”. Hadiyth imepokelewa kikamilifu na al-Haakim (318) na al-Bayhaqiy (20123). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh-ut-Targhiyb wat-Tarhiyb” (37).

[17] al-Bukhaariy (5027).

[18] Muslim (803).

[19] 47:24

[20] 38:29