106. Kuchukua malipo kwa kumsomea Qur-aan maiti


Swali 106: Tuna watu huku kwetu Yemen wanawasomea Qur-aan wafu na wanachukua malipo juu ya hilo. Je, wafu wanafaidika chochote? Anapofariki mmoja katika wao basi wanasoma Qur-aan kwa muda wa siku tatu na wanafanya vichinjwa na chakula. Je, haya yamo katika Shari´ah[1]?

Jibu: Kusoma Qur-aan kwa ajili ya wafu ni Bid´ah. Aidha kuchukua malipo juu ya hilo. Haikupokelewa katika Shari´ah takasifu yanayojulisha juu ya hayo. ´Ibaadah ni kwa mujibu wa dalili kutoka katika Qur-aan na Sunnah na haijuzu kutoka humo isipokuwa yale Allaah aliyoyawekea Shari´ah.  Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yeyote atakayezua katika amri yetu hii yale yasiyokuwemo basi atarudishiwa mwenyewe.”[2]

Kuna maafikiano juu ya usahihi wake.

Vivyo hivo kuchinja vichinjwa na kupika chakula kwa ajili ya maiti yote ni Bid´ah na maovu na hayajuzu. Ni mamoja hayo yatafanyika kwa muda wa siku moja au siku nyingi. Kwa sababu Shari´ah takasifu haikuyapokea. Bali ni miongoni mwa matendo katika kipindi cha kikafiri. Imethibiti kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwamba amesema:

“Mambo mane katika Ummah wangu ni miongoni mwa mambo ya kipindi cha kikafiri na hawatoyaacha; kujifakhari kwa unasabu, kutukaniana nasabu, kuinasibisha mvua kwa nyota na kuomboleza.”

Vilevile amesema:

“Mwanamke mwenye kuomboleza ikiwa hakutubia kabla ya kufa kwake, basi atafufuliwa siku ya Qiyaamah na huku akiwa amevishwa nguo ya shaba iliyoyeyuka na kanzu ya ukoma.”[3]

Ameipokea Muslim katika “as-Swahiyh” yake.

Jariyr bin ´Abdillaah al-Bajaliy (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia:

“Tulikuwa tukizingatia kukusanyika nyumbani kwa maiti na kutengeneza chakula baada ya kuzika ni katika kuomboleza.”[4]

Ameipokea Imaam Ahmad kwa cheni ya wapokezi nzuri.

Miongoni mwa hayo ni maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Mambo mane katika Ummah wangu ni miongoni mwa mambo ya kipindi cha kikafiri na hawatoyaacha; kujifakhari kwa unasabu, kutukaniana nasabu, kuinasibisha mvua kwa nyota na kuomboleza.”

Haikuwa ni katika matendo yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wala matendo ya Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum) ya kwamba anapofariki maiti wanamsomea Qur-aan, wanamchinjia, kumfanyia matanga, chakula au sherehe. Yote haya ni Bid´ah. Ni lazima kutahadhari na kuwatahadharisha watu kutokamana na hayo.

Ni lazima kwa wanazuoni kwa njia maalum kuwakataza watu juu ya yale ambayo Allaah amewaharamishia na wawashike mkono wajinga na wapumbavu mpaka wanyooke juu ya njia ilionyooka ambayo Allaah amewawekea Shari´ah waja Wake. Kwa njia hiyo zitatengemaa hali na jamii na itashinda hukumu ya Kiislamu na yatapotea mambo ya kipindi cha kikafiri.

Kilichosuniwa ni familia ya mfiwa watengenezewe chakula kitachoagizwa na majirani au jamaa zake. Kwa sababu wakati Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipopata khabari za kufariki kwa Ja´far bin Abiy Twaalib (Radhiya Allaahu ´anh) alisema kuwaambia ahli zake:

“Watengenezeeni familia ya Ja´far chakula. Kwani hakika wamefikwa na kitu kinachowashughulisha.”[5]

Ameipokea Imaam Ahmad na watunzi wa Sunan kwa cheni ya wapokezi Swahiyh.

[1] Majmuu´-ul-Fataawaa (13/263-265).

[2] al-Bukhaariy (2697) na Muslim (1718).

[3] Muslim (934).

[4] Ahmad (6866) na Ibn Maajah (1612).

[5] Ahmad (1754), Ibn Maajah (1610), at-Tirmidhiy (998) na Abu Daawuud (3132).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam-ul-Janaa-iz, uk. 75-77
  • Imechapishwa: 10/01/2022