Miongoni mwa baraka za Shaam ni kwamba nuru ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wakati wa kuzaliwa kwake iliangaza juu yake na kasiri yake ikaanza kuangaza. Ilikuwa ndio mwanzo wa kuingia nuru yake Shaam. Halafu kukaingia nuru ya dini na kitabu chake na ikaangaza na ikasafisha shirki na maasi yaliyokuwemo ndani yake. Kwa hiyo utukufu na baraka za Shaam zikawa zimetimia.

80- Imaam Ahmad na al-Haakim wamepokea kupitiak wa al-´Irbaadhw bin Saariyah ambaye kamsikia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema:

“Mimi ni mja wa Allaah na Mtume wa mwisho na hakika Aadam alilowekwa kwenye udongo. Nitakuelezeni hilo; du´aa ya baba yangu Ibraahiym, bishara ya ´Iysaa juu yangu na mtazamo wa mama yangu.”

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alizaliwa Makkah na huko ndiko alianza utume wake. Kitabu aliteremshiwa Makkah. Halafu akasafirishwa usiku kutoka msikiti Mtakatifu kwenda msikiti wa Aqswaa Shaam. Halafu akarejea Makkah ambapo akahajiri kwenda al-Madiynah. Mwishoni mwa uhai wake akawaandikia Shaam, Hirakli na wengi ambao wako chini yake. Halafu akatoka kwa nafsi yake katika vita vya Tabuuk kisha akarejea. Kisha akaagiza kikosi kwenda Mu´tah na jeshi la Usaamah. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akafa kabla ya wao kuwahi kutoka. Baada ya hapo Abu Bakr as-Swiddiyq akaanza kuiteka Shaam na operesheni hiyo ikakamilishwa wakati wa ´Umar (Radhiya Allaahu ´anh).

81- Abul-Aswad al-Qurashiy ameeleza kutoka kwa ´Urwah ambaye amesema kuwa Abu Bakr alimwandikia Khaalid bin al-Waliyd:

“Harakisheni mje kwa ndugu zenu Shaam! Ninaapa kwa Allaah napendelea zaidi kijiji katika ardhi Takatifu ambacho Allaah anakifungua kupitia kwetu kuliko sehemu yote ya nchi ya Iraq.”

82- Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema kuwa hakitosimama Qiyaamah kabla ya kujitokeza kwa moto kutoka Hijaaz na utaangazia shingo za ngamia Baswrah. al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kupitia kwa Abu Hurayrah ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Qiyaamah kabla ya kujitokeza kwa moto kutoka Hijaaz na utaangazia shingo za ngamia Baswrah.”[1]

Moto huu ulijitokeza katika bonde nje kidogo na mji wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) mwaka 654. Jambo lake lilienea na usiku huo mwanga wa moto ulikuwa unaweza kuonekana kwenye shingo za ngamia Baswrah. Muda kidogo baadaye Iraq ikashindwa kwa tukio lilitokea Baghdaad. Makafiri wengi wakaingia ndani ya mji na khalifah wa Banul-´Abbaas na wafuasi wake wengi wakauawa. Kwa ajili hiyo kukawepo uharibifu mashariki kupitia mikono na wamongolia. Baada ya hapo wairaki wengi na walio bora wakahamia Shaam. Ikapelekea Shaam kuzidi kuwa kubwa, wakawa wengi wakazi wake na ikaenea elimu ya utume iliyorithiwa kutoka kwa Mtume wa mwisho (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Katika zama za mwisho kutatokea moto ambao utawakusanya watu wote kuelekea Shaam. Hiyo ndio alama ya kwanza ya Qiyaamah.

83- al-Bukhaariy amepokea kupitia kwa Anas ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Alama ya kwanza ya Qiyaamah ni moto utaojitokeza mashariki na kuwakusanya magharibi.”[2]

Wakati huo watu wote watakusanyika Shaam. Shaam ndio sehemu ya mkusanyiko na sehemu ya kufufuliwa. Kisha ndio kutokee Qiyaamah.

[1] al-Bukhaariy (7118) na Muslim (2902).

[2] al-Bukhaariy (3938).

  • Mhusika: Imaam ´Abdur-Rahmaan bin Rajab al-Baghdaadiy al-Hanbaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fadhwaa-il-ush-Shaam, uk. 93-96
  • Imechapishwa: 10/02/2017