11. Dalili juu ya masuala mane aliyotaja Shaykh


Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Suala la nne: Kusubiri juu ya maudhi yatakayompata mtu ndani yake.

Dalili ni Kauli Yake (Ta´ala):

وَالْعَصْرِ إِنَّ الْإِنسَانَ لَفِي خُسْرٍ إِلَّا الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ وَتَوَاصَوْا بِالْحَقِّ وَتَوَاصَوْا بِالصَّبْرِ

“Naapa kwa al-‘Aswr. Hakika ya mwanaadamu bila ya shaka yumo katika khasara. Isipokuwa wale walioamini na wakatenda mema na wakausiana kwa kufuata ya haki na wakausiana kuwa na subira.”[1]

MAELEZO

Masuala haya mane ni lazima uyasome kwa upambanuzi. Je, kuna dalili juu ya yale yaliyosemwa na Shaykh? Masuala haya mane ni wajibu kwetu kujifunza nayo. Ametuahidi kuwa hatosema kitu isipokuwa kwa dalili. Dalili iko wapi? Amesema kwamba dalili ya hayo ni maneno Yake (Ta´ala):

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَنِ الرَّحِيم

Kwa jina la Allaah, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.

وَالْعَصْرِ إِنَّ الْإِنسَانَ لَفِي خُسْرٍ إِلَّا الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ وَتَوَاصَوْا بِالْحَقِّ وَتَوَاصَوْا بِالصَّبْرِ

“Naapa kwa al-‘Aswr. Hakika ya mwanaadamu bila ya shaka yumo katika khasara. Isipokuwa wale walioamini na wakatenda mema na wakausiana kwa kufuata ya haki na wakausiana kuwa na subira.”

Isipokuwa wale walioamini – Hili ndio suala la kwanza. Kwa sababu imani haiwi isipokuwa kwa elimu ambayo ni kumtambua Allaah (´Azza wa Jall), kumjua Mtume Wake na kuijua dini ya Uislamu kwa dalili.

Suala la pili: Wakatenda mema – Huku ndio kuitendea kazi elimu.

Suala la tatu: Wakausiana kwa kufuata ya haki – Huku ndio kulingania katika elumu na matendo.

Suala la nne: Wakausiana kuwa na subira – Wakausiana kuwa na subira juu ya maudhi katika njia ya ulinganizi katika elimu na matendo.

Maneno Yake:

وَالْعَصْرِ

“Naapa kwa al-‘Aswr.”

Ni kiapo. Makusudio ni wakati na zama. Allaah (Ta´ala) ameapa kwa zama na wakati ambavyo vimeumbwa. Allaah (Jalla wa ´Alaa) anaapa kwa atakavyo katika viumbe. Viumbe hawaapi isipokuwa kwa Allaah. Allaah haapi isipokuwa kwa kitu kilicho na umuhimu. Ndani yake kuna alama miongoni mwa alama Zake (Subhaanahu wa Ta´ala). Zama hizi ndani yake kuna mazingatio na umuhimu. Ndio maana Allaah akaapa kwa ´Aswr, akaapa kwa usiku unapoingia na akaapa kwa wakati wa asubuhi.

Viumbe wao hawafai kuapa isipokuwa kwa Allaah pekee. Haijuzu kwetu kuapa kwa asiyekuwa Allaah. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Mwenye kuapa kwa mwengine asiyekuwa Allaah amekufuru au ameshirikisha.”[2]

“Mwenye kuapa basi aape kwa Allaah au anyamaze.”[3]

Allaah anaapa kwa atakacho na wala haapi isipokuwa kwa kitu kilicho na umuhimu na ndani yake mna mazingatio. Mna mazingatio yepi katika zama hizi? Mazingatio ni makubwa ambapo mchana unapishana na usiku ambapo kimoja kinafunika kingine. Kimoja kinakuwa kirefu na kingine kinakuwa kifupi. Vinafuatana katika mpangilio huu wa ajabu ambao hauchelewi wala kubadilika. Hii ni dalili inayoonyesha uwezo wa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Jengine yale yanayopitika katika wakati huu katika matukio mbalimbali kukiwemo majanga, misiba, neema na kheri. Yale yanayopitika katika wakati huu ni miongoni mwa mazingatio. Vivyo hivyo usiku na mchana ndipo kunapitika matendo mema. Amesema (Ta´ala):

وَهُوَ الَّذِي جَعَلَ اللَّيْلَ وَالنَّهَارَ خِلْفَةً

“Naye ndiye amejaalia usiku na mchana ufuatane… “

Bi maana vinapishana kimoja kinafunika kingine:

لِّمَنْ أَرَادَ أَن يَذَّكَّرَ أَوْ أَرَادَ شُكُورًا

“… kwa atakaye kukumbuka au atakaye kushukuru.”[4]

Katika baadhi ya visomo imekuja:

لِمَنْ أَرَادَ أَنْ يَذَّكَّرَ

“… kwa atakaye kukumbuka.”

[1] 103:01-03

[2] Abu Daawuud (3251) na at-Tirmidhiy (1535).

[3] al-Bukhaariy (6108) na Muslim (1646) (03).

[4] 25:62

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 28-31
  • Imechapishwa: 24/11/2020