Allaah (Subhaanah) amebainisha lengo la kuwaumba majini na watu. Amewaumba kwa lengo moja tu; ambalo ni ´ibaadah. Kwa ajili hiyo ndio maana ameanza kwa njia ya kufupiza na akasema:

وَمَا خَلَقْتُ الْجِنَّ وَالْإِنسَ إِلَّا لِيَعْبُدُونِ

“Sikuumba majini na watu isipokuwa waniabudu.”[1]

Majini na watu hawakuwepo kwa lengo lingine zaidi ya kumwabudu Yeye. Hekima ya kuwepo kwa viumbe si nyingine isipokuwa ni kumwabudu Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Amewaumba majini na watu kwa lengo wamwabudu Yeye na ameumba vyengine vyote kwa ajili ya manufaa yao. Amewawepesishia navyo ili wavitumie katika kumwabudu Yeye (Subhaanahu wa Ta´ala). Maneno Yake (Ta´ala):

إِلَّا لِيَعْبُدُونِ

“… isipokuwa waniabudu.”

Maana yake ni kwamba wampwekeshe Yeye kwa ´ibaadah. Kwa sababu Tawhiyd na ´ibaadah maana zake ni kitu kimoja.

Pamoja na kwamba Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amewaumba wamwabudu Yeye wako ambao wanafanya hivo na wako ambao hawafanyi hivo. Haina maana kwa kuwa amewaumba kwa lengo moja tu kwamba wote watalitekeleza. Wale anaotaka kuwaongoza wanamwabudu na wale anaotaka kuwapotosha wanamkufuru. Kwa hivyo maana ya:

إِلَّا لِيَعْبُدُونِ

“… isipokuwa waniabudu.”

ni kwamba niwaamrishe waniabudu Mimi. Au kwa ajili niwaamrishe na niwakataze. Amesema (Ta´ala):

أَيَحْسَبُ الْإِنسَانُ أَن يُتْرَكَ سُدًى

”Je, anadhani mtu kwamba ataachwa burebure?”[2]

Bi maana asiamrishwe na asikatazwe kitu. Midhali Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amewaamrisha watu na majini wamwabudu Yeye, hii ina maana kwamba ´ibaadah na Tawhiyd ndio msingi na asili.

[1] 51:56

[2] 75:36

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: I´aanat-ul-Mustafiyd bi Sharh Kitaab-it-Tawhiyd, uk. 26-27
  • Imechapishwa: 08/08/2019