107. Kuwasomea al-Faatihah wafu na waliohai baada ya swalah


Swali 107: Je, inafaa kuwasomea al-Faatihah wafu wote na waliohai – nakusudia Mitume, mashahidi, mawalii na waumini wengine waliobakia na ndugu jamaa – baada ya kumaliza kuswali au katika wakati wowote[1]?

Jibu: Hili halina msingi katika Shari´ah takasifu. Haikuwekwa katika Shari´ah kumsomea al-Faatihah yoyote. Kwa sababu hili halikupokelewa kutoka kwa yeyote katika Maswahabah. Hivyo halina msingi wowote.

Baadhi ya wanazuoni wameona kuwa hapana kizuizi kumtumia thawabu za kisomo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na mtu mwengine. Lakini ni maoni yasiyokuwa na dalili. Tahadhari zaidi ni kuacha kufanya hivo. Kwa sababu ´ibaadah ni kwa mujibu wa dalili katika Qur-aan na Sunnah. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yeyote atakayefanya kitendo kisichoafikiana na amri yetu basi atarudishiwa mwenyewe.”[2]

Lakini inapasa kumswalia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa wingi, kuwaombea du´aa wazazi wawili na ndugu jamaa. Du´aa ni yenye kunufaisha.

Kuhusu kumsomea kisomo cha al-Faatihah Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) au mtu mwengine ni jambo halikusuniwa kwa mujibu wa maoni sahihi zaidi ya wanazuoni kutokana na Hadiyth iliyotajwa:

“Yeyote atakayefanya kitendo kisichoafikiana na amri yetu basi atarudishiwa mwenyewe.”

[1] Majmuu´-ul-Fataawaa (13/279-280).

[2] Muslim (1718).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam-ul-Janaa-iz, uk. 77-78
  • Imechapishwa: 09/01/2022