100. Hitimisho


Mwandishi (Rahimahu Allaah) amesema:

Midhali utaendelea daima kuyaitakidi haya

     basi wewe utakuwa katika kheri jioni na asubuhi

MAELEZO

Hutokuwa miongoni mwa wale wanaoamka asubuhi hali ya kuwa ni waumini na ikifika jioni ni makafiri au wanaingiliwa na jioni wakiwa ni waumini na wanapambazukiwa wakiwa ni makafiri. Yote haya kwa sababu ya fitina. Usiwe hivyo kwa sababu uko katika mfumo wa Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah. Hili ndio kundi lililookoka. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Utafarikiana Ummah huu katika mapote sabini na tatu. Yote yataingia Motoni isipokuwa moja.”[1]

Limeitwa kuwa “limeokoka” kwa sababu limeokoka na Moto na halikuanguka na mapote yanayoenda kinyume. Wameitwa Ahl-us-Sunnah kwa sababu wanazitendea kazi Sunnah za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kutokamana na maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Jilazimieni na Sunnah zangu.”

Wameitwa “al-Jamaa´ah” kwa sababu ni wenye kukusanyika wala hawatofautiani. Miongoni mwa sifa za Ahl-ul-Haqq ni kuwa wanakusanyika na miongoni vilevile mwa sifa za watu wa batili ni kuwa wanafarikiana na kutofautiana.

Allaah amjaze kheri mshairi juu ya Uislamu na waislamu. Tunamuomba Atunufaishe na yale aliyoyataja, atuthibitishe sisi, nyinyi na waislamu katika neno la haki na kulitendea kazi mpaka siku tutakutana Naye.

Mpaka hapa ndio mwisho wa upambanuzi wa shairi hili lililobarikiwa. Na Allaah ndiye mjuzi zaidi.

Swalah na salaam zimwendee Muhammad, kizazi chake na Maswahabah zake. Himdi zote zinamstahikia Allaah, Mola wa walimwengu.

[1] Abu Daawuud (4597) na wengineo