12. Kheri na shari zinatokamana na matakwa ya Allaah

Mada hii ni kubwa. Qadariyayh wamepotea ndani yake. Wamegawanyika aina mbili:

1- Wako wanaosema kwamba Allaah hakukadiria kheri wala shari. Kwa mujibu wao wanaona kuwa waja wenyewe ndio wenye kukadiria matendo yao, ya kheri na ya shari.

2- Wako wanaosema kwamba Allaah anakadiria kheri tupu na si shari. Pote hili wanaifanya akili ni yenye kuhukumu dalili na ndio maana wamepotea.

Pote hili lililoangamia limekabiliwa na pote lingine ambalo nalo limeangamia lililochupa mipaka katika kuthibitisha matendo ya Allaah kiasi cha kwamba wakakanusha matendo ya viumbe. Wanaitwa Jabriyyah. Wanasema kwamba mja ametenzwa nguvu katika matendo yake na kwamba hana uwezo wala khiyari. Wanasema ni kama upepo. Wamemfananisha na mti ambao unapelekwa na upepo kuliani na kushotoni pasi na uwezo wala kutaka.

Haki ni kwamba mja ana jukumu juu ya matendo yake na anafanya kheri na shari kwa uwezo na kutaka kwake mwenyewe chini ya utashi wa Allaah. Mja anafanya mema na maovu kwa kutaka kwake mwenyewe chini ya utashi uliofungamana na utashi wa Allaah. Allaah ndiye mwenye kumuumba mtendaji na matendo yake, mema na maovu. Elewa haya na yakite. Mja hakutezwa nguvu. Kwa sababu Allaah amempa uwezo, khiyari na matakwa yaliyo chini ya matakwa ya Allaah (´Azza wa Jall). Akifanya mambo ya kheri, basi ni kutokana na fadhilah na rehema za Allaah na kisha ni kutokana na kitendo chake mwenyewe na chumo lake ambalo Allaah anamlipa kwacho Akifanya shari, ni kutokana na hekima na uadilifu wa Allaah na kisha ni kutokana na kitendo chake mwenyewe ambacho ataadhibiwa kwacho. Hii ndio ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah katika maudhui haya. Hawako kama Qadariyyah wapindukaji ambao wamekanusha matendo ya Allaah (´Azza wa Jall) kama ambavo hawako kama Jabriyyah ambao wamechupa mipaka katika kuthibitisha matendo ya Allaah (´Azza wa Jall) mpaka wakakanusha matendo ya viumbe. Kwa mtazamo wa Jabriyyah ni kwamba matendo ya mja yananasibishwa kwake kimafumbo na si kihakika. Fikira yao inapelekea kwamba mtenda dhambi anaadhibiwa kwa dhuluma kwa sababu ametenzwa kutenda dhambi hiyo.

Kama tulivosema Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah wako kati na kati. Wanathibitisha kwamba mja ni mtenda wa kikweli na kwamba Allaah amekadiria makadirio yote. Amemuumba mja na akaumba matendo yake. Matendo, ni mamoja ya kheri na shari, kuthibitishwa kwa mja inahusiana na kule kuyachuma kwa kutaka kwake, pamoja na kwamba hayatoki nje ya matakwa ya Allaah:

وَمَا تَشَاءُونَ إِلَّا أَن يَشَاءَ اللَّـهُ رَبُّ الْعَالَمِينَ

”Hamtotaka isipokuwa atake Allaah, Mola wa walimwengu.”[1]

Kuyanasibisha mambo ya kheri na ya shari kwa Allaah ni kwa njia ya kuyaumba, kuyafanya yakapatikana na kuyakadiria. Shari tupu hainasibishwi kwa Allaah kwa sababu matendo yote ya Allaah ni yenye hekima na ni mazuri. Kwa ajili hiyo shari hainasibishwi Kwake kama shari – inanasibishwa kwa waja walioifanya na kuichuma. Hata hivyo Allaah ameikadiria. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Shari hainasibishwi Kwako.”[2]

  Bi maana Allaah si mwenye kuiridhia, kuiamrisha wala kuridhia wale wenye kuifanya. Amesema (´Azza wa Jall):

إِن تَكْفُرُوا فَإِنَّ اللَّـهَ غَنِيٌّ عَنكُمْ ۖ وَلَا يَرْضَىٰ لِعِبَادِهِ الْكُفْرَ ۖ وَإِن تَشْكُرُوا يَرْضَهُ لَكُمْ

“Mkikufuru, basi hakika Allaah ni mkwasi kwenu, na wala haridhii kwa waja Wake ukafiri na mkishukuru huridhika nanyi.”[3]

[1] 81:29

[2] Muslim (771).

[3] 39:07

  • Mhusika: ´Allaamah Zayd bin Muhammad al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Latwiyfah ´alaa Usuwl-is-Sunnah al-Muniyfah, uk. 60-62
  • Imechapishwa: 03/10/2019