Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Amesema (Ta´ala):

وَمَا خَلَقْتُ الْجِنَّ وَالْإِنسَ إِلَّا لِيَعْبُدُونِ

“Sikuumba majini na watu isipokuwa waniabudu.”[1]

MAELEZO

Zingatia kutilia umakini wa Shaykh (Rahimahu Allaah) wakati alipofuatishia “Kitabu cha Tawhiyd” kwa Aayah hii. Lengo ni kuweka wazi maana ya Tawhiyd, ambayo ni kumpwekesha Allaah kwa ´ibaadah. Tawhiyd maana yake sio kukubali uola wa Allaah. Bali maana yake ni kumpwekesha Allaah kwa ´ibaadah. Dalili ya hilo ni Aayah hii. Vilevile Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amebainisha hekima ya kuwaumba majini na watu.

Majini ni walimwengu wasioonekana. Tunawaamini japokuwa hatujawaona.

إِنَّهُ يَرَاكُمْ هُوَ وَقَبِيلُهُ مِنْ حَيْثُ لَا تَرَوْنَهُمْ

“Hakika yeye anakuoneni, yeye na kabila lake, hali ya kuwa nyinyi hamuwaoni.”[2]

Ni wajibu kuamini juu ya uwepo wao. Yule mwenye kupinga hilo ni kafiri, kwa sababu amemkadhibisha Allaah, Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na maafikiano ya Ummah juu ya kuwepo kwa majini. Hawa ambao wanapinga uwepo wao dalili yao ni ipi? Hawana dalili nyingine isipokuwa tu ni kwa sababu hawawaoni. Je, wewe unakiona kila kilichopo? Kuna vitu vingi vilivyopo ambavyo huvioni. Je, wewe unaiona roho? Wewe unaziona akili zako? Si lazima ukione kila kitu kilichopo. Vipo vitu vingi visivyodhibitika ambavyo hatuvioni. Pengine hata vitu hivyo vinaishi kati yetu. Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) ni Mwenye hekima na miongoni mwa hekima Zake ni majini. Majini ni ulimwengu mkubwa ambao hatuuoni. Wao wamelazimishwa ´ibaadah kama watu.

[1] 51:56

[2] 07:27

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: I´aanat-ul-Mustafiyd bi Sharh Kitaab-it-Tawhiyd, uk. 26
  • Imechapishwa: 08/08/2019