111. al-Qummiy upotoshaji wake wa tatu wa al-Maa-idah


al-Qummiy amesema:

“Kuhusiana na maneno Yake:

الْيَوْمَ أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ وَأَتْمَمْتُ عَلَيْكُمْ نِعْمَتِي وَرَضِيتُ لَكُمُ الْإِسْلَامَ دِينًا

“Leo Nimekukamilishieni dini yenu na nimekutimizieni neema Yangu na nimekuridhieni kwenu Uislamu iwe dini yenu.”[1]

baba yangu alinihadithia, kutoka kwa Swafwaan bin Yahyaa, kutoka kwa al-´Alaa´, kutoka kwa Muhammad bin Muslim, kutoka kwa Abu Ja´far ambaye amesema: “Uongozi ndio ilikuwa faradhi ya mwisho aliyoteremsha Allaah. Hakuna faradhi nyingine iliyoteremshwa baada ya hapo[2]. Kisha akateremsha:

الْيَوْمَ أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ وَأَتْمَمْتُ عَلَيْكُمْ نِعْمَتِي وَرَضِيتُ لَكُمُ الْإِسْلَامَ دِينًا

“Leo Nimekukamilishieni dini yenu na nimekutimizieni neema Yangu na nimekuridhieni kwenu Uislamu iwe dini yenu.”[3]

Kiraa´-ul-Ghamm. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliisoma Juhfah. Baada ya hapo hakukuteremshwa faradhi zengine.”[4]

Ndani ya Aayah hii kuna neema kubwa ya Allaah juu ya Ummah huu na khaswa khaswa Maswahabah wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) walio-onja neema hii, wakaishuhudia na wakakutana nayo. Maswahabah walishinda juu ya maadui, Uislamu ukazishinda dini zote na ukakamilishwa kutokana na I´tiqaad zake na Shari´ah zake zinazokusanya hukumu za dunia na Aakhirah.

Iliteremshwa katika hajj ya kuaga takriban siku mia moja kabla ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kufariki. Zaidi ya Maswahabah laki moja walihudhuria hajj hii. Aayah inawazungumzisha wao wote na ni neema kwao wote.

Wasomi wa kiyahudi walielewa ukubwa wa neema hii juu ya Maswahabah wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na juu ya Ummah huu. Kuna mmoja wao alimwambia kiongozi wa waumini ´Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anh):

“Ee kiongozi wa waumini! Lau Aayah hii:

الْيَوْمَ أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ وَأَتْمَمْتُ عَلَيْكُمْ نِعْمَتِي وَرَضِيتُ لَكُمُ الْإِسْلَامَ دِينًا

“Leo Nimekukamilishieni dini yenu na nimekutimizieni neema Yangu na nimekuridhieni kwenu Uislamu iwe dini yenu.”[5]

ingelituteremkia sisi basi tungeliifanya siku hiyo kuwa sikukuu.” Ndipo ´Umar (Radhiya Allaahu ´anh) akasema: “Najua ni siku gani iliteremshwa; iliteremshwa siku ya ´Arafah siku ya ijumaa.”[6]

Kwa kifupi ni kwamba Aayah hii inawazungumzisha Maswahabah na ni neema ya Allaah kwao. Walimuamini Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na wakaonja utamu wa imani.  Athari ya Qur-aan ilidhihiri kwao. I´tiqaad zao, ´ibaadah zao na mapambano yao yalikuwa ni yenye kuafikiana na Qur-aan. Walijitolea nafsi zao na mali zao kwa njia mbalimbali. Waliitendea kazi Aayah moja moja. Kadhalika ndivyo ilikuwa msimamo wao inapokuja katika Sunnah. Allaah amewasifu katika Aayah nyingi. Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amewasifu katika mamia ya Hadiyth – mmoja mmoja na kwa pamoja.

Yote haya yanawachukiza Raafidhwah Baatwiniyyah. Katika hayo ni maneno Yake (Ta´ala):

ُّحَمَّدٌ رَّسُولُ اللَّـهِ ۚ وَالَّذِينَ مَعَهُ أَشِدَّاءُ عَلَى الْكُفَّارِ رُحَمَاءُ بَيْنَهُمْ ۖتَرَاهُمْ رُكَّعًا سُجَّدًا يَبْتَغُونَ فَضْلًا مِّنَ اللَّـهِ وَرِضْوَانًا ۖ سِيمَاهُمْ فِي وُجُوهِهِم مِّنْ أَثَرِ السُّجُودِ ۚ ذَٰلِكَ مَثَلُهُمْ فِي التَّوْرَاةِ ۚ وَمَثَلُهُمْ فِي الْإِنجِيلِ كَزَرْعٍ أَخْرَجَ شَطْأَهُ فَآزَرَهُ فَاسْتَغْلَظَ فَاسْتَوَىٰ عَلَىٰ سُوقِهِ يُعْجِبُ الزُّرَّاعَ لِيَغِيظَ بِهِمُ الْكُفَّارَ

“Muhammad ni Mtume wa Allaah. Na wale walio pamoja naye ni wakali zaidi dhidi ya makafiri wanahurumiana baina yao. Utawaona wakirukuu na wakisujudu wakitafuta fadhila na radhi kutoka kwa Allaah. Alama zao dhahiri zi katika nyuso zao kutokana na athari za sujudu. Huo ni mfano wao katika Tawraat na mfano wao katika Injiyl kama mmea umetoa chipukizi lake, likautia nguvu kisha likawa nene, kisha likasimama sawasawa juu ya shina lake liwapendezeshe wakulima ili liwaghadhibishe makafiri.”[7]

Hawa ndio Maswahabah wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambao Raafidhwah wanawachukia hali ya juu na vibaya sana. Imaam Maalik na wengineo wamewakufurisha kwa kutumia Aayah hii kwa sababu hakuna wengine wanaowachukia na kuwabughudhi Maswahabah wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kama wanavofanya wao. Hakuna yeyote anawachukia na kuwatuhumu kuikengeusha Qur-aan kama wao. Wameyatupilia mbali mapokezi ya Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kwa ajili hiyo wakawa na dini nyingine iliyojengeka juu ya uongo na ni dini iliyo na migongano mikubwa na dini ya haki ambayo Allaah amemteremshia nayo Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na ikaaminiwa na Maswahabah na wale waliowafuata kwa wema.

[1] 05:03

[2] Allaah hakuteremsha dalili yoyote juu ya uongozi huu. Ni Shaytwaan ndiye alikuteremshieni ili muweze kuipotosha Qur-aan na kuwakufurisha Maswahabah wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

[3] 05:03

[4] Tafsiyr al-Qummiy (1/162).

[5] 05:03

[6] al-Bukhaariy (7268) na Ahmad (1728).

[7] 48:29

  • Mhusika: ´Allaamah Rabiy´ bin Haadiy al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Intiswaar li Kitaab-il-´Aziyz al-Jabbaar, uk. 158-160
  • Imechapishwa: 23/04/2018