12. Dalili kuthibitisha matakwa ya mja na kwamba hayatoki nje ya matakwa ya Allaah

Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah wako kati na kati, kama ilivyo kawaida yao katika mambo yote ya dini wako kati na kati, wakathibitisha kuwa mja kutenda, matakwa na khiyari. Lakini hata hivyo mambo hayo hayatoki nje ya matakwa na utashi wa Allaah. Hivyo wakamthibitishia mja matakwa, khiyari, utashi na kutenda, tofauti na Jabriyyah. Lakini mambo hayo hayatoki nje ya mipango na makadirio ya Allaah, tofauti na Qadariyyah. Hivi ndivo zinafahamisha dalili kutoka katika Qur-aan na Sunnah. Lau mja asingekuwa na matakwa, kutaka mwenyewe na uwezo basi Allaah asingelimuadhibu juu ya matendo yake. Angelikuwa ni mwenye kutenzwa nguvu – kama wanavoamini Jabriyyah – basi asingemuadhibu juu ya matendo ambayo hana kutaka kwake mwenyewe.

Miongoni mwa dalili za Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah ni maneno Yake (Ta´ala):

لِمَن شَاءَ مِنكُمْ أَن يَسْتَقِيمَ وَمَا تَشَاءُونَ إِلَّا أَن يَشَاءَ اللَّـهُ رَبُّ الْعَالَمِينَ

“Kwa yule atakaye miongoni mwenu anyooke – na hamtotaka isipokuwa atake Allaah Mola, wa walimwengu.”[1]

Maneno Yake:

لِمَن شَاءَ مِنكُمْ أَن يَسْتَقِيمَ

“Kwa yule atakaye miongoni mwenu anyooke.”

ni dalili inayoonyesha kuwa mja ananyooka juu ya kumtii Allaah kwa kutaka kwake mwenyewe. Halazimishwi juu ya jambo hilo. Ima akanyooka na ima akaasi. Yeye ndiye mwenye kuamini na yeye huyohuyo ndiye mwenye kukufuru. Yeye ndiye muumini, kafiri, fasiki, mzinifu, mwizi na mnywaji pombe. Mwenye kuyafanya hayo kwa kutaka kwake mwenyewe. Amemthibitishia mja kutaka pale aliposema:

لِمَن شَاءَ مِنكُمْ أَن يَسْتَقِيمَ

“Kwa yule atakaye miongoni mwenu anyooke.”

Kisha akasema:

وَمَا تَشَاءُونَ إِلَّا أَن يَشَاءَ اللَّـهُ رَبُّ الْعَالَمِينَ

“Hamtotaka isipokuwa atake Allaah Mola, wa walimwengu.”

Hii ni Radd kwa Qadariyyah. Sehemu ya kwanza ya Aayah ni Radd kwa Jabriyyah na sehemu ya mwisho ya Aayah ni Radd kwa Qadariyyah. Kwa hivyo Aayah inawaraddi mapote hayo mawili. Ndani ya Aayah kuna Radd juu ya mapote mawili. Maneno Yake:

لِمَن شَاءَ

“Kwa yule atakaye… “

Hapa kuna Radd kwa Jabriyyah ambao wanapinga mja kutaka na kwamba anaendeshwa pasi na kutaka kwake mwenyewe. Maneno Yake:

إِلَّا أَن يَشَاءَ اللَّـهُ

“… isipokuwa atake Allaah.”

Hapa kuna Radd kwa Qadariyyah ambao wanapinga Qadar na wanachupa mpaka katika kuthibitisha kutaka kwa mja na wanasema kuwa mja hutaka ijapokuwa Allaah hakutaka wala kukadiria. Yeye hufanya na kutaka kwa kuanza kwake mwenyewe. Baadhi yao husema kuwa Allaah hayajui mambo isipokuwa baada ya kutokea kwake. Hawa ndio wachupaji mpaka. Baadhi yao husema kwamba huyajua lakini hayakadirii. Huu ndio ufupi wa utafiti katika masuala haya.

[1] 81:28-29

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh ´Aqiydat-il-Imaam Mujaddid Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab, uk. 31-32
  • Imechapishwa: 04/03/2021